“Wewe ni Mwalimu katika Kanisa la Yesu Kristo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano Jipya 2023 (2022.)
“Wewe ni Mwalimu katika Kanisa la Yesu Kristo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2023
Wewe ni Mwalimu katika Kanisa la Yesu Kristo
Umeitwa na Mungu kufundisha watoto Wake katika njia ya Mwokozi. Umesimikwa katika wito huu kwa mamlaka ya ukuhani Wake mtakatifu. Hata kama wewe sio mwalimu mzoefu, unapoishi kwa kustahili, kusali kila siku, na kujifunza maandiko, Baba wa Mbinguni atakupatia ushawishi na nguvu za Roho Mtakatifu ili kukusaidia kufanikiwa (ona 2 Nefi 33:1).
Wale waliowekwa chini ya uangalizi wako ni watoto wa Baba wa mbinguni, na Yeye anajua kile wanachohitaji na jinsi ya kuwafikia vyema. Kwa sala unapotafuta ushawishi wa Roho Mtakatifu, Yeye atakuongoza wakati wa maandalizi yako na wakati unapofundisha. Atakufunulia kile unachopaswa kusema na kile unachopaswa kufanya (ona 2 Nefi 32:5).
Madhumuni muhimu ya kufundisha injili na kujifunza ni kuzidisha uongofu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Lengo lako kama mwalimu ni kuwasaidia wale unaowafundisha kufanya kila wawezacho kuwa waongofu zaidi—juhudi ambazo huenda zaidi ya muda wa darasani. Waalike wale unaowafundisha kushiriki kikamilifu katika kujifunza kuhusu Yesu Kristo na injili Yake na kutendea kazi yale wanayojifunza. Wahimize kufanya kujifunza kwao binafsi na kama familia nje ya darasa kuwa chanzo cha msingi kwao cha kujifunza injili. Wanapotenda kwa imani kwa kujifunza kama watu binafsi na familia, watamwalika Roho katika maisha yao na ni Roho ndiye aletaye uongofu wa kweli. Kila kitu ufanyacho kama mwalimu hakina budi kuelekeza katika dhumuni hili takatifu.
Fundisha tu mafundisho ya injili ya urejesho ya Yesu Kristo kama yanavyopatikana katika maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho. Mafundisho safi—ya milele, ukweli usiobadilika uliofundishwa na Mungu na watumishi Wake—humwalika Roho na yana nguvu ya kubadilisha maisha.
Wito wa kufundisha ni wajibu mtakatifu, na ni kawaida kuhisi kuzidiwa wakati mwingine. Lakini kumbuka kwamba Baba yako wa Mbinguni ndiye aliyekuita, na Yeye hatakuacha kamwe. Hii ni kazi ya Bwana, na unapohudumu “kwa moyo, uwezo, akili na nguvu zako zote” (Mafundisho na Maagano 4:2), Yeye atapanua uwezo, vipawa, na vipaji vyako na huduma yako itabariki maisha ya wale unaowafundisha.