Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 23


Sehemu ya 23

Mfululizo wa mafunuo matano yaliyotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Manchester, New York, Aprili 1830, kwa Oliver Cowdery, Hyrum Smith, Samuel H. Smith, Joseph Smith Mkubwa, na Joseph Knight Mkubwa. Kama matokeo ya matamanio ya dhati ya watu hawa watano waliotajwa ya kutaka kujua wajibu wao, Nabii alimwuliza Bwana na kupokea ufunuo kwa ajili ya kila mtu.

1–7, Wanafunzi hawa wa mwanzo wameitwa kuhubiri, kushawishi, na kuliimarisha Kanisa.

1 Tazama, ninasema na wewe Oliver, maneno machache. Tazama, wewe umebarikiwa, na huna hatia yoyote. Lakini jihadhari na majivuno, usije ukaingia majaribuni.

2 Fanya wito wako ujulikane kwa kanisa, na pia mbele ya ulimwengu, nao moyo wako utafunguliwa kuhubiri ukweli tangu leo na hata milele. Amina.

3 Tazama, ninasema na wewe, Hyrum, maneno machache; kwani na wewe pia huna hatia yoyote, na moyo wako umefunguliwa, na ulimi wako umelegezwa; na wito wako ni wa kushawishi, na kuliimarisha kanisa daima. Kwa hivyo wajibu wako ni kwa kanisa milele, na hii ni kwa sababu ya familia yako. Amina.

4 Tazama, ninasema na wewe maneno machache, Samuel; kwani na wewe pia huna hatia yoyote, na wito wako ni wa kushawishi, na kuliimarisha kanisa; na wewe bado hujaitwa kuhubiri mbele za ulimwengu. Amina.

5 Tazama, ninasema kwako maneno machache, Joseph; kwani na wewe pia huna hatia yoyote, na wito wako pia ni wa kushawishi, na kuliimarisha kanisa; na huu ndiyo wajibu wako tangu leo hata milele. Amina.

6 Tazama, ninakufunulia wewe, Joseph Knight, kwa maneno haya, kwamba wewe lazima ujitwike msalaba wako, kwamba ni lazima uombe kwa sauti mbele ya ulimwengu na pia sirini, na katika familia yako, na miongoni mwa marafiki zako, na katika mahali pote.

7 Na, tazama, ni wajibu wako kuungana na kanisa la kweli, na utoe lugha yako kwa kushawishi daima, ili kwamba uweze kupokea ujira wa mfanya kazi. Amina.