“Juni 3–9: ‘Waliimarishwa na Hawangeondolewa.’ Mosia 29–Alma 4,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)
“Juni 3–9. Mosia 29–Alma 4,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)
Juni 3–9: “Waliimarishwa na Hawangeondolewa”
Mosia 29–Alma 4
Wengine wangeweza kuona pendekezo la Mfalme Mosia la kubadilisha wafalme na nafasi yao kuchukuliwa na waamuzi waliochaguliwa kama mabadiliko ya kisiasa tu. Lakini kwa Wanefi, hasa wale ambao waliishi chini ya utawala wa Nuhu, Mfalme Mwovu, badiliko hili lilikuwa na umuhimu wa kiroho pia. Walikuwa wameshuhudia jinsi mfalme mwovu alivyokuwa amewaharibu watu wake, na walikuwa “na shauku kubwa” kuondolewa katika nguvu za aina kama hiyo. Badiliko hili lingewaruhusu wao wenyewe kuwajibika kwa ajili ya haki yao wenyewe na “kujibu kwa ajili ya dhambi [zao] wenyewe” (Mosia 29:38).
Bila shaka, mwisho wa utawala wa wafalme haukumaanisha mwisho wa matatizo katika jamii ya Wanefi. Watu wajanja kama Nehori na Amlisi waliendeleza dhana za uongo, wasioamini waliwatesa Watakatifu na waumini wengi wa Kanisa walijawa na kiburi na kukengeuka. Lakini “wafuasi wa Mungu waliokuwa wanyenyekevu” walibaki “imara na hawangeondolewa” licha ya yale ambayo yalikuwa yakifanyika kuwazunguka (Alma 4:15; 1:25).
Mawazo kwa ajili ya kujifunza Nyumbani na Kanisani
Ninaweza kuwa ushawishi chanya katika jumuiya yangu.
Miaka mitano tu katika uongozi wa waamuzi, mgogoro uliibuka ambao ungeingiza majaribuni tangazo la Mosia kwamba sauti ya watu kwa kawaida ingelichagua kile kilicho haki (ona Mosia 29:26). Jifunze Alma 2:1–7 ili kujua lilikuwa ni jambo lipi na Wanefi walifanya nini kuhusu hilo. Nini kingeweza kutokea kama “watu wa kanisa” wasingefanya sauti zao zisikike? Ni kipi kingine unajifunza kutoka katika hadithi hii kuhusu namna Bwana anavyotaka wewe ujihusishe katika jumuiya yako (ona pia Mosia 29:26–27).
Ni mambo yapi muhimu yanaikabili jumuiya yako? Fikiria kwamba wewe, kama wale Wanefi, unaweza kuhakikisha kwamba sauti yako inajumuishwa katika “sauti ya watu.” Ni kwa njia zipi zingine unaweza, kama mfuasi wa Yesu Kristo, kuishawishi jumuiya yako kwa wema?
Ona Dallin H. Oaks, “Wapendeni Maadui Zenu,” Liahona,, Nov. 2020, 26–29.
Neno la Mungu linaweza kunisaidia nitambue mafundisho ya uongo.
Ingawaje Nehori hatimaye alikiri kwamba yale aliyofundisha hayakuwa ya kweli, mafundisho yake yaliendelea kuwa na nguvu kwa Wanefi kwa miaka mingi. Kwa nini unadhani watu walipenda kile Nehori alichokifundisha? Katika Alma 1:2–6, tafuta uwongo ulioko kwenye mafundisho ya Nehori—na kweli alizotumia kwenye uwongo huo.
Gideoni alipambana na Nehori “kwa maneno ya Mungu” (Alma 1:7, 9). Hapa kuna baadhi ya maandiko ambayo yanapinga uwongo wa Nehori: Mathayo 7:21–23; 2 Nefi 26:29–31; Mosia 18:24–26; na Helamani 12:25–26. Jaribu kufanya ufupisho wa kila andiko. Je, umejifunza nini kutoka kwa manabii walio hai ambacho kinapinga mafundisho ya uongo katika siku zetu?
Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni “wafuasi wanyenyekevu wa Mungu.”
Mlango wa 1 na 4 wa Alma unafafanua vipindi ambapo Kanisa lilistawi, lakini waumini wa Kanisa walichukulia ustawi huo kwa utofauti. Kwa mfano, linganisha Alma 1:19–30 na Alma 4:6–15 ili kuona jinsi waumini wa Kanisa walivyobadilika ndani ya miaka michache tu. Kulingana na kile ambacho umekisoma, ni kwa namna gani wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo huhisi kuhusu watu ambao wana imani tofauti? Ni mtazamo upi ambao wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo wanakuwa nao kwenye utajiri na mafanikio? Je, ni kitu gani unahisi kushawishika kubadili kuhusu mtazamo wako wewe mwenyewe?
Mfano na ushuhuda wangu vinaweza kuibadili mioyo ya watu.
Pengine unaweza kuhisi huzuni Alma aliyoihisi wakati alipoona kile kilichokuwa kikitokea miongoni mwa watu wake. Tafuta matatizo aliyoyaona katika Alma 4:6–15. Je, umeona matatizo yoyote ambayo yanafanana? Pengine una wasiwasi kuhusu mpendwa ambaye anapambana na matatizo kama haya. Je, umewahi kujiuliza ni kitu gani ungeweza kufanya ili kusaidia?
