“Septemba 6–12. Mafundisho na Maagano 98–101: ‘Tulieni na Jueni kuwa Mimi ni Mungu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Septemba 6–12. Mafundisho na Maagano 98–101,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2021
Septemba 6–12
Mafundisho na Maagano 98–101
“Tulieni na Jueni Kuwa Mimi ni Mungu”
Je, ni aina zipi za changamoto au majaribu ambayo watu katika darasa lako hukabiliwa nayo? Ni aina gani ya maneno ya ushauri na faraja kwenye Mafundisho na Maagano 98–101 yanaweza kuwasaidia?
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Unaweza kuwaalika washiriki wa darasa kuelezea kitu walichojifunza kutoka Mafundisho na Maagano 98–101 kilichowasaidia katika jaribu au changamoto ambayo wamekuwa wakikabiliwa nayo.
Fundisha Mafundisho
Mafundisho na Maagano 98:1–3, 11–16, 23–30, 37; 101:2–5, 9–16
Majaribu yetu yanaweza kufanya kazi pamoja kwa faida yetu.
-
Mateso na upinzani tunaopitia leo vinaweza kuwa tofauti na kile ambacho Watakatifu walikumbana nacho huko Missouri mwaka 1833, lakini ushauri wa Bwana katika Mafundisho na Maagano 98 bado unafaa. Ili kuwasaidia watu katika darasa lako kujifunza kutoka kwenye ushauri huu, zingatia kuandika maswali kama yafuatayo ubaoni: Je, ni kwa mtazamo upi Bwana huwataka Watakatifu Wake kuutazama upinzani? Je, Bwana anatutaka tuitikie mateso kwa njia gani? Washiriki wa darasa wangeweza kufanya kazi katika vikundi vidogo ili kupata majibu katika Mafundisho na Maagano 98:1–3, 11–16, 23–30 na kisha kujadiliana wanachojifunza. Je, ni ukweli gani tunaupata ambao unaweza kutusaidia kuwa wanafunzi bora zaidi wa Yesu Kristo? Maneno kwenye “Nyenzo za Ziada” yangeweza kuongezea kwenye mjadala huu.
-
Katika nyakati za mateso au majaribu, ujumbe huu kutoka sehemu ya 98 na 101 unaweza kusaidia: Bwana atatusaidia kama tuko tayari kumwamini Yeye. Ili kuwasaidia washiriki wa darasa kupata ujumbe huu, unaweza kuandika orodha zifuatazo za mistari kwenye ubao na uwaalike washiriki wa darasa lako kuchagua michache ya kusoma: Mafundisho na Maagano 98:1–3, 11–12, 37; 101:2–5, 9–16. Waombe kushiriki na wengine kile walichokipata ambacho kinawahimiza kumuamini Bwana. Mistari hii inafundisha nini kuhusu jinsi ya kuweka tumaini letu katika Bwana? (Tazama pia Linda S. Reeves, “Dai Baraka za Maagano Yako,” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 118–20.)
Mafundisho na Maagano 101:1–8, 43–62
Kufuata ushauri wa Mungu hutusaidia kutuweka salama.
-
Je unawezaje kuwasaidia washiriki wa darasa kutambua usalama ambao huja wakati “tunapoisikiliza sauti ya Bwana”? (mstari wa 7). Pengine ungeweza kuwaalika washiriki wachache darasani kuigiza fumbo katika Mafundisho na Maagano 101:43–62 wakati mshiriki mwingine wa darasa akilisoma kwa sauti. Kisha mngeweza kujadiliana maswali kama haya: Je, vipengele tofauti vya fumbo vingeweza kuwakilisha nini? Ni kipi kiliwasababisha watumishi kupoteza shamba la mizabibu? Ni somo lipi tunalojifunza kutoka kwenye matendo ya watumishi? Tunajifunza nini kuhusu Bwana kutokana na matendo ya bwana mwenye shamba? Pia ingeweza kusaidia kulinganisha mistari 1–8 na mistari 47–51 na kujadiliana jinsi tunavyoweza kuwa “waaminifu na wenye hekima” katika juhudi zetu za kuijenga Sayuni katika maisha yetu binafsi, nyumbani mwetu, na kama Kanisa.
Nyenzo za Ziada
Kugeuza shavu lingine kunahitaji ujasiri wa Kikristo.
Mzee Robert D. Hales alifundisha:
“Baadhi ya watu kimakosa hufikiria kwamba majibu kama vile kunyamaza, upole, kutoa msamaha, na kutoa ushuhuda wa unyenyekevu ni kutoonyesha hisia au udhaifu. Lakini ‘kuwapenda adui [zetu], kuwaombea wanaotuudhi [sisi], kuwatendea mema wanaotuchukia [sisi], na kuwaombea wanaotutumia [sisi] kwa chuki na kutunyanyasa [sisi]’ (Mathayo 5:44) huhitaji imani, nguvu, na zaidi ya yote, ujasiri wa Kikristo. …
“Tusipolipiza kisasi—tukigeuza shavu lingine na kuzuia hisia za hasira—sisi pia tunasimama na Mwokozi. Tunaonesha upendo Wake, ambao ni nguvu pekee inayoweza kudhibiti mabaya na kuwajibu washitaki wetu bila ya kuwashitaki wao. Huo si udhaifu. Huo ni Ujasiri wa Kikristo” (“Ujasiri wa Kikristo, Gharama ya Ufuasi,” Ensign au Liahona, Nov. 2008, 72).
Kusamehe siyo kupuuza.
Elder Kevin R. Duncan alisema: “Akina kaka na akina dada, tafadhali msielewe vibaya. Kusamehe siyo kupuuza. Hatupuuzi tabia mbaya au kuruhusu watu wengine kututendea mabaya kwa sababu ya masumbuko yao, maumivu, au mapungufu yao. Lakini tunaweza kupata uelewa mzuri na amani tunapoona kwa mtazamo mpana. … Msamaha ni kanuni tukufu, ya uponyaji. Hatuhitaji kuwa waathirika mara mbili. Tunaweza kusamehe” (“marhamu ya Uponyaji wa Msamaha,” Ensign au Liahona, Mei 2016, 35).