“Februari 10–16. 2 Nefi 6–10: ‘Ee Jinsi Gani Ulivyo Mkuu Mpango wa Mungu Wetu ’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Februari 10–16. 2 Nefi 6–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Februari 10–16
2 Nefi 6–10
“Ee Jinsi Gani Ulivyo Mkuu Mpango wa Mungu Wetu!”
Unaposoma 2 Nefi 6–10, tafuta mwongozo kutoka kwa Roho kuhusu nini ufundishe. Muhtasari huu pamoja na Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia vinaweza kuchochea mawazo ya ziada.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Wahimize watoto kufanya zamu kushiriki jambo fulani walilojifunza kuhusu Yesu Kristo na Upatanisho Wake wakati wakijifunza 2 Nefi 6–10 kibinafsi au na familia zao.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Yesu Kristo huniokoa kutokana na dhambi na kifo.
Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia 2 Nefi 9:7–13 na 20–23 kuwasaidia watoto kuelewa kwamba Yesu Kristo humwokoa kila mtu kutokana na kifo na kufanya iwezekane kwetu kutubu dhambi?
Shughuli za Yakini
-
Wasimulie watoto hadithi ya mtu aliyetumbukia ndani ya shimo refu ambapo asingeweza kutoka nje. Mtu mwingine alikuja na kumwinua mtu huyu nje ya shimo. Unaweza kutaka kuchora picha ya hadithi hii ubaoni au kuifanyia igizo pamoja na watoto. Elezea kwamba shimo hili ni kama kifo na mtu aliyemsaidia aliye shimoni ni sawa na Yesu Kristo, ambaye aliwaokoa watu wote kutokana na kifo kwa kutupatia zawadi ya ufufuko. Waambie watoto kwamba mtu huyu huyu alitumbukia kwenye shimo lingine. Mara hii mwokozi alimpa mtu huyu ngazi kutumia kupanda kutoka nje ya shimo. Elezea kwamba shimo hili ni kama dhambi na ngazi ni Upatanisho wa Yesu Kristo, ambao huturuhusu kutubu na kusamehewa dhambi zetu. Soma 2 Nefi 9:22–23, na toa ushuhuda wako wa Yesu Kristo na Upatanisho Wake.
-
Imbeni kwa pamoja wimbo kuhusu upendo wa Yesu Kristo, kama vile “I Feel My Savior’s Love” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 74–75). Waalike watoto wachore picha za vitu vinavyowasaidia kujua Mwokozi anawapenda.
“Moyo wangu unafurahishwa na uadilifu.”
Ni kwa jinsi gani unaweza kuwatia moyo watoto unaowafundisha “[kufurahishwa] na uadilifu,” au kwa furaha kumtii Bwana? (2 Nefi 9:49).
Shughuli za Yakini
-
Soma 2 Nefi 9:49 kwa watoto, na wasaidie kupata na kuelewa kile ambacho Yakobo alikisema kwamba anakipenda na kukichukia. Shiriki matukio ambapo mtoto anafanya uchaguzi mzuri au uchaguzi mbaya, na waalike watoto kusimama kama uchaguzi unaleta furaha na kukaa kama uchaguzi unaleta huzuni. Kwa nini kuchagua mema hutupatia furaha? Je, ni wakati gani umehisi furaha kwa sababu ulifanya uchaguzi sahihi?
-
Imbeni kwa pamoja wimbo kuhusu furaha ambayo huja kutokana na utiifu, kama vile “When We’re Helping” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto 198), na waombe watoto kusikiliza kile kinachotufanya tuwe na furaha. Acha watoto wafanye zamu kujifanya kuwa ni mzazi akiwataka watoto wengine kufanya jambo fulani. Wafanye watoto wengine wajifunze kutii kwa furaha.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Bwana daima atatimiza ahadi Zake.
Kuelewa kwamba Bwana anatimiza ahadi Zake kunaweza kuwasaidia watoto kujenga imani yao Kwake na tumaini lao katika kutii amri Zake.
Shughuli za Yakini
-
Waombe watoto kuzungumzia baadhi ya ahadi ambazo wamefanya, kama vile ahadi waliyofanya kwa rafiki au maagano waliyofanya kwenye ubatizo. Kwa nini wakati mwingine ni vigumu kutunza ahadi zetu? Kwa nini ni muhimu kutunza ahadi zetu? Soma kishazi kifuatacho: “Bwana Mungu atatimiza maagano yake aliyoagana na watoto wake” (2 Nefi 6:12). Shiriki mfano wa jinsi Mungu alivyotunza maagano Yake, hata kama baraka hazikuja mara moja.
