Misaada ya Kujifunza
Mathayo


Mathayo

Mtume wa Yesu Kristo na mwandishi wa kitabu cha kwanza katika Agano Jipya. Mathayo ni Myahudi ambaye alikuwa mtoza ushuru kwa ajili ya Warumi huko Kapernaumu, yawezekana alikuwa katika huduma ya Herode Antipasi. Alijulikana kama Lawi kabla ya uongofu wake mwana wa Alfayo (Mk. 2:14). Mara baada ya wito wake wa kuwa mwanafunzi wa Yesu, alitengeneza karamu ambayo Bwana naye alikuwepo (Mt. 9:9–13; Mk. 2:14–17; Lk. 5:27–32). Huenda Mathayo alikuwa na ujuzi mpana wa maandiko ya Agano la Kale na aliweza kuona kwa uwazi utimilifu wa unabii katika maisha ya Bwana. Juu ya maisha ya baadaye ya Mtume huyu yanajulikana kidogo. Pokeo moja linadai kwamba alikufa mauti ya mfiadini.

Injili ya Mathayo

Kitabu cha kwanza katika Agano Jipya. Injili ya Mathayo huenda mwanzoni aliiandika kwa matumizi ya Wayahudi katika Palestina. Inatumia nukuu nyingi kutoka katika Agano la Kale. Lengo kuu la Mathayo lilikuwa kuonyesha kwamba Yesu alikuwa ndiye Masiya ambaye manabii wa Agano la Kale walimzungumzia. Yeye pia alisisitiza kuwa Yesu ni Mfalme na Mwamuzi wa watu.

Kwa orodha ya matukio katika maisha ya Mwokozi kama yalivyoelezwa katika Injili ya Mathayo, ona Upatanifu wa Injili katika kiambatisho.