Misaada ya Kujifunza
Samweli, Nabii wa Agano la Kale


Samweli, Nabii wa Agano la Kale

Mwana wa Elkana na Hanna, Samweli alizaliwa kama jibu la sala za mama yake (1 Sam. 1). Akiwa mdogo aliwekwa katika usimamizi wa Eli, kuhani mkuu katika hema huko Shilo (1 Sam. 2:11; 3:1). Bwana alimwita Samweli kuwa nabii katika umri mdogo (1 Sam. 3). Baada ya kifo cha Eli, Samweli akawa ndiye nabii na mwamuzi mkuu wa Israeli na akarejesha sheria, taratibu, na ibada za kawaida kidini katika nchi (1 Sam. 4:15–18; 7:3–17).

1 Samweli 28:5–20 ni historia ya Samweli alivyoamriwa kurudi kutoka kwa wafu na mchawi wa Endori kwa ombi la Mfalme Sauli. Hili lisingeweza kuwa ono kutoka kwa Mungu, kwa sababu mchawi au mtu mwingine yeyote aliye hai anayedai kuwasiliana na roho za wafu hawezi kumfanya nabii ajitokeze kwa ombi lake.

Kitabu cha 1 na 2 Samweli

Katika baadhi ya Biblia, vitabu 1 na 2 Samweli ni kitabu kimoja. Katika nyingine ni vitabu viwili. Vitabu hivi vinachukua kipindi cha takribani miaka 130, tangu kuzaliwa kwa Samweli hadi kabla tu ya kifo cha Daudi.

Kitabu cha 1 Samweli

Mlango 1–3 inaeleza kwamba Bwana aliilaani na kuiadhibu familia ya Eli na akamwita Samweli kuwa kuhani na mwamuzi mkuu. Mlango 4–6 inaelezea namna sanduku la agano lilivyoangukia katika mikono ya Wafilisti. Mlango wa 7–8 inaandikwa maonyo ya Samweli juu ya kuwa na miungu wa uongo na mfalme mwovu. Mlango 9–15 inaelezea kuvikwa kwa taji la ufalme kwa Sauli na utawala wake kama mfalme. Mlango 16–31 ni historia ya Daudi na kujipatia kwake madaraka—Samweli alimpaka mafuta Daudi aliyemwua Goliati. Sauli alimchukia Daudi, lakini Daudi alikataa kumuua Sauli ingawa alipata nafasi ya kufanya hivyo.

Kitabu cha 2 Samweli

Kitabu kina maelezo marefu juu ya utawala wa Daudi kama mfalme wa Yuda na hatimaye wa Israeli yote. Mlango wa 1–4 inaonyesha mapambano marefu kati ya wafuasi wa Daudi baada ya kuvikwa taji la kifalme na Yuda, na wafuasi wa Sauli. Mlango wa 5–10 inamwonyesha Daudi anakuwa mwenye nguvu sana katika nchi nyingi. Mlango wa 11–21 inaonyesha kushuka kwa nguvu za kiroho za Daudi kwa sababu ya dhambi zake na uasi ndani ya familia yake mwenyewe. Mlango wa 22–24 inaelezea jaribio la Daudi la kujipatanisha na Bwana.