Sehemu ya 51
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii huko Thompson, Ohio, 20Â Mei 1831. Kwa wakati huu watakatifu wanaohamia kutoka mashariki walianza kufikia Ohio, na ilikuja kuwa muhimu kufanya mipango ya makazi yao. Na kazi hii ilikuwa wajibu wa ofisi ya askofu, Askofu Edward Partridge aliomba mwongozo juu ya jambo hili, na hivyo Nabii alimwomba Bwana.
1–8, Edward Partridge ameteuliwa kudhibiti usimamizi na mali; 9–12, Watakatifu lazima wafanyiane haki na kupokea sawa sawa; 13–15, Ni lazima wawe na ghala ya askofu na kupanga mali kulingana na sheria ya Bwana; 16–20, Ohio patakuwa mahali pa kukusanyika kwa muda.
1 Nisikilizeni Mimi, asema Bwana Mungu wenu, na nitasema naye mtumishi wangu Edward Partridge, na kumpa yeye maelekezo; kwani ni muhimu kwamba apokee maelekezo namna ya kuwasimamia watu hawa.
2 Kwani ni muhimu kwamba wasimamiwe kulingana na sheria zangu; vinginevyo, watakatiliwa mbali.
3 Kwa hivyo, mtumishi wangu Edward Partridge, na wale aliowateua, ambao ninapendezwa nao, wawagawie watu hawa sehemu zao, kila mtu sawa kulingana na familia yake, na kulingana na hali yake na matakwa na shida zake.
4 Na mtumishi wangu Edward Partridge, wakati atakapomgawia mtu sehemu yake, na ampe hati ambayo itahakikisha kuwa ni sehemu yake, kwamba ataishikilia hati hiyo na urithi huu katika kanisa, hadi avunje sheria na kutohesabiwa kustahili kwa sauti ya kanisa, kulingana na sheria na maagano ya kanisa, juu ya ustahiki kanisani.
5 Na kama atavunja sheria na hahesabiwi kuwa mwenye kustahili kuwa katika kanisa, hatakuwa na uwezo wa kudai ile sehemu ambayo aliyoiweka wakfu kwa askofu kwa ajili ya maskini na wenye shida wa kanisa langu; kwa hiyo, hatarejeshewa zawadi hiyo, bali atakuwa na madai tu ya sehemu ile aliyogawiwa yeye.
6 Na hivyo ndivyo mambo yote yatakavyolindwa, kulingana na sheria za nchi.
7 Na hivyo kile kilicho cha watu hawa kigawanywe kwa watu hawa.
8 Na fedha zilizosalia kwa watu hawa—na pateuliwe wakala kwa watu hawa, na kuchukua fedha hizo kwa ajili ya kuleta vyakula na mavazi, kulingana na mahitaji ya watu hawa.
9 Na kila mtu na afanye haki, na kuwa sawa miongoni mwa watu hawa, na kupokea sawa, ili kwamba muweze kuwa na umoja, kama vile nilivyowaamuru.
10 Na kile kilicho cha watu hawa kisichukuliwe na kutolewa kwa wale wa kanisa jingine.
11 Kwa hiyo, kama kanisa jingine watapokea fedha za kanisa hili, na walipe kwa kanisa hili tena kulingana na makubaliano yao;
12 Na hii itafanyika kupitia kwa askofu au wakala, ambaye atateuliwa kwa sauti ya kanisa.
13 Na tena, na askofu ataanzisha ghala kwa kanisa hili; na mambo yote ya fedha na katika vyakula, ambayo ni zaidi ya mahitaji kwa watu hawa, vitunzwe katika mikono ya askofu.
14 Na yeye pia ajiwekee kwa mahitaji yake yeye mwenyewe, na kwa mahitaji ya familia yake, tangu atakapoajiriwa katika kufanya shughuli hii.
15 Na hivyo ndivyo ninavyowapa watu hawa nafasi ya kujisimamia wenyewe kulingana na sheria zangu.
16 Nami ninaiweka wakfu nchi hii kwa ajili yao kwa majira mafupi, hadi Mimi, Bwana, nitakapopanga vinginevyo, na kuwaamuru kwenda kutoka hapa;
17 Na saa wala siku haijatolewa kwao, kwa hiyo wafanye katika nchi hii kana kwamba wapo kwa miaka mingi, na hii itageuka kuwa vyema kwao.
18 Tazama, huu utakuwa ni mfano kwa mtumishi wangu Edward Partridge, katika mahali pengine, katika makanisa yote.
19 Na yeyote atakayepatikana kuwa mwaminifu, mwenye haki, na mtumishi mwenye hekima ataingia katika shangwe ya Bwana wake, na ataurithi uzima wa milele.
20 Amini, ninawaambia, Mimi ndimi Yesu Kristo, naja upesi, katika saa msiyodhani. Hivyo ndivyo. Amina.