Kama ilivyotumika katika maandiko, kulipia dhambi ni kuadhibiwa kwa ajili ya tendo la dhambi, kwa njia hiyo unaondoa athari ya dhambi kutoka kwa mtenda dhambi na kumruhusu apate kupatanishwa na Mungu. Yesu Kristo alikuwa mtu pekee mwenye uwezo wa kufanya upatanisho mkamilifu kwa ajili ya wanadamu wote. Aliweza kufanya hivyo kwa sababu ya kuchaguliwa Kwake na kuteuliwa kabla katika Baraza Kuu kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu (Eth. 3:14; Musa 4:1–2; Ibr. 3:27), uungu Mwana Wake, na maisha Yake yasiyo na dhambi. Upatanisho Wake ulijumuisha kuteseka Kwake kwa ajili ya dhambi za wanadamu, katika, kumwagika kwa damu Yake, na kifo Chake na hatimaye ufufuko kutoka kaburini (Isa. 53:3–12; Lk. 22:44; Mos. 3:5–11; Alma 7:10–13; M&M 19:16–19). Kwa sababu ya Upatanisho, watu wote watafufuka kutoka wafu wakiwa na miili isiyokufa (1 Kor. 15:22). Upatanisho pia umeleta njia ambayo kwayo sisi tunaweza kusamehewa dhambi zetu na kuishi pamoja na Mungu milele. Lakini mtu aliyefikia umri wa uwajibikaji na kupokea sheria anaweza kupata baraka hizi endapo tu atakuwa na imani katika Yesu Kristo, akatubu dhambi zake, na kupokea ibada za wokovu, na kutii amri za Mungu. Wale ambao hawafikii umri wa uwajibikaji na wale wasio na sheria wamekombolewa kwa njia ya Upatanisho (Mos. 15:24–25; Moro. 8:22). Maandiko kwa uwazi kabisa yanatufundisha kama Kristo asingelipa kwa ajili ya dhambi zetu, hakuna sheria, ibada, au dhabihu ambayo ingeridhisha matakwa ya haki, na mwanadamu kamwe asingeweza kufika tena katika uwepo wa Mungu (2 Ne. 2; 9).