Maandiko Matakatifu
Mafundisho na Maagano 72


Sehemu ya 72

Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio 4 Desemba 1832. Wazee kadhaa na waumini wengine walikuwa wamekusanyika ili kujifunza wajibu wao, na ili kuinuliwa zaidi katika mafundisho ya Kanisa. Sehemu hii ni mkusanyiko wa mafunuo matatu yaliyopokelewa siku moja. Aya ya 1 mpaka ya 8 zinajulisha juu ya wito wa Newel K. Whitney kama askofu. Ndipo aliitwa na kutawazwa, baadaye aya ya 9 hadi ya 23 zilipokelewa, zikitoa habari za nyongeza juu ya kazi ya askofu. Baadae aya 24 hadi 26 zilitolewa zikitoa maelekezo kuhusu kukusanyika Sayuni.

1–8, Wazee watatoa taarifa ya usimamizi wao kwa askofu; 9–15, Askofu atatunza ghala na kutunza maskini na wenye shida; 16–26, Maaskofu watathibitisha ustahilifu wa wazee.

1 Sikilizeni, na mkasikie sauti ya Bwana, Enyi wote mliojikusanya pamoja, mlio makuhani wakuu wa kanisa langu, ambao ufalme na uwezo vimetolewa.

2 Kwani amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana, ni muhimu kwangu kwa askofu kuteuliwa kwenu, au kutoka kwenu, kwa ajili ya kanisa katika sehemu hii ya shamba la mizabibu la Bwana.

3 Na amini katika jambo hili mmefanya kwa busara, kwani yatakiwa na Bwana, kwa mkono wa kila msimamizi, kutoa hesabu ya usimamizi wake, katika wakati huu na milele.

4 Kwani yule aliye mwaminifu na mwenye busara anahesabiwa kuwa mwenye kustahili kurithi makao yaliyoandaliwa na Baba yangu kwa ajili yake.

5 Amini ninawaambia, wazee wa kanisa katika sehemu hii ya shamba langu la mizabibu watatoa hesabu ya usimamizi wao kwa askofu, ambaye nimemteua katika sehemu hii ya shamba langu la mizabibu.

6 Mambo haya yatatunzwa katika kumbukumbu, ili yakabidhiwe kwa askofu katika Sayuni.

7 Na kazi ya askofu itajulikana kwa amri zilizotolewa, na kwa sauti ya mkutano.

8 Na sasa, amini ninawaambia, mtumishi wangu Newel K. Whitney ndiye mtu atakayeteuliwa na kutawazwa katika uwezo huu. Haya ndiyo mapenzi ya Bwana Mungu wenu, na Mkombozi wenu. Hivyo ndivyo. Amina.

9 Neno la Bwana, ambalo ni nyongeza ya sheria zilizotolewa, zikijulisha kazi ya askofu ambaye amekwisha tawazwa kwa kanisa katika sehemu hii ya shamba la mizabibu, ambalo amini hili ndilo—

10 Kuitunza ghala ya Bwana; kupokea fedha za kanisa katika sehemu hii ya shamba la mizabibu;

11 Kupokea taarifa ya wazee kama ilivyoamriwa hapo awali; na kushughulikia mahitaji yao, wale watakaolipa kwa ajili ya yale wanayopokea, ilimradi wanao uwezo wa kulipa;

12 Ili hii pia iweze kuwekwa wakfu kwa manufaa ya kanisa, kwa maskini na wenye shida.

13 Na kwa yule asiye na uwezo wa kulipa, hesabu yake itachukuliwa na kukabidhiwa kwa askofu wa Sayuni, ambaye atalipa deni kutokana na kile Bwana atakachokiweka mikononi mwake;

14 Na kazi za uaminifu za wafanya kazi katika mambo ya kiroho, katika kusimamia injili na mambo ya ufalme kwa kanisa, na kwa ulimwengu, zitakubaliwa kulipa deni kwa askofu katika Sayuni;

15 Hivyo malipo yatatoka kanisani, kwa kuwa kulingana na sheria kila mtu ambaye huja Sayuni ni lazima aweke vitu vyote mbele ya askofu katika Sayuni.

16 Na sasa, amini ninawaambia, kwamba kwa vile kila mzee katika sehemu hii ya shamba la mizabibu lazima atoe taarifa ya usimamizi wake kwa askofu katika sehemu hii ya shamba la mizabibu—

17 Hati kutoka kwa jaji au askofu katika sehemu hii ya shamba la mizabibu, kwenda kwa askofu katika Sayuni, humfanya kila mtu aweze kukubaliwa, na hujibu mambo yote, kwa ajili ya urithi, na kupokelewa kama msimamizi mwenye busara na mfanyakazi mwaminifu;

18 Vinginevyo hatakubaliwa na askofu wa Sayuni.

19 Na sasa, amini ninawaambia, na kila mzee ambaye atatoa taarifa kwa askofu wa kanisa katika sehemu hii ya shamba la mizabibu athibitishwe na kanisa au makanisa, ambako hutenda kazi, ili aweze kuonyesha mwenyewe na taarifa yake wamethibitishwa katika mambo yote.

20 Na tena, acha watumishi wangu ambao wameteuliwa kuwa kama wasimamizi juu ya mambo yahusuyo maandishi ya kanisa langu wanayo madai kwa ajili ya msaada kutoka kwa askofu au maaskofu katika mambo yote—

21 Ili mafunuo yaweze kuchapishwa, na kuenea hata miisho ya dunia; kwamba nao pia waweze kupata fedha ambazo zitalinufaisha kanisa katika mambo yote;

22 Ili nao pia waweze kuonyesha kuwa wamethibitishwa katika mambo yote, na wahesabiwe kama wasimamizi wenye busara.

23 Na sasa, tazama, huu utakuwa utaratibu kwa matawi yote makubwa ya kanisa, katika nchi yoyote yatakakoanzishwa. Na sasa ninafanya mwisho wa maneno yangu. Amina.

24 Maneno machache ya nyongeza katika sheria ya ufalme, kuhusu waumini wa kanisa—wale ambao wameteuliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwenda Sayuni, na ambao wamepata nafasi ya kwenda Sayuni—

25 Na wapeleke hati ya uthibitisho kwa askofu kutoka kwa wazee watatu wa kanisa, au hati ya uthibitisho kutoka kwa askofu;

26 Vinginevyo yule atakayekwenda nchi ya Sayuni hatahesabiwa kama msimamizi mwenye busara. Huu pia ni mfano. Amina.