Njoo, Unifuate
Kiambatisho C: Mashahidi Watatu


“Kiambatisho C: Mashahidi Watatu” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Kiambatisho C,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Kiambatisho C

Mashahidi Watatu

Kwa zaidi ya miaka mitano—kutoka wakati wa matembezi ya kwanza ya malaika Moroni kwa Joseph Smith kufikia 1829—Joseph peke yake alikuwa mtu aliyekubaliwa kuona bamba za dhahabu. Hii ilisababisha ukosoaji na mateso mengi kutoka kwa wale walioamini kwamba alikuwa akiwahadaa watu. Kwa hivyo fikiria shangwe aliyohisi Joseph wakati, alipokuwa akitafsiri Kitabu cha Mormoni, alijifunza kwamba Bwana angewaruhusu wengine kuziona bamba zile na wao pia “wangeshuhudia ukweli wa kitabu hicho kwa vitu vilivyomo” (2 Nefi 27:12–14; ona pia 2 Nefi 11:3; Etheri 5:2–4).

Mnamo Juni 1829, Oliver Cowdery, David Whitmer, na Martin Harris waliomba ruhusa wawe wale mashahidi watatu ambao Kitabu cha Mormoni kilitabiri. Bwana aliwakubalia hamu yao (ona MM 17) na kumtuma malaika, ambaye aliwaonyesha bamba zile. Watu hawa walikuja kujulikana kama Mashahidi Watatu, na ushuhuda wao umewekwa katika kila nakala ya Kitabu cha Mormoni.1

Rais Dallin H. Oaks alieleza ni kwa nini ushuhuda wa Mashahidi Watatu ni ni wa kuvutia sana: “Ushuhuda wa Mashahidi Watatu kwa Kitabu cha Mormoni unasimama mbele kwa nguvu kubwa. Kila mmoja kati ya hao watatu alikuwa na sababu kubwa na nafasi ya kukanusha ushuhuda wake kama ungekuwa wa uongo, au kutatiza maneno juu ya ndani kama chochote kingekuwa si cha kweli. Kama inavyojulikana vizuri, kwa sababu ya kutokubaliana au wivu kuhusiana na viongozi wengine wa Kanisa, kila mmojawapo wa hawa mashashidi watatu alitengwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho karibu takribani miaka minane baada ya chapisho la ushuhuda wao. Wote watatu walikwenda njia zao tofauti, bila masilahi ya pamoja kusaidia juhudi za kushirikiana. Hata mwishoni mwa maisha yao—vipindi kadiri ya miaka 12 mpaka 50 baada ya kutengwa kwao—hakuna kati ya mashahidi hawa aliyekengeuka kutoka kwenye ushuhuda wake uliochapishwa au aliyesema chochote ambacho kina mashaka yoyote juu ya ukweli wake”2

Kufikia mwisho mwa maisha yao, Mashahidi Watatu walikuwa imara katika uaminifu wao kwa ushuhuda wao juu ya Kitabu cha Mormoni.

Oliver Cowdery

Baada ya kubatizwa Kanisani na muda mfupi kabla ya kifo chake, Oliver alitembelewa na mmisionari Mzee Jacob Gates, ambaye alikuwa akipita katika eneo la Richmond, Missouri, akiwa njiani kutumikia misheni yake kule Uingereza. Mzee Gates alimuuliza Oliver kuhusu ushuhuda wake juu Kitabu cha Mormoni. Mwana wa Mzee Gates alisimulia jibu la Oliver:

