Vitabu vya Maelekezo na Miito
27. Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Walio Hai


“27. Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Walio Hai,” Kurasa Zilizochaguliwa Kutoka Kitabu cha Maelezo ya Jumla (2023).

“27. Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Walio Hai,” Kurasa Zilizochaguliwa Kutoka Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

bibi na bwana harusi

27.

Ibada za Hekaluni kwa ajili ya Walio Hai

27.0

Utangulizi

Hekalu ni nyumba ya Bwana. Hekalu hutuelekeza kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Katika mahekalu, tunashiriki katika ibada takatifu na kufanya maagano na Baba wa Mbinguni ambayo hutuunganisha kwake na kwa Mwokozi wetu. Maagano haya na ibada hizi zinatuandaa kurudi kwenye uwepo wa Baba wa Mbinguni na kuunganishwa pamoja kama familia milele.

Katika maagano na ibada za Hekaluni, “nguvu za uchamungu hujidhihirisha” (Mafundisho na Maagano 84:20).

Maagano na ibada za hekaluni ni takatifu. Ishara zinazohusiana na maagano ya hekaluni hazipaswi kujadiliwa nje ya hekalu. Wala hatupaswi kujadili taarifa takatifu tunazoahidi hekaluni kutozifichua. Hata hivyo, tunaweza kujadili madhumuni ya msingi na mafundisho ya maagano ya hekaluni na ibada na hisia za kiroho tulizokuwa nazo katika hekalu.

Viongozi wa kata na kigingi wanajadili taarifa katika sura hii na waumini wanaojitayarisha kupokea endaumenti au ibada za kuunganishwa.

27.1

Kupokea Ibada za Hekaluni

27.1.1

Kujitayarisha Kupokea Ibada za Hekaluni

Waumini wanapaswa kujitayarisha wenyewe kiroho kupokea ibada za hekaluni na kufanya na kuheshimu maagano ya hekaluni.

Wazazi wana jukumu la msingi la kuwasaidia watoto wao wajiandae kupokea baraka za hekaluni. Viongozi wa vigingi na kata, akina kaka na akina dada wanaohudumu na jamaa wa waumini wanawasaidia wazazi katika jukumu hili.

Nyenzo za kuwasaidia waumini kujiandaa kupokea ibada za hekaluni zinapatikana kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org.

Waumini ambao wanajitayarisha kupokea endaumenti zao au kuunganishwa na mume au mke wanahimizwa kushiriki katika kozi ya matayarisho ya hekaluni 25.2.8).

27.1.3

Waumini Wenye Ulemavu wa Kimwili

Waumini wenye kustahili ambao wana ulemavu wa kimwili wanaweza kupokea ibada zote za hekaluni. Waumini hawa wanahimizwa kuhudhuria hekaluni pamoja na jamaa au marafiki ambao tayari wamepokea endaumenti zao wa jinsia sawa na yao ambao wanaweza kuwasaidia. Kama waumini hawawezi kuhudhuria pamoja na mwanafamilia au rafiki, wanaweza kulitaarifu hekalu mapema ili kuona ni matayarisho gani yanaweza kufanywa.

27.1.4

Msaada wa Tafsiri au Ukalimani

Kama waumini wanahitaji msaada wa tafsiri au ukalimani, wanapaswa kuwasiliana na hekalu mapema kuona kama huduma hiyo inapatikana.

27.1.5

Mavazi ya Kuvaa Hekaluni

Waumini wanapokwenda hekaluni, wanapaswa kuvaa aina ya mavazi yanayofanana na yale wanayovaa wakati wa mkutano wa sakramenti.

Ona 27.3.2.6 kwa ajili ya taarifa kuhusu mavazi ya kuvaa kwenye ndoa ya hekaluni au kuunganishwa.

Ona 38.5 kwa ajili ya taarifa kuhusu:

  • Mavazi ya kuvaa wakati wa ibada za endaumenti na kuunganishwa.

  • Jinsi ya kupata, kuvaa na kujali nguo na mavazi ya hekaluni.

27.1.6

Uangalizi wa Watoto

Watoto lazima wawe na uangalizi wa mtu mzima kama wapo kwenye viwanja vya hekalu. Wafanyakazi wa hekaluni wanapatikana kuwaangalia watoto katika hali zifuatazo pekee:

  • Kama wanaunganishwa na wazazi

  • Kama wanaangalia kuunganishwa kwa ndugu zao walio hai, ndugu wa kambo, au ndugu zao wa mzazi mmoja.

