Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 44


Sehemu ya 44

Ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith Nabii na Sidney Rigdon, huko Kirtland, Ohio, mwishoni mwa Februari 1831. Katika kutimiza masharti yaliyowekwa humu, Kanisa lilipanga mkutano ufanyike mapema katika mwezi wa Juni iliyofuata.

1–3, Wazee wakusanyike katika mkutano; 4–6, Wanapaswa kulianzisha kulingana na sheria za nchi na kuwajali maskini.

1 Tazama, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu ninyi watumishi wangu, ni muhimu kwangu kuwa wazee wa kanisa langu yawapasa waitwe pamoja, kutoka mashariki na kutoka magharibi, na kutoka kaskazini na kutoka kusini, kwa barua au njia nyinginezo.

2 Na itakuwa kwamba kadiri watakavyokuwa waaminifu, na kutenda imani kwangu, nitaimwaga Roho yangu juu yao katika siku ile watakayokutana pamoja.

3 Na itakuwa kwamba watakwenda kwenye maeneo yaliyowazunguka, na kuhubiri toba kwa watu.

4 Na wengi wataongolewa, kiasi kwamba mtapata nguvu ya kujisimamia wenyewe kulingana na sheria za mwanadamu;

5 Ili kwamba maadui zenu wasiweze kuwa na nguvu juu yenu; ili muweze kulindwa katika mambo yote; ili muwezeshwe kushika sheria zangu; kwamba kila mnyororo uweze kuvunjwa ambao kwa huo adui ataka kuwaangamiza watu wangu.

6 Tazama, ninawaambia, kwamba inawalazimu kuwatembelea wagonjwa na wenye shida na kuwapatia msaada, ili waweze kutunzwa hadi mambo yote yaweze kufanywa kulingana na sheria yangu ambayo mmeipokea. Amina.