Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 135


Sehemu ya 135

Tangazo la kifo cha kishahidi cha Joseph Smith Nabii na kaka yake, Hyrum Smith Patriaki, huko Carthage, Illinois, 27 Juni 1844. Hati hii ilijumuishwa mwishoni mwa toleo la 1844 la Mafundisho na Maagano, ambalo ilikuwa linakaribia kuwa tayari kwa uchapishaji wakati Joseph na Hyrum Smith walipouawa.

1–2, Joseph na Hyrum wauawa kifo cha kishahidi katika gereza la Carthage; 3, Nafasi ya juu kabisa ya Nabii yatangazwa kwa shangwe; 4–7, Damu yao isiyo na hatia yashuhudia ukweli na utakatifu wa kazi hii.

1 Ili kutia muhuri ushuhuda wa kitabu hiki na Kitabu cha Mormoni, tunatangaza mauaji ya kishahidi ya Joseph Smith Nabii, na Hyrum Smith Patriaki. Walipigwa risasi gerezani Carthage, mnamo 27 Juni 1844, kiasi cha saa kumi na moja jioni, na kundi la wahuni wenye silaha—waliojipaka rangi nyeusi—watu wapatao 150 hadi 200. Hyrum alipigwa kwanza na kuanguka kimya kimya, akigutia: Nimekufa! Joseph aliruka kutoka dirishani, na alipigwa na kufa alipokuwa akijaribu kuruka, akigutia: Ee Bwana Mungu wangu! Wote walipigwa risasi baada ya kuwa wamekufa, katika namna ya kinyama, na wote walipokea risasi nne.

2 John Taylor na Willard Richards, wawili kati ya Kumi na Wawili, walikuwa watu pekee katika chumba kile kwa wakati ule; wa kwanza alijeruhiwa kikatili kwa risasi nne, lakini kwa sasa amepona, wa pili, kwa majaliwa ya Mungu, aliepuka, pasipo hata tundu katika joho lake.

3 Joseph Smith, Nabii na Mwonaji wa Bwana, amefanya mengi, isipokuwa Yesu pekee yake, kwa ajili ya wokovu wa wanadamu katika ulimwengu huu, kuliko mwanadamu mwingine yeyote aliyeishi ndani yake. Katika kipindi kifupi cha miaka ishirini, amekileta Kitabu cha Mormoni, ambacho amekitafsiri kwa kipawa na uwezo wa Mungu, na amekuwa njia ya kukichapisha katika mabara mawili; amepeleka utimilifu wa injili isiyo na mwisho, ambayo imo ndani yake, kwenye robo nne za dunia; ameleta mafunuo na amri ambazo zinaunda kitabu hiki cha Mafundisho na Maagano, na maandishi mengine mengi ya busara na maelekezo kwa manufaa ya wanadamu; kimewakusanya maelfu mengi ya Watakatifu wa Siku za Mwisho, ameanzisha mji mkubwa, na ameacha sifa na jina ambalo haliwezi kuuawa. Aliishi vyema, na amekufa vyema machoni pa Mungu na watu wake; na kama wengi wa wapakwa mafuta wa Bwana katika siku za kale, ametia muhuri huduma yake na kazi zake kwa damu yake yeye mwenyewe; na vivyo hivyo kaka yake Hyrum. Katika maisha hawakugawanyika, na katika mauti hawakutenganishwa!

4 Wakati Joseph alipokwenda Carthage kujitoa mwenyewe kama sheria ilivyodhaniwa kudai, siku mbili au tatu kabla ya mauaji yake, alisema: “Ninakwenda kama kondoo kwa mchinjaji; lakini nimetulia kama asubuhi ya kiangazi; ninayo dhamira isiyo na hatia mbele za Mungu, na mbele za watu wote. Mimi nitakufa bila hatia, na bado itasemwa juu yangu—aliuawa kikatili.”—Asubuhi hiyo hiyo, baada ya Hyrum kuwa tayari kwenda—tuseme kwa mwuaji? ndiyo, kwani ndivyo ilivyokuwa—alisoma aya ifuatayo, karibuni na mwisho wa mlango wa kumi na mbili wa Etheri, katika Kitabu cha Mormoni, na akaukunja ukurasa ule:

5 Na ikawa kwamba niliomba kwa Bwana kwamba awape neema Wayunani, ili wapate kuwa na hisani. Na ikawa kwamba Bwana akasema nami kuwa: Kama hawana hisani haikuhusu wewe, umekuwa mwaminifu; kwa hiyo nguo zako zitafanywa safi. Na kwa sababu umeuona udhaifu wako, utafanywa kuwa mwenye nguvu, hata kwa kukaa katika mahali ambapo nimepatayarisha katika nyumba ya Baba yangu. Na sasa, mimi … ninaaga kwa Wayunani; ndiyo, na pia kwa ndugu zangu ambao ninawapenda, mpaka tutakapokutana mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ambapo watu wote watajua kwamba mavazi yangu hayajawekwa mawaa na damu yenu. Mashahidi hawa sasa wamekufa, na ushuhuda wao bado una nguvu.

6 Hyrum Smith alikuwa na umri wa miaka arobaini na minne hapo Februari, 1844, na Joseph Smith alikuwa na miaka thelathini na minane hapo Desemba, 1843; na tangu sasa na kuendelea majina yao yataorodheshwa miongoni mwa waliouawa kama mashahidi wa dini; na msomaji katika kila taifa atakumbushwa kwamba Kitabu cha Mormoni, na kitabu hiki cha Mafundisho na Maagano ya kanisa, vimegharimu damu iliyo bora ya karne ya kumi na tisa kuvileta kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu ulio haribiwa; na kwamba kama moto unaweza kuushambulia mti mbichi kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ni rahisi namna gani kuunguza miti mikavu kutakasa shamba la mizabibu la uharibifu. Waliishi kwa ajili ya utukufu; walikufa kwa ajili ya utukufu; na utukufu ndiyo thawabu yao ya milele. Kutoka umri mmoja hadi mwingine majina yao yatakwenda chini kwa wazao kama vito kwa ajili ya waliotakaswa.

7 Walikuwa hawana hatia yoyote ya uhalifu, kama mara kwa mara ilivyothibitika kabla, na walikuwa wamezuiliwa tu kifungoni kwa njama za wasaliti na watu waovu; na damu yao isiyo na hatia juu ya sakafu ya gereza la Carthage ni muhuri mkubwa uliobandikwa kwenye “Umormoni” ambao hauwezi kukataliwa na mahakama yoyote juu ya dunia, na damu yao isiyo na hatia juu ya nembo ya Jimbo la Illinois, pamoja na imani iliyovunjika kwa jimbo kama ilivyonenwa na gavana, ni ushahidi wa ukweli wa injili isiyo na mwisho ambao ulimwengu mzima hauwezi kukamisha; na damu yao isiyo na hatia juu ya bendera ya uhuru, na juu ya katiba kuu ya Muungano wa Mataifa ya Marekani ni balozi wa dini ya Yesu Kristo, ambayo itagusa mioyo ya watu waaminifu miongoni mwa mataifa yote; na damu yao isiyo na hatia, pamoja na damu isiyo na hatia ya waliouawa kama mashahidi wa dini wote chini ya madhabahu ile ambayo Yohana aliiona, italia kwa Bwana wa Majeshi hadi atakapolipiza kisasi cha damu hiyo juu ya dunia. Amina.