Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 102


Sehemu ya 102

Kumbukumbu za muundo wa baraza kuu la kwanza la Kanisa, huko Kirtland, Ohio, 17 Februari 1834. Kumbu kumbu halisi ziliandikwa na Wazee Oliver Cowdery na Orson Hyde. Siku mbili baadaye, Nabii alifanya marejeo muhtasari ule siku iliyofuata, siku iliyofuata tena muhtasari ule uliosahihishwa ulikubaliwa kwa kura zote na baraza kuu kama “muundo na katiba ya baraza kuu” la Kanisa. Aya ya 30 hadi 32, inahusika na Baraza la Mitume Kumi na Wawili, iliongezwa mwaka 1835 chini ya maelekezo ya Joseph Smith wakati sehemu hii ikitayarishwa kwa ajili ya kuchapishwa katika Mafundisho na Maagano.

1–8, Baraza kuu limeanzishwa ili kutatua matatizo muhimu yanayojitokeza katika Kanisa; 9–18, Taratibu zinatolewa kwa ajili ya kusikiliza mashauri; 19–23, Rais wa baraza ndiye atoaye uamuzi; 24–34, Utaratibu wa kukata rufani unaelezwa.

1 Siku ya leo baraza kuu la makuhani wakuu ishirini na wanne limekusanyika katika nyumba ya Joseph Smith, Mdogo, kwa ufunuo, na kuanza kuunda baraza kuu la kanisa la Kristo, ambalo litaundwa na makuhani wakuu kumi na wawili, na rais mmoja au watatu, kama shauri litakavyohitaji.

2 Baraza kuu liliteuliwa kwa ufunuo kwa madhumuni ya kutatua matatizo muhimu ambayo yangeweza kujitokeza katika kanisa, ambayo hayangeweza kutatuliwa na kanisa au baraza la askofu ili kuziridhisha pande hizi.

3 Joseph Smith, Mdogo, Sidney Rigdon na Frederick G. Williams walikubalika kama marais kwa sauti ya baraza; na Joseph Smith, Mkubwa, John Smith, Joseph Coe, John Johnson, Martin Harris, John S. Carter, Jared Carter, Oliver Cowdery, Samuel H. Smith, Orson Hyde, Sylvester Smith, na Luke Johnson, makuhani wakuu, walichaguliwa kuwa baraza la kudumu kwa kanisa, kwa kura nyingi za baraza.

4 Wajumbe waliotajwa hapo juu waliulizwa kama wanakubali uteuzi wao, na kama watatenda katika ofisi ile kulingana na sheria ya mbinguni, ambapo wote walijibu kwamba wamekubali uteuzi wao, nao watazitumikia ofisi zao kulingana na neema ya Mungu iliyowekwa juu yao.

5 Na idadi iliyounda baraza, ambao walipiga kura katika jina na kwa ajili ya kanisa katika kuchagua majina ya wajumbe waliotajwa hapo juu walikuwa arobaini na watatu, kama ifuatavyo: makuhani wakuu tisa, wazee kumi na saba, makuhani wanne, na waumini wa kanisa kumi na watatu

6 Ilipigwa kura: kwamba baraza kuu halitakuwa na uwezo wa kuamua bila wajumbe saba waliotajwa hapo juu, au wawakilishi wao walioteuliwa rasmi kuwepo.

7 Hawa saba watakuwa na uwezo wa kuwateua makuhani wengine wakuu, ambao watawaona kuwa wanastahili na kuwa wanauwezo wa kutenda katika nafasi za wajumbe wasiokuwepo.

8 Ilipigwa kura: kwamba iwapo nafasi yoyote itatokea kutokana na kifo, kuondolewa kutoka katika nafasi kwa ajili ya kuvunja sheria, au kuondolewa kutoka katika mipaka ya serikali ya kanisa hili, kwa yeyote kati ya wajumbe waliotajwa hapo juu, itajazwa kwa uteuzi wa rais au marais, na kuungwa mkono na sauti ya baraza kuu la makuhani wakuu, litakaloitishwa kwa madhumuni hayo, ya kutenda katika jina la kanisa.

9 Rais wa kanisa, ambaye pia ni rais wa baraza, huteuliwa kwa ufunuo, na kuthibitishwa katika utawala wake kwa sauti ya kanisa.

10 Na ni kulingana na heshima ya ofisi yake yampasa kuwa kiongozi wa baraza la kanisa; na ni haki yake kusaidiwa na marais wengine wawili, walioteuliwa kwa jinsi hiyo hiyo ambayo yeye mwenyewe aliteuliwa.

11 Na ikiwa mmoja wapo au wote wawili walioteuliwa kumsaidia hawapo, yeye anao uwezo wa kuliongoza baraza bila ya msaidizi; na iwapo yeye mwenyewe hayupo, marais wengine wanao uwezo wa kuongoza badala yake, iwe wote au mmoja wao.

12 Wakati wowote baraza kuu la kanisa la Kristo likiwa limeanzishwa rasmi, kulingana na utaratibu uliotajwa, itakuwa ni wajibu wa wajumbe kumi na wawili kupiga kura kwa namba, kwa njia hiyo watabainisha nani kati ya hao kumi na wawili atazungumza kwanza, wakianza nambari moja na hivyo kuendelea hadi nambari kumi na mbili.

13 Wakati wowote baraza hili likutanapo kuamua shauri lolote, wajumbe hawa kumi na wawili watatafakari iwapo ni gumu au hapana; kama hapana, wawili tu kati ya wajumbe ndiyo watazungumza juu yake, kulingana na utaratibu ulioandikwa hapo juu.

