Dhabihu
Katika siku za kale, dhabihu ilikuwa na nia ya kufanya kitu fulani au mtu fulani kuwa mtakatifu. Sasa inamaanisha kuacha au kukubali kupotea kwa mambo ya kiulimwengu kwa ajili ya Bwana na ufalme Wake. Waumini wa Kanisa la Bwana yawapasa kuwa tayari kutoa dhabihu vitu vyote kwa ajili ya Bwana. Joseph Smith alifundisha kwamba “dini ambayo hailazimu kutoa dhabihu ya vitu vyote kamwe haina uwezo wa kutosha kuzalisha imani muhimu kwa ajili ya uzima na wokovu.” Katika mtazamo wa milele, baraka zinazopatikana kwa kujitoa dhabihu ni kubwa zaidi kuliko kitu chochote ambacho tumekitoa.
Baada ya Adamu na Hawa kutupwa nje ya Bustani ya Edeni, Bwana aliwapa amri ya dhabihu. Sheria hii ilijumuisha kutoa sadaka mzaliwa wa kwanza wa mifugo yao. Dhabihu hii ilikuwa ni ishara ya dhabihu ambayo ingelifanywa na Mwana Mzaliwa Pekee wa Mungu (Musa 5:4–8). Desturi hii iliendelea hadi kile kifo cha Yesu Kristo, ambacho kilimaliza dhabihu za wanyama kama agizo la injili (Alma 34:13–14). Katika Kanisa siku hizi waumini hushiriki sakramenti ya mkate na maji katika ukumbusho wa dhabihu ya Yesu Kristo. Waumini wa Kanisa la Kristo siku hizi pia wanaombwa kutoa dhabihu ya moyo uliovunjika na roho iliyopondeka (3 Ne. 9:19–22). Hii maana yake ni kwamba watakuwa wanyenyekevu, wenye kutubu, na walio tayari kutii amri za Mungu.