Sura ya 1
Jinsi Tulivyopata Kitabu cha Mormoni
Wakati Joseph alipokuwa na umri wa miaka 14, makanisa mengi yalidai kuwa ya kweli, na hakujua ni lipi angejiunga nalo.
Siku moja Joseph alisoma Yakobo 1:5 katika Biblia: “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu.” Joseph alitaka kujua ni kanisa gani lilikuwa la kweli, kwa hiyo aliamua kumuuliza Mungu.
Asubuhi moja ya majira ya kuchipua, Joseph alikwenda msituni karibu na nyumbani kwake kusali.
Wakati Joseph alipopiga magoti na kuanza kusali, Shetani alijaribu kumzuia. Joseph alisali kwa nguvu zaidi, akimwomba Baba wa Mbinguni msaada.
Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walimjia Joseph Smith katika nguzo ya mwanga. Baba wa Mbinguni alimwonyesha Yesu na akasema: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”
Joseph aliuliza ni kanisa gani angejiunga nalo. Yesu alimwambia asijiunge na kanisa lolote kwani yote yalikuwa si sahihi.
Wakati Joseph alipowaambia baadhi ya watu kile alichokuwa ameona na kusikia, walimcheka. Viongozi wengi wa makanisa yaliyokuwa katika eneo lake walimtesa.
Miaka mitatu ilipita. Usiku mmoja Joseph alikuwa akisali kwa ajili ya msamaha wa dhambi zake na kwa ajili ya kujua kile alichohitajika kukifanya.
Malaika kwa jina Moroni alimtokea na kumwambia Joseph kuhusu kitabu ambacho kilikuwa kimeandikwa kwenye bamba za dhahabu. Joseph alitakiwa kuzitafsiri bamba hizi kwa Kiingereza.
Wakati Moroni alipoondoka, Joseph aliwaza kuhusu kile ambacho Moroni alikuwa amemwambia yeye. Moroni alirudi tena mara mbili zaidi usiku huo.
Siku iliyofuata Joseph alikwenda kileleni mwa Mlima Kumorah, aliokuwa ameuona katika ono. Hapo alikuta jiwe kubwa. Aliinua jiwe lile kwa kutumia fimbo.
Chini ya jiwe lile kulikuwa na sanduku lililoundwa kwa mawe. Joseph alipokuwa akitazama ndani ya sanduku, aliziona bamba za dhahabu.
Moroni alimtokea na kumwambia Joseph asichukue zile bamba ila arudi tena siku kama hiyo kila mwaka kwa miaka minne. Kila wakati Joseph alipokwenda, Moroni alimfunza.
Baada ya miaka minne Joseph hatimaye aliruhusiwa kuchukua bamba zile. Alitumia Urimu na Thumimu kutafsiri baadhi ya bamba hizo.
Waandishi walimsaidia Joseph kwa kuandika maneno wakati alipokuwa akiyatafsiri kutoka kwenye bamba za dhahabu.
Joseph aliyapeleka maneno yaliyokuwa yametafsiriwa kwa mpiga chapa na kuyatengeneza kuwa kitabu.
Historia ya Kanisa 1:71
Kitabu hicho kinaitwa Kitabu cha Mormoni. Kinasimulia kuhusu watu walioishi Marekani miaka mingi iliyopita. Pia kinasimulia kuhusu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.