Njoo, Unifuate
Februari 3–9. 2 Nefi 1–5: “Tuliishi kwa Furaha”


“Februari 3–9. 2 Nefi 1–5: ‘Tuliishi kwa Furaha,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Februari 3–9. 2 Nefi 1–5,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020

Adamu na Hawa wakiondoka katika Bustani ya Edeni

Adam na Hawa, na Douglas Fryer

Februari 3–9

2 Nefi 1–5

“Tuliishi kwa Furaha”

Lehi aliwafundisha kila mmoja wa watoto wake kulingana na mahitaji yao binafsi na hali zao. Fuata mfano wake unapojiandaa kufundisha watoto darasani kwako.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Baada ya kuelezea kwamba Lehi aliifundisha familia yake kuhusu uhuru wa kufanya chaguzi zetu wenyewe, waalike watoto kushiriki uzoefu ambao wamekuwa nao kwenye kuchagua mema. Walijisikiaje baada ya kufanya uchaguzi huo? Ni kwa jinsi gani wanaweza kukumbuka kuchagua mema siku za baadaye?

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

2 Nefi 1:20 

Ninabarikiwa pale ninapotii.

Kanuni inayofundishwa katika mstari huu—utiifu huleta baraka—imeelezwa kwa mfano mara nyingi kote kwenye Kitabu cha Mormoni. Fikiria jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto kuitambua katika maisha yao wenyewe.

Shughuli za Yakini

  • Waombe watoto wakusaidie kutoa maana ya neno amri na tengeneza orodha ya amri. Soma 2 Nefi 1:20, na sisitiza kwamba tuta “fanikiwa,” au kubarikiwa, pale tunapotii amri. Je, tunahisi vipi tunapotii amri hizi?

  • Waonyeshe watoto vitu ambavyo hutoa ulinzi, kama vile viatu, kofia, na glavu. Waache wajaribu kuvivaa. Ni kwa jinsi gani vitu hivi hutulinda? Waambie kwamba amri za Baba wa Mbinguni zinaweza kutulinda dhidi ya hatari za kiroho. Shiriki uzoefu wako wakati ulipolindwa kwa kufuata amri.

2 Nefi 2:11, 16, 27

Mungu amenipa uhuru wa kuchagua.

Kwa sababu ya chaguzi zao, Adamu na Hawa walitakiwa kuondoka kwenye Bustani ya Edeni. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwafundisha watoto kwamba uchaguzi wa Adamu na Hawa unaturuhusu sisi kutumia uhuru wetu wa kujiamulia kumchagua Baba wa Mbinguni leo?

Shughuli za Yakini

  • Chora picha ya mtu huru na picha ya mfungwa (labda mtu aliye gerezani), na waalike watoto kuonyesha kwa kidole picha sahihi unaposoma maneno uhuru na utumwa katika 2 Nefi 2:27. Sisitiza kirai “huru kuchagua,” na mwalike kila mtoto kukirudia.

  • Pitia tena pamoja na watoto hadithi ya Adamu na Hawa (ona 2 Nefi 2:17–19; ona pia “Sura ya 3: Adamu na Hawa,” Hadithi za Agano la Kale, 15–18, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org) na uchaguzi waliofanya ndani ya Bustani ya Edeni. Wasaidie watoto kuorodhesha baadhi ya chaguzi wanazofanya kila siku. Shuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni alitupatia uhuru wa kuchagua kati ya mema na mabaya, na waalike watoto kuruka juu na chini au kupiga makofi kusherehekea kuwa huru kuchagua.

  • Chezeni mchezo ambapo wewe unasema maneno (kama vile nuru) na watoto wanasema kinyume chake (giza). Rudieni shughuli hii mara kadhaa. Ili kuwasaidia watoto kuelewa jinsi gani kuwa na vinyume hutusaidia kufanya chaguzi, soma nusu ya kwanza ya 2 Nefi 2:11 na 2 Nefi 2:16. Wasimulie watoto hadithi kuhusu mtoto ambaye amejaribiwa kufanya uchaguzi mbaya. Wasaidie watoto kufikiria juu ya kile ambacho ni kinyume cha uchaguzi huo, na waalike kukifanyia igizo. Shuhudia kwamba Baba wa Mbinguni hutubariki sisi pale tunapochagua mema.

  • Imbeni kwa pamoja wimbo kuhusu kufanya chaguzi, kama vile “I’m Trying to Be like Jesus” or “Choose the Right Way” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78–79, 160–61), na waulize watoto kile wanachojifunza kutoka kwenye wimbo kuhusu kufanya chaguzi.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

2 Nefi 1:20

Ninabarikiwa pale ninapotii.

Pale watoto wanapokuwa na imani kwamba Mungu atawasaida kwa kutii amri—hata kama baraka hizo haziji mara moja—ni rahisi kwao kufanya chaguzi za haki.

