Sura ya 45 Yesu Kristo Anatufundisha kuhusu Sakramenti na Sala Yesu Kristo aliwatuma wafuasi wake waende wakalete mkate na divai. Aliwaambia Wanefi waketi chini. 3 Nefi 18:1–2 Baada ya wanafunzi kurejea, Mwokozi aliumega mkate katika vipande vipande na kuubariki. Aliwapa wanafunzi wake na kuwataka wawapatie watu wengine pia. 3 Nefi 18:3–4 Yesu alisema kwamba watu wanaoshiriki sakramenti wanaahidi daima kumkumbuka Yeye na dhabihu Yake. Kisha wanapokea Roho Wake. 3 Nefi 18:7 Yesu Kristo alibariki divai na kutoa kiasi kwa wanafunzi Wake. Wanafunzi waliwapa watu divai kiasi. 3 Nefi 18:8 Yesu alisema wale wanaoshiriki sakramenti wanaahidi kutii amri Zake. 3 Nefi 18:10 Yesu tena aliwaambia wanafunzi Wake kwamba kila mtu anayeshiriki sakramenti na kumkumbuka daima atakuwa na Roho Wake. 3 Nefi 18:11 Aliwaambia mitume wake wangebarikiwa kama wangetii amri Zake. 3 Nefi 18:14 Aliwaambia wasali kila wakati na wasali jinsi walivyokuwa wamemuona akisali. 3 Nefi 18:15–16 Mwokozi aliwaambia Wanefi wote wasali kwa Baba wa Mbinguni kwa jina Lake. Pia aliwaamuru wasali pamoja na familia zao. 3 Nefi 18:19, 21 Alisema watu lazima wakutane pamoja mara kwa mara. Wanapaswa kuwakaribisha wengine katika mikutano yao, kusali kwa niaba yao, na kuwa mifano mizuri kwao. 3 Nefi 18:22–24 Yesu aliwapatia wanafunzi Wake uwezo kutoa Roho Mtakatifu. Kisha mawingu yakawafunika watu kwa hivyo ni wanafunzi tu waliomuona Yesu Kristo akienda juu mbinguni. 3 Nefi 18:36–39