Njoo, Unifuate
Agosti 5–11. Warumi 1–6 ‘Uweza wa Mungu uuletao Wokovu’


Agosti 5–11. Warumi 1–6: ‘ Uweza wa Mungu uuletao Wokovu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2019 (2019)

Agosti 5–11. Warumi 1–6.“ Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2019

Picha
Paulo akiandika waraka

Agosti 5–11

Warumi 1–6

“Uweza wa Mungu uuletao Wokovu”

Je, ni ushawishi gani unaupata unaposoma Warumi 1–6? Ushawishi huu unaweza kukusaidia kuchagua kutoka kwenye mawazo yafuatayo ya kufundishia.

Andika Misukumo Yako

Picha
ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Waalike watoto kushiriki kile walichofanya katika kuitikia mialiko yoyote uliyowapa katika somo la wiki iliyopita. Kwa mfano, je, waliongea na familia zao kuhusu maangamizo ya meli baharini yaliyoelezwa katika Matendo ya Mitume 27 na kuhusu kumfuata nabii?

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho

Watoto Wadogo

Warumi 1:16–17

Ninaweza kuonyesha imani yangu katika Yesu Kristo kwa kumfuata Yeye.

Paulo alifundisha kwamba injili ina uwezo wa kuleta wokovu kwa kila mtu ambaye anaishi kwa imani katika Yesu Kristo. Je, unawezaje kuwasaidia watoto kuonyesha imani yao katika Yesu Kristo kwa kumfuata yeye?

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto kuitafuta Rumi kwenye ramani. Eleza kwamba kitabu cha Warumi kina barua ambayo Paulo aliandika kwa Watakatifu wa huko Rumi ili kuwasaidia kuelewa kanuni za injili kama vile imani.

  • Wasomee watoto Warumi 1:17, na wasaidie kukariri kirai “Wenye haki wataishi kwa imani.” Unaweza kupangia kila mtoto neno moja katika kirai na uwaombe waseme neno hilo unapowaonyesha. Elezea kwamba kirai hiki kinamaanisha kwamba hatuna budi kila siku kuishi kwa imani katika Yesu Kristo. Je, watoto wanajua imani ni nini? Onyesha picha ya Yesu Kristo na eleza kwamba tunaamini kuwa yeye yupo kweli hata kama hatujamwona. Hii ni imani—kusadiki katika kitu hata kama hatujakiona.

  • Eleza kwamba tunaonyesha imani zetu katika Yesu Kristo kwa kumtii Yeye. Ficha picha humo chumbani ya watu wakifanya kile ambacho Yesu ametutaka tufanye. Acha watoto wachuke zamu kutafuta na kuelezea picha. Je, tunaweza kufanya nini ili kumfuata Yesu?

  • Mfumbe macho mmoja wa watoto, na mwongoze kuvuka chumba kuelekea picha ya Yesu. Acha kila mtoto apate zamu. Wasaidie watoto kuelewa kwamba hawana budi kufuata mafundisho ya Yesu kama vile walivyofuata maelekezo yako.

Warumi 6:1–11

Kubatizwa ni kama kuwa mtu mpya.

Watoto unaowafundisha wanajitayarisha kwa ubatizo. Wanaweza kujifunza nini kuhusu ubatizo kutokana na maelekezo ya Paulo “kuenenda katika upya wa uzima”?

Shughuli Yamkini

  • Waalike watoto kurudia kirai “Kuenenda katika upya wa uzima” (Warumi 6:4). Eleza kwamba wakati tunapobatizwa, tunasamehewa dhambi zetu. Tunayo nafasi ya kusonga mbele kwa kufanya chaguzi nzuri, kutubu wakati tunapofanya makosa, na kujitahidi kuwa zaidi kama Yesu. Tumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kuwafundisha watoto kwamba ubatizo unatusaidia kuwa mtu mpya.

  • Waambie watoto jinsi ulivyojisikia wakati ulipobatizwa, na waalike kushiriki uzoefu wao wakati walipohudhuria ubatizo. Waalike kuchora picha zao wenyewe juu ya siku ya ubatizo wao baadaye na waelezee kile wanachoweza kufanya ili kujitayarisha kwa ubatizo wao.

  • Imba pamoja na watoto wimbo kuhusu ubatizo, kama vile “When I Am Baptized” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto 103) Tunajifunza nini kuhusu ubatizo kutoka wimbo huu?

Picha
mvulana akibatizwa

Ubatizo unaashiria kuanza maisha mapya kama mfuasi wa Kristo.

Picha
ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho

Watoto Wakubwa

Warumi 1:16–17

Ninaweza kuonyesha imani yangu katika Yesu Kristo kwa kumfuata Yeye.

Paulo alifundisha kwamba injili ina uwezo wa kuleta wokovu kwa kila mtu ambaye anaishi kwa imani katika Yesu Kristo. Imani ni kanuni ya kwanza ya injili. Inatuhamasisha kutii amri. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto waelewe vyema imani?