“Kwa kuuliza swali hili kulionekana kumgusa Oliver kwa dhati. Hakujibu hata neno, lakini alinyanyuka kutoka kwenye kiti chake cha kupumzikia, akaenda kwenye kabati ya vitabu, akachukua toleo la kwanza la Kitabu cha Mormoni, akafungua ushuhuda wa Mashahidi Watatu, na kusoma kwa taadhima kubwa maneno ambayo alikuwa ametia saini kwa jina lake, karibu miaka ishirini na minne iliyokuwa imepita. Akimtazama baba yangu, alisema: “Jacob ninataka wewe ukumbuke kile nitakachokuelezea. Mimi ni mtu anayekufa, na itanifaidi nini nikikudanganya? Ninajua,’ alisema, ‘kwamba Kitabu cha Mormoni kilitafsiriwa kupitia karama na uwezo wa Mungu. Macho yangu yaliona, maskio yangu yalisikia, na kuelewa kwangu kuliguswa, na ninajua kwamba nilichoshuhudia ni kweli. Haikuwa ndoto, wala fikra za bure za akili—ilikuwa kweli.’”3

David Whitmer

Katika miaka yake ya mwisho, David Whitmer alifahamu ya kwamba kulikuwa na uvumi kwamba alikuwa amekana ushuhuda wake wa Kitabu cha Mormoni. Katika kujibu mashtaka haya, David alisisitiza tena ushuhuda wake kupitia barua iliyochapishwa katika gazeti la eneo lake. Richmond Conservator:

“Ili ulimwengu uweze kujua ukweli, ningependa sasa, kutoa msimamo, kama ilivyokuwa, katika mwisho wa safari yangu ya maisha, na katika kumwogopa Mungu mara moja na ya mwisho, kutoa kauli hii kwa umma:

“Kwamba sijawahi kwa wakati wowote kukana ushuhuda ule , au sehemu yake yoyote, ambayo kwa muda mrefu imechapishwa pamoja na Kitabu kile, kama mmoja wa mashahidi watatu. Wanaonijua vizuri, wanafahamu vyema kwamba daima nimeshikilia ushuhuda huo. Na kwamba mtu yeyote asipotoshwe au kuwa na wasiwasi na mitazamo yangu kwa wakati huu kuhusiana na hilo, kwa mara nyingine ninathibitisha ukweli wa kauli zangu zote, kama zilivyotolewa na kuchapishwa.

“‘Yeye ambae ana sikio la kusikilizia, mwache asikie,’ haikuwa ulaghai! Kilichoandikwa kimeandikwa—na yule anayesoma mwache aelewe.”4

Martin Harris

Kama Oliver Cowdery, Martin Harris aliacha Kanisa kwa muda lakini hatimaye alibatizwa tena. Katika miaka yake ya baadaye, alijulikana kwa kubeba nakala ya Kitabu cha Mormoni ubavuni na kushuhudia juu ya ukweli wake kwa wote ambao wangemsikiliza: “Ninajua Kitabu cha Mormoni kuwa cha kweli kabisa.” Ingawa watu wote wanaweza kukana ukweli wa kitabu hicho, sidhubutu kufanya hivyo. Moyo wangu uko imara. Ee Mungu, moyo wangu uko imara! Nisingeweza kujua kwa dhati au dhahiri kuliko ninavyojua.”5

George Godfrey, mtu aliyemfahamu Martin, aliandika: “Saa chache kabla ya kifo chake … Nilimuuliza [Martin] kama hakuhisi kwamba kulikuwa na dalili hata kidogo, ya ulaghai na udanganyifu kuhusu vitu ambavyo viliandikwa na kusemwa juu ya Kitabu cha Mormoni, na alijibu kama alivyokuwa akijibu siku zote … na kusema: ‘Kitabu cha Mormoni si bandia. Ninajua kile ninachokijua. Nimekiona kile nilichoona na nimesikia kile nilichosikia. Nimeziona bamba za dhahabu ambazo kutoka kwake Kitabu cha Mormoni kiliandikwa. Malaika alitutokea mimi pamoja na wengine na kushuhudia juu ya ukweli wa kumbukumbu hii, na kama ningekuwa na nia ya kusema uwongo na kuapa kwa udanganyifu juu ya ushuhuda ninaoutoa kwa wakati huu ningekuwa mtu tajiri sana, lakini nisingeweza kushuhudia tofauti na jinsi ambavyo nimefanya na ninavyofanya kwa maana vitu hivi ni vya kweli.’”6

