Neno lililotumika katika maandishi halisi ya Kiyunani linaanisha “chovya” au “zamisha.” Ubatizo kwa uzamisho katika maji na mtu mwenye mamlaka ni ibada ya kwanza ya injili na ni ya muhimu ili kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hutanguliwa na imani katika Yesu Kristo na katika toba. Ni lazima ufuatiwe na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu ili uweze kuwa kamili (2 Ne. 31:13–14). Ubatizo kwa maji na Roho ni muhimu kabla mtu hajaingia katika ufalme wa selestia. Adamu alikuwa mtu wa kwanza kubatizwa (Musa 6:64–65). Yesu pia alibatizwa ili kutimiza haki yote na ili kuonyesha njia kwa ajili ya wanadamu wote (Mt. 3:13–17; 2 Ne. 31:5–12).
Kwa sababu si watu wote duniani hupata nafasi ya kuipokea injili wakiwa duniani, Bwana ametoa mamlaka ubatizo kufanyika kwa watu walio hai kwa niaba ya wale waliokufa. Kwa hiyo, wale waipokeao injili katika ulimwengu wa roho wanaweza kustahili kuingia katika ufalme wa Mungu.