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto kutafuta Rumi kwenye ramani. Wasaidie watoto kuelewa kwamba wiki chache zijazo, watajifunza kutoka kwenye barua Paulo alizoandika kwa waumini wa Kanisa katika sehemu mbali mbali, kuanzia na barua yake kwa Warumi.

  • Andika maandishi kutoka Warumi 1:16 ubaoni, ukibadilisha maneno machache na mapengo. Waombe watoto kutafuta kwenye maandiko na kujaza mapengo. Taja wazi kirai “Siionei haya injili ya Kristo,” na waalike watoto kuelezea kirai hiki kinamaanisha nini kwao.

  • Mwalike mtoto kusoma kwa sauti Warumi 1:17, na waombe watoto wengine kusikiliza neno ambalo litarudiwa. Maana ya “kuishi kwa imani” ni nini? Wasaidie watoto kutafuta ufafanuzi wa imani katika nyenzo kama vile Mwongozo wa Maandiko, “Imani,” scriptures.lds.org. Je, ni kwa jinsi gani maisha yetu yangekuwa tofauti kama tusingekuwa na imani katika Yesu Kristo?

  • Waonyeshe watoto mmea na mbegu, na waulize jinsi tunavyosaidia mbegu kuwa mmea. Eleza kwamba wakati tunapopanda na kunyunyizia maji mbegu, tunaonyesha kwamba tuna imani kwamba itaota na kukua. Tunaonyeshaje kwamba tuna imani katika Yesu Kristo? Fikiria kuimba wimbo kuhusu imani, kama vile “Imani” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 96), kama sehemu ya shughuli hii.

Warumi 3:23–24

Sisi wote tunamhitaji Yesu Kristo ili tusamehewe dhambi zetu.

Paulo aliwataka Warumi waelewa kwamba wokovu unakuja tu kupitia Yesu Kristo na neema Yake. Tafakari jinsi unavyoweza kufundisha ukweli huu kwa watoto.

Shughuli Yamkini

  • Mwalike mmoja wa watoto kusoma Warumi 3:23–24. Watoto wanafikiria aya hizi zinatufundisha nini sisi? Eleza kwamba “neema” katika aya 24 inamaanisha karama ya Mwokozi ya upendo na rehema, inayofanya iwezekane kwetu sisi kupokea msamaha wa dhambi zetu.

  • Ning’iniza zawadi au picha juu kwenye ukuta au sehemu nyingine ambayo watoto hawawezi kufikia wao wenyewe. Waache wajaribu kuifikia, na fananisha hii na kile Paulo anafundisha katika Warumi 3:23. Kisha wasaidie kuifikia. Mwokozi amefanya nini kwa ajili yetu ambacho hatuwezi kujifanyia wenyewe? Waalike watoto kushiriki jinsi wanavyojisikia kuhusu Mwokozi wakati wanapofikiri kuhusu kile alichofanya kwa ajili yao.

Warumi 6:1–11

Kubatizwa ni kama kuwa mtu mpya.

Paulo alifundisha kwamba ubatizo unaashiria kifo na Ufufuko wa Kristo. Pia unaashiria “kifo” cha utu wetu wenye dhambi na kuinuliwa juu “kuenenda katika upya wa uzima” (Warumi 6:4). Tunarejesha upya ahadi yetu ya kuenenda katika upya wa uzima kila wakati tunapopokea sakramenti.

Shughuli Yamkini

  • Mwalike mtoto asome Warumi 6:3–6. Je, Paulo alisema ubatizo ni nini “katika mfano wa”?

  • Jadili ni kwa namna gani ubatizo unaashiria kifo na ufufuko. Fikiria kuonyesha video “Ubatizo wa Yesu” (LDS.org). Je, kwa nini kifo na ufufuko ni viashiria vizuri vya kile kinachotokea wakati tunapobatizwa?

  • Someni pamoja sala za Sakramenti (ona Mafundisho na Maagano 20:77 79). Wakumbushe watoto kwamba tunapopokea sakramenti, tunafanya upya ahadi tulizofanya wakati tulipobatizwa kumfuata Yesu Kristo. Je, ni kwa jinsi gani Sakramenti inatusaidia “kutembea katika upya wa uzima”?

  • Waalike watoto kutengeneza mabango ambayo yanaonyesha nini inamaanisha kwao “kutembea katika upya wa uzima.” Watoto wanaweza kuning’iniza hivi katika vyumba vyao ili kuwasaidia kukumbuka kufanya chaguzi nzuri.

Picha
ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Wahimize watoto kuwaomba wanafamilia wawajulishe wakati wanapoona kuwa watoto wanafanya kitu ambacho kinaonyesha imani.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Jenga imani ya watoto. Ili kuwasaidia watoto kujenga kujiamini kwamba wanaweza kujifunza injili wao wenyewe, wasifu wanaposhiriki darasani.

Chapisha