27.1.7

Kukutana na Waumini baada ya Kupokea Ibada za Hekaluni

Waumini mara nyingi wana maswali baada ya kupokea ibada za hekaluni. Wanafamilia waliopokea endaumenti, askofu, viongozi wengine wa kata na akina kaka na akina dada wahudumiaji wanaweza kukutana na waumini kujadili uzoefu wao wa hekaluni.

Nyenzo za kusaidia kujibu maswali zinapatikana kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org.

27.2

Endaumenti

Neno endaumenti linamaanisha “tunu.” Endaumenti ya hekaluni ni tunu kutoka kwa Mungu ambayoo kupitia hiyo anawabariki watoto Wake. Baadhi ya tunu ambazo waumini wanapokea kupitia endaumenti ya hekaluni hujumuisha:

  • Ufahamu mkubwa wa madhumuni na mafundisho ya Bwana.

  • Uwezo wa kufanya vyote ambavyo Baba wa Mbinguni anataka watoto Wake wafanye.

  • Mwelekeo mtakatifu wakati wa kumtumikia Bwana, familia zao na wengine.

  • Ongezeko la tumaini, faraja na amani.

Ukamilifu wa baraka hizi unategemea juu ya uaminifu kwenye injili ya Yesu Kristo.

Endaumenti inapokelewa katika sehemu mbili. Katika sehemu ya kwanza, mtu anapata ibada ya mwanzo inayoitwa ibada ya utangulizi. Ibada ya utangulizi pia inajulikana kama kuoshwa na kupakwa mafuta (ona Kutoka 29:4–9). Ibada hii inajumuisha baraka maalumu zinazohusiana na urithi mtukufu wa mtu na uwezekano wake wa kuwa.

Wakati wa ibada ya utangulizi, muumini anaruhusiwa kuvaa gamenti za hekaluni. Gamenti inawakilisha uhusiano wake binafsi pamoja na Mungu na msimamo wa kutii maagano yaliyofanywa hekaluni. Waumini wanapokuwa waaminfu kwenye maagano yao na kuvaa gamenti ipasavyo maisha yao yote, gamenti hiyo pia hutumika kama ulinzi. Kwa maelezo kuhusu kuvaa na kuitunza gamenti, ona 38.5.5.

Katika sehemu ya pili ya endaumenti, mpango wa wokovu unafundishwa, ukijumuisha Uumbaji, Kuanguka kwa Adamu na Hawa, Upatanisho wa Yesu Kristo, Ukengeufu na Urejesho. Waumini pia wanapokea maelekezo juu ya jinsi ya kurudi kwenye uwepo wa Bwana.

Katika endaumenti, waumini wanaalikwa kufanya maagano matakatifu kama yafuatayo:

  • Kuishi sheria ya utiifu na kujitahidi kushika amri za Baba wa Mbinguni.

  • Kutii sheria ya dhabihu, ambayo inamaanisha kutoa dhabihu ili kusaidia kazi ya Bwana na kutubu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.

  • Kutii sheria ya injili ya Yesu Kristo, ambayo ni sheria ya juu ambayo aliifundisha wakati alipokuwa duniani.

  • Kutii sheria ya usafi wa kimwili, ambayo inamaanisha kwamba muumini awe na uhusiano wa kimapenzi na mtu mmoja pekee ambaye wamefunga ndoa kisheria na kihalali kulingana na sheria ya Mungu.

  • Kushika sheria ya wakfu, ambayo inamaanisha kwamba waumini wanaweka wakfu muda wao, vipaji vyao, na kila kitu ambacho Bwana amewabariki nacho ili kujenga Kanisa la Yesu Kristo dunuani.

Ndipo Baba wa Mbinguni anaahidi kwamba wale wanaobaki waaminifu kwa maagano yao ya hekaluni watapata tunu ya “uwezo kutoka juu” (Mafundisho na Maagano 38:32, 38; ona pia Luka 24:49; Mafundisho na Maagano 43:16).

27.2.1

Nani Anaweza Kupokea Endaumenti

Waumini wote watu wazima wa Kanisa wenye kuwajibika wanaalikwa kujiandaa kwa ajili ya, na kupokea endaumenti zao wenyewe. Ibada zote za awali lazima zifanywe na kurekodiwa kabla waumuni hawajapokea endaumenti (ona 26.3.1).