Shughuli za Yakini

  • Wasaidie watoto kupitia tena baadhi ya chaguzi ambazo Nefi na kaka zake walifanya. Kwa mfano, ona 1 Nefi 2:11–16; 3:5–7; na 18:9–11. Waalike kusoma 2 Nefi 1:20 pamoja na kushiriki kwa nini wanafikiri Lehi angetoa ujumbe huu kwa watoto wake.

  • Andika vifungu vya maneno kutoka 2 Nefi 1:20 kwenye vipande vya karatasi, na jadilini vifungu hivyo humaanisha nini. Waalike watoto kuweka vipande katika mpangilio sahihi kwa kutumia mstari. Kuonyesha kwa mfano tofauti kati ya kufanikiwa na kutengwa, waonyeshe watoto mmea uliositawi na jani au tawi ambalo limetengwa kutoka kwenye mmea. Ni nini tofauti kati ya jani lililoko kwenye mmea na lile lililotengwa? Ni kwa jinsi gani sisi ni kama jani kwenye mmea pale tunapotii amri za Mungu? Waalike watoto kuandika katika shajara jinsi Mungu anavyowabariki pale wanapochagua mema.

2 Nefi 2:22–28

Mungu alinipatia uhuru wa kuchagua.

Yesu Kristo alituokoa kutokana na kifo cha kimwili na kifo cha kiroho (utengano na Mungu kwa sababu ya dhambi) kupitia Upatanisho wake na Ufufuko. Ili kuishi na Baba wa Mbinguni tena, lazima tutumie haki yetu ya kujiamulia daima kutubu na kujitahidi kuishi kwa haki.

Shughuli za Yakini

  • Nyanyua juu picha ya Adamu na Hawa (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 4), na waalike watoto kushiriki kile wanachojua kuhusu kilichotokea kwa Adamu na Hawa ndani ya Bustani ya Edeni. Wasaidie watoto kupata majibu katika 2 Nefi 2:22–27. Elezea kwamba kwa sababu ya uchaguzi wa Adamu na Hawa, tunabarikiwa kwa kuja duniani na kutumia haki yetu ya kujiamulia kufanya chaguzi nzuri na kutubu kupitia Upatanisho wa Kristo pale tunapofanya chaguzi mbaya.

  • Andika maneno ya 2 Nefi 2:27 ubaoni. Wasaidie watoto kukariri mstari kwa kuurudia na kufanya zamu kufuta maneno kila mara wanapourudia. Wasaidie watoto kufikiria maisha bila ya chaguzi yangekuwaje. Kwa nini wana shukrani kwa ajili ya haki ya kujiamulia?

  • Waalike watoto kushiriki uzoefu wakati walipofanya uchaguzi mzuri. Walijisikiaje baada ya kufanya uchaguzi huo? Je, tunaweza kufanya nini ili kujisaidia wenyewe kuchagua mema pale tunapojaribiwa kufanya jambo baya? Fikiria kuimba wimbo kuhusu kufanya chaguzi, kama vile “Choose the Right” (Nyimbo za Dini, na. 239), na waalike watoto kushiriki kile wanachojifunza kutoka kwenye wimbo.

2 Nefi 3:6–24

Joseph Smith alikuwa “mwonaji bora.”

Katika 2 Nefi 3 Lehi alinena unabii kuhusu Nabii Joseph Smith. Unaweza kutumia hii kama fursa ya kufundisha watoto kuhusu wito wake katika siku za mwisho.

Shughuli za Yakini

  • Waalike watoto kutafuta dokezo kwenye 2 Nefi 3:6–24 kuhusu nabii yupi anazungumziwa. Orodhesha dokezo zao ubaoni. Kwa nini Joseph Smith anaitwa “mwonaji bora”? Ni nini ambacho Joseph Smith alifanya kile ambacho ni “cha thamani kuu kwa [ndugu zake]? (mstari wa 7).

  • Imbeni wimbo kuhusu Joseph Smith, kama vile “Sifa kwa Mwanaume” (Nyimbo za Dini, na. 27), au tazama video ambayo inafafanua vipengele tofauti vya wito wake, kama zile zinazopatikana kwenye history.ChurchofJesusChrist.org/article/joseph-smith-video-downloads. Waulize watoto kwa nini wana shukrani kwa Nabii Joseph Smith.

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Wahimize watoto kutambua fursa walizonazo kufanya chaguzi wiki hii. Waalike kuwa tayari kushiriki wiki ijayo chaguzi walizofanya na matokeo ya chaguzi zao.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Watoto wanaweza kutambua ushawishi wa Roho. Wafundishe watoto kwamba hisia za amani, upendo, na ukunjufu walizonazo wakati wanaongea au kuimba kuhusu Yesu Kristo na injili Yake zinatoka kwa Roho Mtakatifu. Hisia hizi zinaweza kujenga shuhuda zao.