“Mathali Mashahidi Wengi Kama Apendavyo”

Ushahidi wa Mashahidi Watatu ni wa kuvutia hasa ukifikiria uzoefu wao ndani na nje ya Kanisa.7 Baada ya yote, Oliver, David, na Martin kamwe hawakukoma kushuhudia juu ya kile walichokishuhudia kwamba Kitabu cha Mormoni kilitafsiriwa kupitia karama na uwezo wa Mungu. Na haikuwa wao peke yao.

Hapo kale, Nefi alisema, “Bwana Mungu ataendelea kutoa maneno ya kitabu hicho; na kwa vinywa vya mashahidi wengi kama apendavyo ataimarisha neno lake” (2 Nefi 27:14). Pamoja na Nabii Joseph Smith na Mashahidii Watatu, Bwana pia Alichagua mashahidi wengine wanane waweze kuona bamba zile. Ushuhuda wao pia umejumuishwa katika kila nakala ya Kitabu cha Mormoni. Kama Oliver, David, na Martin, Mashahidi Wanane walisalia kuwa waaminifu kwa ushuhuda wao wa Kitabu cha Mormoni na ushuhuda wao juu bamba za dhahabu.

William E. McLellin alikuwa muongofu wa mwanzo Kanisani ambaye aliwafahamu wengi wa mashahidi wa Kitabu cha Mormoni kibinafsi. William hatimaye aliacha Kanisa, lakini aliendelea kuathirika kwa kina na ushahidi wa dhati aliokuwa ameusikia kutoka kwa mashahidi.

“Na sasa ningeuliza,” McLellin aliandika kuelekea mwisho wa maisha yake, “nitafanya nini na mashahidi wengi waaminifu, wanaotoa ushahidi wa kimantiki na wenye taadhima? Hawa mabwana wakiwa katika upeo wa maisha yao, waliona ono la malaika wa Mungu, na kuwashuhudia watu wote. Na wanaume wanane waliona bamba, na kuzishika kwa mikono. Na hivyo basi watu hawa walijua kwamba vitu walivyo vitangaza kwa uhakika kuwa vya kweli kabisa. Na hilo pia wakati wakiwa na umri mdogo, na sasa wakiwa wazee wanasema vitu vile vile.”8

Hata kama hatujaziona bamba za dhahabu jinsi Mashahidi Watatu walivyofanya, tunaweza kupata nguvu kutoka kwenye shuhuda zao. Hata wakati sifa zao zilipokuwa mashakani na usalama wa maisha yao kutishiwa kwa sababu ya shuhuda zao, watu hawa wenye uadilifu kwa ujasiri walikuwa wakweli kwa ushahidi wao hadi mwisho kabisa.

  1. Soma kuhusu uzoefu wao katika Saints: The Story of the Church of Jesus Christ in the Latter Days, vol. 1, The Standard of Truth, 1815–1846 (2018), 73–75.

  2. Dallin H. Oaks, “The Witness: Martin Harris,” Ensign, Mei 1999, 36.

  3. Jacob F. Gates, “Testimony of Jacob Gates,” Improvement Era, Mac. 1912, 418–19.

  4. Katika Lyndon W. Cook, ed., David Whitmer Interviews: A Restoration Witness (1991), 79.

  5. Katika Mitchell K. Schaefer, “The Testimony of Men: William E. McLellin and the Book of Mormon Witnesses,” BYU Studies, vol. 50, no. 1 (2011), 108; matumizi ya herufi kubwa yamesawazishwa.

  6. George Godfrey, “Testimony of Martin Harris” (unpublished manuscript), dondoo katika Eldin Ricks, The Case of the Book of Mormon Witnesses (1961), 65–66.

  7. Kwa mfano, ona Saints, 1:182–83.

  8. Katika Schaefer, “Testimony of Men,” 110.

Chapisha