27.2.1.1

Waumini Waliobatizwa Karibuni

Waumini wapya watu wazima wanaostahili wanaweza kupokea endaumenti zao angalau mwaka mmoja kamili kutoka tarehe ya kuthibitishwa kwao.

27.2.1.2

Waumini Ambao Wana Mwenza Asiye na Endaumenti

Muumini anayestahili ambaye mwenza wake hana endaumenti anaweza kupokea endaumenti yake wakati masharti yafuatayo yanapokamilishwa:

  • Mwenza asiye na endaumenti anatoa idhini yake.

  • Muumini, askofu na rais wa kigingi wana imani kwamba majukumu yatokanayo na maagano ya hekaluni hayatakuwa ya kuharibu ndoa.

Masharti haya yanatumika ikiwa mwenza ni muumini wa Kanisa au la.

27.2.1.3

Waumini Ambao Wana Ulemavu wa Afya ya Akili

Waumini ambao wana ulemavu wa akili wanaweza kupokea endaumenti yao wenyewe kama:

  • Wamepokea ibada zote za awali (ona 26.3.1).

  • Wana uwezo wa kiakili kuelewa, kufanya na kushika maagano husika.

Askofu anashauriana na muumini huyo na, pale inapofaa, na wazazi wake. Yeye pia anatafuta maelekezo ya Roho. Anaweza kushauriana na rais wa kigingi.

27.2.2

Kuamua Siku ya Kupokea Endaumenti

Uamuzi wa kupokea endaumenti ni wa binafsi na unapaswa kufanywa kwa sala. Endaumenti ni baraka ya nguvu na ufunuo kwa wote ambao wanajiandaa kuipokea. Waumini wanaweza kuchagua kupokea endaumenti zao wenyewe wakati wanapokamilisha masharti yote yafuatayo:

  • Wana umri angalau wa miaka 18.

  • Wamemaliza shule ya upili au hawahudhurii tena shule ya upili, shule ya sekondari, au zinazofanana na hizo.

  • Mwaka mmoja kamili umepita tangu kuthibitishwa kwao.

  • Wanahisi matamanio ya kupokea na kuheshimu maagano ya hekaluni kwa maisha yao yote.

Waumini ambao wamepokea wito wa misheni au wanajitayarisha kuunganishwa hekaluni wanapaswa kupokea endaumenti.

Kabla ya kutoa kibali cha hekaluni kwa muumini kupokea endaumenti, askofu na rais wa kigingi wanapaswa kuhisi kwamba mtu huyo amejitayarisha kuelewa na kutunza maagano matakatifu ya hekaluni. Kustahili huku kunaamuliwa kwa ajili ya kila mtu binafsi.

27.2.3

Kupanga na Kuweka Ratiba ya Endaumenti

27.2.3.1

Kupokea Kibali kwa ajili ya Ibada za Walio Hai

Muumini lazima apokee kibali kwa ajili ya ibada za walio hai ili kuingia hekaluni na kupokea endaumenti. Kwa maelezo kuhusu vibali hivi, ona 26.5.1.

27.2.3.2

Kuwasiliana na Hekalu

Waumini ambao wanapanga kupokea endaumenti wanapaswa kuwasiliana na hekalu mapema ili kuweka Ratiba ya ibada.

27.2.3.3

Wasindikizaji kwa ajili ya Waumini Wanaopokea Endaumenti

Waumini wanaopokea endaumenti zao wenyewe wanaweza kumwalika muumini ambaye amekwishapata endaumenti wa jinsia sawa na yao kuwa kama msindikizaji na kuwasaidia wakati wa kikao cha endaumenti. Msindikizaji lazima awe na kibali cha hekaluni. Hekalu linaweza kutoa msindikizaji kama anahitajika.

27.3

Kuunganishwa kwa Mume na Mke

Kuunganishwa hekaluni kunamleta mume na mke pamoja kwa wakati huu na milele yote. Watapokea baraka hizi kama ni waaminifu kwa maagano wanayoyafanya hekaluni. Kupitia ibada hii, watoto wao wanaweza pia kuwa sehemu ya familia yao ya milele.

