Njoo, Unifuate
Aprili 13–19. Mosia 1–3: “Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote”


“Aprili13–19. Mosia 1–3: ‘Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Aprili13–19. Mosia 1–3,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Picha
Mfalme Benyamini akiwafundisha watu wake

Minerva K. Teichert (1888–1976), Hotuba ya Buriani ya Mfalme Benyamini, 1935, mafuta juu ya ubao, inchi 36 x 48. Chuo Kikuu cha Sanaa cha Brigham Young

Aprili 13–19

Mosia 1–3

“Kujazwa na Upendo kwa Mungu na kwa Watu Wote”

Mfalme Benyamini alitoa sababu moja ya kuandika misukumo yetu ya kiroho: “Kwani haingewezekana kwamba baba yetu Lehi, angevikumbuka vitu hivi vyote, kuvifundisha kwa watoto wake, bila usaidizi wa bamba hizi” (Mosia 1:4).

Andika Misukumo Yako

Unaposikia neno mfalme, unaweza ukafikiria kuhusu mataji, ngome, watumishi, na viti vya enzi. Katika Mosia 1–3, utasoma kuhusu mfalme wa aina tofauti. Badala ya kujikimu kutokana na jasho la watu wake, Mfalme Benyamini “alifanya kazi kwa mikono [yake] mwenyewe” (Mosia 2:14). Badala ya kuwahitaji wengine kumtumikia, aliwatumikia watu wake “kwa uwezo wote, akili na nguvu ambazo Bwana [alim]patia” (Mosia 2:11). Mfalme huyu hakutaka watu wake wamuabudu; badala yake, aliwafundisha wamuabudu mfalme mkuu kuliko yeye mwenyewe, kwa sababu alielewa kwamba ni “Bwana Mwenyezi ambaye anatawala” (Mosia 3:5). Kama viongozi wote wakuu katika ufalme wa Mungu, maneno na mfano wa Mfalme Benyamini vinatuelekeza kwa Mfalme wa Mbinguni, ambaye ni Mwokozi, Yesu Kristo. Mfalme Benyamini alishuhudia ya kwamba Yesu alishuka “chini kutoka mbinguni” na kwenda “miongoni mwa watu, akitenda miujiza mikuu. … Na lo, anawajia walio wake, ili wokovu uwafikie watoto wa watu hata kupitia imani kwa jina lake” (Mosia 3:5, 9).

Picha
ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

Mosia 2:1–9

Kupokea neno la Mungu kunahitaji maandalizi.

Wakati Mfalme Benyamini alipotuma ujumbe kwamba alitaka kuzungumza na watu wake, watu wengi walikuja “kwamba hawakuhesabika” (Mosia 2:2). Walikuja, kwa sehemu, kwa sababu ya shukrani na upendo kwa kiongozi wao. Lakini muhimu zaidi, walikuja kufundishwa neno la Mungu.

Unaposoma Mosia 2:1–9, tafuta kile watu walichofanya ili kuonyesha ya kwamba walithamini neno la Mungu. Je, ni nini Mfalme Benyamini aliwataka wafanye ili kujitayarisha kusikiliza neno la Mungu? (ona mstari wa 9). Je, ni jinsi gani unaweza kujitayarisha vyema wewe mwenyewe kwa ajili ya kupokea neno la Mungu katika kujifunza kwako kibinafsi na kifamilia na katika mikutano ya Kanisa?

Ona Pia Mathayo 13:18–23; Alma 16:16–17.

Mosia 2:10–26

Ninapowatumikia wengine, ninamtumikia Mungu pia.

Je, unapambana kupata wakati wa kuhudumu au unatamani ya kwamba huduma yako ingekuletea shangwe zaidi? Unafikiri Mfalme Benyamini angesema nini ikiwa ungemuuliza ni kwa nini alihudumu kwa “uwezo, akili, na nguvu” zake zote? (Mosia 2:11). Unaposoma Mosia 2:10–26, tambua kweli ambazo Mfalme Benyamini alifundisha kuhusu huduma na tafakari jinsi unavyoweza kuzitumia maishani mwako. Kwa mfano, ina maana gani kwako kujua ya kwamba wakati unapowatumikia watu wengine, unamtumikia Mungu pia? (ona Mosia 2:17). Fikiria kuhusu jinsi unavyoweza kumtumikia mtu fulani wiki hii!

Ona pia Mathayo 25:40.

Picha
wanawake wawili wakikumbatiana

Ninapowatumikia wengine, ninamtumikia Mungu pia.

