Sehemu ya 65
Ufunuo juu ya sala uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Hiram, Ohio, 30Â Oktoba 1831.
1–2, Funguo za ufalme wa Mungu zakabidhiwa kwa mwanadamu duniani, na kazi ya injili itashinda; 3–6, Ufalme wa mbinguni wa milenia utakuja na kuungana na ufalme wa Mungu wa duniani.
1 Sikilizeni, na lo, sauti ya mtu kama aliyetumwa kutoka juu, mwenye uwezo na mwenye nguvu, ambaye kutoka kwake ni hata mwisho wa dunia, ndiyo, ambaye sauti yake yaenda kwa wanadamu—Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.
2 Funguo za ufalme wa Mungu zakabidhiwa kwa mwanadamu duniani, na kutoka huko injili itaenea hata miisho ya dunia, kama vile jiwe lililochongwa mlimani bila kazi ya mikono litabiringika, hadi litaijaza dunia yote.
3 Ndiyo, sauti iliayo—Itengenezeni njia ya Bwana, andaeni karamu ya Mwanakondoo, kuweni tayari kwa ajili ya Bwana Harusi.
4 Ombeni kwa Bwana, mlilingane jina lake takatifu, wajulisheni watu matendo yake ya ajabu.
5 Mlinganeni Bwana, ili ufalme wake uweze kuenea juu ya dunia, ili wakazi wake waweze kuupokea, na kujitayarisha kwa ajili ya siku zijazo, siku ambazo Mwana wa Mtu atashuka kutoka mbinguni, aliyevikwa katika mngʼaro wa utukufu wake, kukutana na ufalme wa Mungu ambao umewekwa duniani.
6 Kwa hiyo, na ufalme wa Mungu uenee, ili ufalme wa mbinguni uweze kuja, ili wewe, Ee Mungu uweze kutukuzwa mbinguni hata na duniani, ili adui zako waweze kushindwa; kwa kuwa ukuu ni wako, uwezo na utukufu, milele na milele. Amina.