Viongozi wa Kanisa huwahimiza waumini wajitayarishe kufunga ndoa na kuunganishwa hekaluni. Katika nchi ambapo ndoa za hekaluni hazitambuliki kisheria, viongozi wa Kanisa walioidhinishwa au wengine wanaweza kufanya ndoa za kiserikali ambazo zinafuatiwa na uunganishwaji hekaluni (ona 38.3). Mpangilio huu unaweza pia kufuatwa wakati ndoa ya hekaluni huenda ikasababisha wazazi au wanafamilia wa karibu kuhisi wametengwa kwa sababu hawawezi kuhudhuria sherehe ya hekaluni.

27.3.1

Nani Anaweza Kuunganishwa Hekaluni

Waumini wote wa Kanisa wenye kuwajibika ambao hawajaoa au kuolewa wanaalikwa kujiandaa kwa ajili ya kuunganishwa hekaluni. Wale ambao wamefunga ndoa serikalini wanahimizwa kuunganishwa kwa muda na milele hekaluni haraka iwezekanavyo pale wanapokuwa wamejiandaa. Waumini lazima wawe na endaumenti kabla hawajaunganishwa (ona 27.2).

Wenza wanaounganishwa hekaluni lazima wawe (1)wameoana kiserikali kabla ya kuunganishwa au (2) wamefunga ndoa na kuunganishwa katika sherehe kama hiyo hekaluni. Ona 27.3.2.

27.3.1.2

Waumini Ambao Wana Ulemavu wa Afya ya Akili

Waumini ambao wana ulemavu wa akili wanaweza kuunganishwa kwa wenza wao au wachumba kama:

  • Wamepokea ibada zote za utangulizi, ikijumuisha endaumenti (ona 27.2.3.1).

  • Wana uwezo wa kiakili kuelewa, kufanya na kushika maagano husika.

Askofu anashauriana na muumini huyo na mwenza au mchumba wake. Pia hutafuta maelekezo ya Roho. Anaweza kushauriana na rais wa kigingi.

27.3.2

Kupanga na Kuweka Ratiba ya Ndoa ya Hekaluni au Kuunganishwa

27.3.2.1

Kupokea Kibali kwa ajili ya Ibada za Walio Hai

Muumini lazima apokee kibali kwa ajili ya ibada za walio hai ili aweze kuunganishwa kwa mwenza wake. Kwa maelezo kuhusu vibali hivi, ona 26.3.

27.3.2.2

Kuwasiliana na Hekalu

Waumini ambao wanapanga kuoana au kuunganishwa kwa mume au mke wanapaswa kuwasiliana na hekalu mapema ili kuratibu ibada hiyo.

27.3.2.3

Kupata Cheti cha Ndoa

Kabla ya kufunga ndoa, mume na mke lazima wapate leseni ya kisheria ya ndoa ambayo ni halali mahala pale ambapo ndoa itafungwa Kama wenza wanapanga kufunga ndoa na kuunganishwa wakati wa sherehe moja, lazima walete cheti halali cha ndoa hekaluni.

Wanandoa wanaounganishwa baada ya ndoa ya kiserikali, hawahitaji kuleta cheti cha ndoa hekaluni. Badala yake wanatoa tarehe na mahali pa ndoa yao ya kiserikali kama sehemu ya mchakato wa uthibitisho.

27.3.2.4

Wasindikizaji kwa ajili ya Bibi na Bwana Harusi

Dada mwenye endaumenti anaweza kufuatana na bibi harusi kumsaidia kwenye chumba cha kuvalia. Kaka mwenye endaumenti anaweza kufanya vivyo hivyo kwa bwana harusi. Msindikizaji lazima awe na kibali hai cha hekaluni. Hekalu linaweza kutoa msindikizaji kama itahitajika.

27.3.2.5

Nani Anafungisha Ndoa za Hekaluni au Kuunganishwa

Ndoa ya hakaluni au kuunganishwa kwa kawaida hufanywa na muunganishaji ambaye amepangiwa kwenye hekalu ambapo wanandoa wataoana au kuunganishwa. Kama mwanafamilia au jamaa ana mamlaka ya kuunganisha na amepangiwa kwenye hekalu ambapo maharusi wataoana au kuunganishwa, wanaweza kumwalika afungishe ndoa au kuunganisha.

27.3.2.6

Nguo Sahihi kwa ajili ya Ndoa ya Hekaluni au Kuunganishwa

Nguo ya Bibi harusi. Gauni la bibi harusi linalovaliwa hekaluni linapaswa liwe jeupe, lililosanifiwa kistaha na kwa kitambaa kizuri na kisicho na mapambo mengi. Pia gauni hilo linapaswa kufunika gamenti ya hekaluni. Kitambaa kinachoonyesha kinapaswa kuwekewa kitambaa kingine kwa ndani.