Mosia 3:1–20

Naweza kumshinda binadamu wa kawaida na kuwa mtakatifu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Mfalme Benyamini, kama manabii wote, alitoa ushuhuda juu ya Yesu Kristo ili watu wake “wapokee msamaha wa dhambi zao, na kushangilia kwa shangwe kuu zaidi” (Mosia 3:13). Pia alifundisha ya kwamba Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake, hatusababishi tu kuwa wasafi lakini pia anatupa nguvu za kumvua “mwanadamu wa kawaida” na kuwa “mtakatifu” (Mosia 3:19; ona pia Mwongozo wa Maandiko, “Mwanadamu wa Kawaida,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org).

Mzee David A. Bednar alieleza: “Ni Upatanisho wa Yesu Kristo ambao unatoa vyote nguvu za kusafisha na kukomboa ambazo zitatusaidia kushinda dhambi na nguvu za kutakasa na kuimarisha ambazo hutusaidia kuwa bora kuliko vile ambavyo tungekuwa tukitegemea nguvu zetu wenyewe. Upatanisho usio na mwisho ni kwa wote mtenda dhambi na mtakatifu katika kila mmoja wetu” (“Mikono Safi na Moyo Safi,” Ensign au Liahona, Nov. 2007, 82).

Haya ni baadhi ya maswali ya kutafakari unaposoma ushuhuda wa Mfalme Benyamini kuhusu Mwokozi katika Mosia 3:1–20:

  • Je, najifunza nini kutoka kwenye mistari hii kuhusu Mwokozi na misheni Yake?

  • Ni kwa jinsi gani Yesu Kristo amenisaidia kushinda dhambi? Ni jinsi gani amenisaidia kubadili asili yangu na kuwa zaidi kama mtakatifu?

  • Je, najifunza nini kuhusu kuwa mtakatifu kutoka Mosia 3:19?

Mosia 3:8

Ni kwa nini Mfalme Benyamini alimtaja Yesu kama “Baba wa mbingu na dunia”?

Rais Joseph F. Smith alieleza: “Yesu Kristo, ambaye tunamtambua pia kama Yehova, alikuwa mtendaji wa Baba, Elohimu, katika kazi ya uumbaji. … Yesu Kristo, akiwa Muumbaji, mara kwa mara anaitwa Baba wa mbingu na dunia … ; na kwa kuwa uumbaji Wake ni wa ubora wa milele inafaa kabisa anapoitwa Baba wa Milele wa mbingu na dunia” (Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph F. Smith [1998], 357).

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

Mosia 1:1–7

Ni kwa jinsi gani bamba za shaba na bamba za Nefi ziliwabariki watu wa Mfalme Benyamini? Ni jinsi gani maandiko yanabariki familia yetu?

Mosia 2–3

Ingeweza kuwa ya kupendeza kwa familia yako kutengeneza mandhari ya hotuba ya Mfalme Benyamini. Ungeweza kutengeneza mnara mdogo na kuwaruhusu wanafamilia kufanya zamu kusoma maneno ya Mfalme Benyamini wakiwa wamesimama juu yake. Wanafamilia wengine wangeweza kusikiliza wakiwa katika hema la muda.

Mosia 2:9–19

Tunajifunza nini kuhusu huduma kutokana na mafundisho na mfano wa Mfalme Benyamini? Je, tunashawishika kufanya nini?

Mosia 2:15–25

Je, inaweza kuwa na manufaa kwa familia yako kujadiliana kuhusu unyenyekevu? Ni kwa nini Mfalme Benyamini hakujigamba kuhusu yale yote aliyokuwa ametenda? Ni nini tunaweza kujifunza kutoka kwenye mafundisho yake kuhusu uhusiano wetu na Mungu?

Mosia 2:36–41

Ni nini Mfalme Benyamini alifundisha kuhusu athari za kufahamu ukweli na kukosa kuishi kulingana nao? Alifundisha nini kuhusu jinsi ya kupata furaha ya kweli?

Mosia 3:19

Tunahitajika kufanya nini ili tuwe watakatifu? Ni tabia ipi kutoka kwenye mstari huu tunaweza kufokasi kuwa nayo kama familia?

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Kibinafsi

Weka malengo yanayowezekana. Kutumia hata dakika chache katika siku kujifunza maandiko kunaweza kubariki maisha yako. Jiwekee sharti la kujifunza kila siku, na tafuta njia ya kujikumbusha mwenyewe ahadi yako.

Picha
Mfalme Benyamini akihubiria watu wake

Hotuba ya Mfalme Benyamini, na Jeremy Winborg

Chapisha