Wengine wanaweza kusema kwamba Alma, kama mwamuzi mkuu, alikuwa mtu bora zaidi wa kushughulikia matatizo haya. Lakini Alma alihisi kwamba kulikuwa na njia bora zaidi. Wakati ukisoma mistari 16–20, nini kinakuvutia katika juhudi zake za kuwasaidia watu wake?
Alma alikuwa na imani kuu katika neno la Mungu na “ushuhuda safi” (mstari wa 19). Ni mifano ipi umeiona yenye nguvu ya ushuhuda safi? Wakati ukitafakari baadhi ya njia ambazo unaweza kushiriki ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo na injili Yake, ungeweza kusoma tena Alma 4:6–14. Matendo ya waumini wa Kanisa kwenye mistari hii yanaonesha nini kuhusu shuhuda zao juu ya Yesu Kristo na mafundisho Yake? Je, unagundua nini kuhusu matokeo ya matendo yao—juu yao wenyewe na kwa wengine? Ungeweza pia kufikiria kuhusu njia ambazo wewe umewahi kubarikiwa kupitia shuhuda safi za watu wengine, iwe ulitolewa kupitia maneno au vitendo.
Fikiria njia ambazo unaweza kushiriki ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo—kwa maneno au vitendo. Je, nani angenufaika kutokana na ushahidi wako?
Ona pia Gary E. Stevenson, “Kulisha na Kutoa Ushuhuda,” Liahona, Nov. 2022, 111–14; “Ushuhuda,” Nyimbo za Dini, na. 69; “Alma the Younger Steps Down as Chief Judge” (video), Gospel Library; Mada za Injili, “Ufunuo,” Gospel Library.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Bwana anaweza kunisadia nitambue mafundisho ya uongo.
-
Njia mojawapo ya kujifunza Alma 1:2–4 pamoja na watoto wako ni kwa kuwasaidia watengeneze maswali ya haraka ya kweli au si kweli kwa kutumia kauli zilizofundishwa na Nehori, mwalimu wa uongo. Kisha ungeweza kuzungumza nao kuhusu kwa nini mara nyingi Shetani huchanganya kweli na uongo. Wasaidie watoto wako wafikirie baadhi ya mifano. Katika mistari 7–9, ni kwa namna gani Gideoni aliushinda uongo wa Nehori? (Ona pia “Mlango wa 20: Alma na Nehori,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 54–55.)
Kama muumini wa Kanisa la Yesu Kristo, ninawapenda na kuwatumikia wengine.
-
Baadhi ya waumini wa Kanisa la Bwana katika wakati wa Alma walikuwa wakarimu na wenye kutoa na waumini wengine walikuwa si wakarimu na walikuwa wenye kiburi. Ili kuwasaidia watoto wako wajifunze kutoka kwenye mifano hii, mngeweza kusoma pamoja Alma 1:27, 30 na tengeneza orodha ya aina za watu waliosaidiwa na waumini wa Kanisa la Bwana. Je, ni nani tunayemjua “ambaye yawezekana [yuko] katika uhitaji” (Alma 1:30) wa upendo na msaada wetu? Pia mngeweza kuimba kwa pamoja wimbo kuhusu upendo na huduma kama vile “Kindness Begins with Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 145), na wasaidie watoto wafikirie matendo ambayo yangeweza kuendana na wimbo.
-
Je, tunapaswa kufanya nini wakati watu wanapokuwa si wakarimu kwetu? Fikiria kusoma pamoja na watoto wako jinsi wafuasi wa Kristo walivyotendewa katika Alma 1:19–20. Zungumza kuhusu jinsi gani wao walijibu katika mstari wa 22 na 25. Pengine mngefanyia mazoezi namna ya kujibu pale wengine wanapokuwa si wakarimu.
Ushuhuda wangu unaweza kuwaimarisha wengine.
-
Mara nyingi “ushuhuda safi” (Alma 4:19) wa mtoto unaweza kuwa na ushawishi wenye nguvu kwa wengine. Ili kuwasaidia watoto wako wagundue hili, ungeweza kusoma nao kwenye Alma 4:8–12, 15, ukiwasaidia wabainishe matatizo ambayo yalikuwa yakitokea kwenye Kanisa. Je, Alma angefanya nini ili kutatua matatizo haya? Wasaidie wapate kitu ambacho Alma aliamua kufanya kutoka kwenye Alma 4:16–20. Pengine mngeweza kushirikishana jinsi ushuhuda wa mtu mwingine juu ya Kristo ulivyowaimarisha ninyi.
-
Kama watoto wako wanahitaji mifano ya kujua ushuhuda ni nini, fikiria kuwaonesha video fupi ya mzungumzaji kwenye mkutano mkuu akitoa ushuhuda. Ungeweza pia kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii au kuimba wimbo kama “Ushuhuda” (Nyimbo za Dini, na. 69). Tunajifunza nini kuhusu shuhuda kutoka kwenye nyenzo hizi? Waruhusu watoto wako wafanye mazoezi kushiriki shuhuda zao.