Misaada ya Kujifunza
Petro


Petro

Katika Agano Jipya, Petro mwanzoni alijulikana kama Simeoni au Simoni (2 Pet. 1:1), mvuvi wa Bethsaida aliyekuwa akiishi Kapernaumu pamoja na mke wake. Yesu alimponya mama wa mke wake (Mk. 1:29–31). Petro aliitwa yeye pamoja na kaka yake Andrea kuwa mfuasi wa Yesu Kristo (Mt. 4:18–22; Mk. 1:16–18; Lk. 5:1–11). Jina lake la Kiaramaya, Kefa, maana yake “mwonaji” au “jiwe” alipewa na Bwana (Yn. 1:40–42; TJS, Yn. 1:42 [Kiambatisho]). Wakati Agano Jipya linataja baadhi ya mapungufu ya Petro katika mwili wenye kufa, pia linatuonyesha kwamba aliyashinda na akaimarishwa kwa imani yake katika Yesu Kristo.

Petro alikiri kwamba Yesu alikuwa ndiye Kristo na Mwana wa Mungu (Yn. 6:68–69), na Bwana alimteua yeye kushikilia funguo za ufalme duniani (Mt. 16:13–19). Juu ya Mlima wa Kugeuka Sura, Petro alimwona Mwokozi aliyegeuka sura, vile vile Musa na Elia (Eliya) (Mt. 17:1–9).

Petro alikuwa ndiye Mtume kiongozi katika siku zake. Baada ya kifo, Ufufuko, na Kupaa kwa Mwokozi, yeye aliliita Kanisa pamoja na akaongoza katika kuitwa kwa Mtume wa kujaza nafasi ya Yuda Iskarioti (Mdo. 1:15–26). Petro na Yohana walimponya mtu aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa (Mdo. 3:1–16) na kimuujiza aliachiliwa huru kutoka gerezani (Mdo. 5:11–29; 12:1–19). Ilikuwa kupitia kwa huduma ya Petro kwamba injili kwa mara ya kwanza ilipelekwa kwa Wayunani (Mdo. 10–11). Katika siku za mwisho, Petro, pamoja na Yakobo na Yohana, walikuja kutoka mbinguni na kutunuku Ukuhani wa Melkizedeki na funguo zake juu ya Joseph Smith na Oliver Cowdery (M&M 27:12–13; 128:20).

Waraka wa Kwanza wa Petro

Waraka wa kwanza uliandikwa kutoka “Babilonia” (huenda ikawa Roma) na ukatumwa kwa Watakatifu katika ile ambayo sasa inaitwa Asia Ndogo mara baada ya Nero kuanza kuwatesa Wakristo.

Mlango wa 1 unazungumzia juu ya nafasi ya Kristo kuteuliwa kabla kuwa Mkombozi. Mlango wa 2–3 inaelezea kwamba Kristo ndiye jiwe kuu la pembeni la Kanisa, kwamba Watakatifu wanaushikilia ukuhani wa Kifalme, na kwamba Kristo alizihubiria roho zilizokuwa gerezani. Mlango wa 4–5 inaelezea ni kwani injili inahubiriwa kwa wafu na ni kwa nini wazee lazima walilishe kundi.

Waraka wa pili wa Petro

Mlango wa 1 unawahimiza Watakatifu kufanya imara miito yao na uteule wao. Mlango wa 2 unaonya dhidi ya walimu wa uongo. Mlango wa 3 unaeleza juu ya siku za mwisho na Ujio wa Pili wa Kristo.