Ili kuendana na mavazi mengine yanayovaliwa hekaluni, gauni la bibi harusi linapaswa kuwa na mikono mirefu au mikono yenye urefu wa robo tatu. Magauni hayapaswi kuwa na mkia (ya kuburuza) isipokuwa kama mkia unaweza kubanwa juu au kutolewa kwa ajili ya sherehe ya kuunganishwa.

Hekalu linaweza kutoa gauni kama itahitajka au ikiwa mtu atapenda.

Nguo za Bwana harusi. Bwana harusi anavaa nguo za kawaida za hekaluni wakati wa kufunga ndoa au sherehe za kuunganishwa (ona 38.5:1 ona 38.5.2).

Nguo za Wageni. Wale ambao wanahudhuria ndoa au sherehe za kuunganishwa wanapaswa kuvaa nguo zinazofanana na zile ambazo wangevaa kwenye mkutano wa sakramenti. Waumini wanaokuja kwenye kuunganishwa moja kwa moja kutoka kwenye kikao cha endaumenti wanaweza kuvaa nguo za sherehe za hekaluni.

Maua. Maharusi na wageni wao hawapaswi kuvaa maua wakati wa kufunga ndoa au sherehe za kuunganishwa.

27.3.2.7

Kuvalishana Pete baada ya Ndoa ya Hekaluni au Kuunganishwa

Kuvalishana pete sio sehemu ya sherehe ya kuunganishwa hekaluni. Hata hivyo, maharusi wanaweza kuvalishana pete baada ya sherehe katika chumba cha kuunganisha. Maharusi hawapaswi kuvalishana pete wakati mwingine wowote au sehemu yoyote katika hekalu au viwanja vya hekalu.

Maharusi ambao wameoana na kuunganishwa katika sherehe hiyo hiyo wanaweza kuvalishana pete baadaye ili kuwashirikisha wanafamilia ambao hawakuweza kuhudhuria ndoa hekaluni. Kuvalishana pete hukupaswi kurudufu sehemu yoyote ya sherehe ya ndoa ya hekaluni au ya kuunganishwa. Wanandoa hawapaswi kula viapo baada ya kuoana au kuunganishwa hekaluni.

Wanandoa ambao walioana kiserikali kabla ya kuunganishwa kwao hekaluni wanaweza kuvalishana pete kwenye sherehe zao za kiserikali, kwenye kuunganishwa kwao au kwenye sherehe zote mbili.

27.3.4

Nani Anaweza Kuhudhuria Ndoa ya Hekaluni au Kuunganishwa

Wanandoa wanapaswa kuwaalika wanafamilia na marafiki wa karibu kwenye harusi ya hekaluni au kuunganishwa. Waumini wenye kuwajibika lazima wawe na endaumenti na wawe na kibali hai cha hekaluni ili kuhudhuria.

Rais wa kigingi anaweza kuidhinisha mtu ambaye hajabatizwa au asiye na endaumenti kwa sababu ya ulemavu wa akili kuangalia ndoa ya hekaluni au kuunganishwa kwa ndugu zake walio hai. Mtu huyo lazima:

  • Awe na umri angalau wa miaka 18.

  • Aweze kubakia mnyenyekevu wakati wa sherehe.

Rais wa kigingi anaandika barua akielezea kwamba mtu huyo ameruhusiwa kuangalia kuunganishwa huko. Barua hii inapelekwa hekaluni.

27.4

Kuwaunganisha Watoto Walio Hai kwa Wazazi

Watoto ambao wamezaliwa baada ya mama yao kuwa ameunganishwa kwa mume hekaluni wamezaliwa katika agano la muungano huo. Hawahitaji kupata ibada ya kuunganishwa kwa wazazi.

Watoto ambao hawakuzaliwa kwenye agano wanaweza kuwa sehemu ya familia ya milele kwa kuunganishwa kwa wazazi wao wa kuwazaa au wazazi waliowaasili. Watoto hawa wana haki ya baraka sawa na wale waliozaliwa katika agano.

27.4.2

Kuwasiliana na Hekalu

Wanandoa ambao wanataka watoto wao kuunganishwa kwao, au watoto wanaotamani kuunganishwa kwa wazazi wao waliofariki, wanapaswa kuwasiliana na hekalu mapema ili kupanga ratiba ya ibada hiyo.