Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 15


Sehemu ya 15

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii kwa John Whitmer, huko Fayette, New York, Juni 1829 (ona kichwa cha habari cha sehemu ya 14). Ujumbe ni wa siri na wa kuvutia kibinafsi ambamo kwamba Bwana anasema juu ya lililojulikana tu kwa John Whitmer na Yeye mwenyewe. John Whitmer baadaye alikuja kuwa mmoja wa Mashahidi Wanane wa Kitabu cha Mormoni.

1–2, Mkono wa Bwana u juu ya ulimwengu wote; 3–6, Kuhubiri injili na kuziokoa nafsi ni jambo la thamani kubwa.

1 Sikiliza mtumishi wangu John, na sikiliza maneno ya Yesu Kristo, Bwana wako na Mkombozi wako.

2 Kwani tazama, ninasema nawe kwa ukali na kwa nguvu, kwani mkono wangu u juu ya ulimwengu wote.

3 Na nitakuambia wewe yale ambayo hakuna mtu ajuaye isipokuwa mimi na wewe pekee—

4 Kwani mara nyingi wewe umetamani kujua kutoka kwangu kwamba ni kipi ambacho kitakuwa na thamani kubwa kwako.

5 Tazama, umebarikiwa wewe kwa jambo hili, na kwa kusema maneno yangu ambayo nimekupa kulingana na amri zangu.

6 Na sasa, tazama, ninakuambia, kwamba jambo ambalo litakuwa la thamani kubwa kwako ni kutangaza toba kwa watu hawa, ili uweze kuzileta nafsi hizo kwangu, na kwamba uweze kupumzika pamoja nao katika ufalme wa Baba yangu. Amina.