Misaada ya Kujifunza
Marko


Marko

Katika Agano Jipya, Yohana Marko alikuwa mwanawe Maria, aliyeishi Yerusalemu (Mdo. 12:12); yawezekana pia akawa binamu (au mpwa) wa Barnaba (Kol. 4:10). Alikwenda pamoja na Paulo na Barnaba kutoka Yerusalemu katika safari yao ya kwanza ya kimisionari na akawaacha wao huko Perga (Mdo. 12:25; 13:5, 13). Baadaye aliongozana na Barnaba kwenda Kipro (Mdo. 15:37–39). Alikuwa pamoja na Paulo huko Rumi (Kol. 4:10; Flm. 1:24), na alikuwa pamoja na Petro huko Babiloni (huenda huko Rumi) (1 Pet. 5:13). Mwishoni, alikuwa pamoja na Timotheo huko Efeso (2 Tim. 4:11).

Injili ya Marko

Kitabu cha pili katika Agano Jipya. Injili ya Marko yawezekana kuwa iliandikwa kwa maelekezo ya Petro. Lengo lake ni kumwelezea Bwana kama ndiye Mwana wa Mungu aliye hai na akitenda miongoni mwa watu. Marko anaelezea, kwa nguvu na unyenyekevu, picha ambayo Yesu aliifanya kwa watazamaji. Mapokeo yanaelezea ya kuwa baada ya kifo cha Petro, Marko alitembelea Misri, akaanzisha Kanisa katika Iskanderia, na akafa kifo cha kishahidi.

Kwa orodha ya matukio katika maisha ya Mwokozi kama yaliyoelezwa na Marko, ona Upatanifu wa Injili katika kiambatisho.