-
Weka picha ya Yesu pembeni mwa picha ya mtoto. Soma 2 Nefi 7:1, na elezea kwamba wakati watu wa Mungu wanapoacha kutii injili Yake, inakuwa kana kwamba wame “mtaliki” Yeye. Ondoa picha ya mtoto pembeni mwa picha ya Yesu kuonyesha kwamba pale tunapokuwa hatutunzi maagano yetu, kama vile agano la ubatizo, tunajitenga na Baba wa Mbinguni na Mwokozi. (Kupitia upya maagano ya ubatizo, ona M&M 20:37.) Ni kwa jinsi gani Upatanisho wa Mwokozi huturuhusu kurudi tena karibu na Yeye? Mnapojadili hili, waalike watoto kurudisha picha zikaribiane tena.
Yesu Kristo huniokoa kutokana na dhambi na kifo.
Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia 2 Nefi 9:10–23 kuwasaidia watoto kujifunza kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wao?
Shughuli za Yakini
-
Waombe watoto wakusaidie kuchora njia ubaoni, na waalike kuongeza baadhi ya vikwazo au vizuizi katika njia. Someni pamoja 2 Nefi 9:10, na waalike watoto kuvipa majina vizuizi kwenye njia kwa maneno kutoka katika mstari huu ambayo yanaelezea vikwazo ambavyo vingeweza kutuzuia kurudi kwa Mungu. Kisha zungumza kuhusu jinsi Yesu Kristo alivyoshinda vizuizi hivi kwa ajili yetu (ona 2 Nefi 9:21–23), na unapofanya hivyo, waalike watoto kufuta vizuizi.
-
Onyesha picha ya Adamu na Hawa, kama vile Wakiondoka Bustani ya Edeni (ChurchofJesusChrist.org). Eleza kwamba wakati Adamu na Hawa walipokula tunda ambalo Mungu aliwaambia wasile katika Bustani ya Edeni, walileta dhambi na kifo katika ulimwengu. Onyesha picha ya Yesu Kristo. Kuwasaidia watoto kuelewa jinsi Yesu alivyoshinda dhambi na kifo, simulia hadithi ya mtu aliyetumbukia shimoni, inayopatikana kwenye wazo la kwanza la kufundisha chini ya “Watoto Wadogo” katika muhtasari huu. Kisha waombe watoto kuchora picha ya hadithi hii au kuiigiza. Soma 2 Nefi 9:21–23, na utoe ushuhuda wako wa Yesu Kristo na Upatanisho Wake.
-
Msaidie kila mtoto kupata wimbo kuhusu Upatanisho wa Mwokozi kwenye aidha kitabu cha nyimbo za kanisa au Kitabu cha Nyimbo za Watoto (vielezo kwenye vitabu hivi vinaweza kusaidia). Waalike watoto kutafuta na kushiriki vifungu vya maneno kutoka kwenye wimbo ambavyo huelezea kile Yesu alichofanya kwa ajili yetu. Waombe watoto kushiriki mawazo na hisia zao kuhusu Upatanisho wa Mwokozi, au shiriki ushuhuda wako.
Nitabarikiwa ninapofuata ushauri wa Mungu.
Wasaidie watoto kujenga msingi imara wa uaminifu kwa Mungu ili kwamba kadiri ufahamu na uwezo wao unapoongezeka, wataendelea kumtegemea Yeye na kufuata ushauri Wake.
Shughuli za Yakini
-
Waalike watoto wakuambie kuhusu jambo fulani wanalolijua sana, kama vile kitabu wanachokipenda sana au jambo wanalolipenda sana. Muombe mtoto asome 2 Nefi 9:20, na shuhudia kwamba Mungu “[anafahamu] vitu vyote.” Kwa nini ni muhimu kwetu kujua kwamba Mungu anafahamu vitu vyote?
-
Waombe watoto wafikirie kwamba walimsikia rafiki akisema kwamba amri au mafundisho ya Kanisa ni ya kijinga. Ni nini wangesema kwa rafiki yao? Kwa nini ni muhimu kuamini ushauri wa Mungu hata kama hatuuelewi kikamilifu? Wahimize watoto kutazama kwenye 2 Nefi 9:20, 28–29, and 42–43 kwa ajili ya msaada wa kutafakari na kujadili maswali haya.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Wasaidie watoto kufikiria jinsi wanavyoweza kufundisha familia zao kile walichojifunza kuhusu Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Kwa mfano, wangeweza kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kuelezea jinsi Mwokozi anavyotusaidia kushinda dhambi na kifo.