14 Lakini ikiwa litadhaniwa kuwa gumu, wanne watateuliwa; na kama ni gumu zaidi, sita; lakini katika hali yoyote ile pasiteuliwe wazungumzaji zaidi ya sita.

15 Mshtakiwa, katika mashauri yote, anayo haki ya kutetewa na nusu ya wajumbe wa baraza, ili kuzuia kufedheheshwa au kutotendewa haki.

16 Na wajumbe walioteuliwa kuzungumza mbele ya baraza watalileta shauri, baada ya ushahidi kuchunguzwa, katika nuru yake ya kweli mbele ya baraza; na kila mtu ataongea kulingana na usawa na haki.

17 Wale wajumbe waliookota namba chanya, ambazo ni 2, 4, 6, 8, 10, na 12, ndiyo watu ambao watasimama kwa niaba ya mshtakiwa, na kuzuia fedheha na kutotendewa haki.

18 Katika mashauri yote mshtaki na mshtakiwa watakuwa na haki ya kuzungumza wenyewe mbele ya baraza, baada ya ushahidi kusikilizwa na wajumbe ambao wameteuliwa kuzungumza juu ya shauri hilo kumaliza kutoa maelezo yao.

19 Baada ya ushahidi kusikilizwa, wajumbe, mshtaki na mshtakiwa kuwa wamezungumza, rais atatoa uamuzi kulingana na ufahamu ambao ataupata juu ya kesi hiyo, na atawaomba wajumbe hao kumi na wawili kupitisha uamuzi huo kwa kura zao.

20 Lakini iwapo wajumbe waliobakia, ambao hawakuzungumza, au yeyote kati yao, baada ya kusikiliza ushahidi na maombi vizuri bila kuegemea kokote, wanagundua kosa katika uamuzi wa rais, wanaweza kulionyesha, na shauri litarudiwa kusikilizwa.

21 Na kama, baada ya marejeo ya usikilizaji wa makini, taarifa yoyote ya nyongeza itaonyeshwa juu ya shauri hilo, uamuzi utarekebishwa mara moja.

22 Lakini iwapo hakuna taarifa ya nyongeza iliyotolewa, uamuzi wa kwanza utasimama, na wingi wa baraza linao uwezo wa kuzingatia uamuzi.

23 Iwapo pana ugumu juu ya mafundisho au kanuni, kama hakuna maandishi ya kutosha kuliweka wazi shauri mawazoni mwa baraza, rais anaweza kuomba na kupata nia ya Bwana kwa ufunuo.

24 Makuhani wakuu, wawapo ngʼambo, wanao uwezo wa kuteua na kuunda baraza kwa jinsi ilivyoelekezwa, ili kutatua matatizo, wakati pande mbili hizi au mmoja kati yao itaomba hivyo.

25 Na baraza lililotajwa hapa la makuhani wakuu litakuwa na uwezo wa kumteua mmoja kati yao wenyewe kuliongoza baraza hilo kwa wakati huo.

26 Utakuwa ni wajibu wa baraza hilo kupeleka, haraka iwezekanavyo, nakala ya yaliyotendeka yenye maelezo kamili ya ushuhuda ulioambatana na uamuzi wao, kwa baraza kuu la kiti cha Urais wa Kwanza wa Kanisa.

27 Iwapo pande zote au moja wapo haikuridhika na uamuzi uliotolewa na baraza husika, wanaweza kukata rufaa kwa baraza kuu la kiti cha Urais wa Kwanza wa Kanisa, na kusikilizwa upya tena, shauri ambalo litaendeshwa, kulingana na utaratibu ulioandikwa, mwanzoni, kama vile uamuzi kama huo haukufanyika.

28 Baraza hili la makuhani wakuu ngʼambo litateuliwa tu wakati wa mashauri magumu sana ya kanisa; na hakuna mashauri ya mara kwa mara au ya kawaida yatakayotosheleza kuitwa kwa baraza la aina hiyo.

29 Makuhani wakuu wasafirio mbali na makao makuu au wale waliowekwa mbali wanao uwezo wa kusema endapo ni muhimu kuteuliwa kwa baraza hilo au hapana.

30 Kuna tofauti kati ya baraza kuu au makuhani wakuu wasafirio mbali na makao, na baraza kuu lisafirilo lenye jumla ya mitume kumi na wawili, katika maamuzi yao.

31 Kutoka kwenye maamuzi ya baraza la kwanza inawezekana kukata rufaa; lakini kutokana na maamuzi ya baraza la pili haiwezekani.

32 La pili linaweza tu kuulizwa na viongozi wakuu wa kanisa katika shauri la kuvunjwa kwa sheria.

33 Imeazimiwa: kwamba rais au marais wa kiti cha Urais wa Kwanza wa Kanisa watakuwa na uwezo wa kuamua iwapo shauri la aina hiyo, kama vile litakavyoweza kukatiwa rufaa, linayo haki ya kusikilizwa upya, baada ya kuchunguza rufani na ushahidi na maelezo yanayoambatana nayo.

34 Wajumbe hao kumi na wawili ndipo waliendelea kupiga kura au kura ya siri, ili kuamua nani azungumze kwanza, na yafuatayo yalikuwa matokeo yake, kwa majina: 1, Oliver Cowdery; 2, Joseph Coe; 3, Samuel H. Smith; 4, Luke Johnson; 5, John S. Carter; 6, Sylvester Smith; 7, John Johnson; 8, Orson Hyde, 9, Jared Carter; 10, Joseph Smith, Mkubwa; 11, John Smith; 12, Martin Harris.Baada ya sala mkutano uliahirishwa.

Oliver Cowdery,

Orson Hyde,

Makarani