“Sasa Nilikubali Changamoto”
Mnano Mei 2005, Stacy Wambui Mugo alikuwa amekuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Eldoret kwa wiki mbili wakati alipoitwa kuwa katibu kwenye Muungano wa Usaidizi. “Hii iliniogopesha sana,” anakumbuka. “Sijui chochote, bado mimi ni mgeni, Bwana anategemea nifanye nini? Hivyo niliondoka Eldoret na kwenda Bungoma.” Huko, umbali wa kilomita 100 (maili 62), Stacy alijaribu kuweka mambo sawa na kuendelea na maisha. “Nilikaa huko takribani miezi sita. Vitu havikwenda sawa,” alisema. “Nilifikiri, labda kwa sababu nilikimbia toka Eldoret na nilikimbia wito niliokuwa nimepewa, ndio maana matatizo yote haya yalikuwa yakija. Hivyo niliamua kurudi.”
Stacy alikwenda kwa binamu yake, aliyemtambulisha Kanisani na akamuomba msaada. Binamu yake alimuonyesha Kitabu cha Maelekezo cha Kanisa na kumwambia ampigie simu ikiwa atakuwa na maswali. Stacy alitumikia kwenye wito wake kama katibu kwenye Muungano wa Usaidizi. Wakati hatimaye alipopumzishwa toka wito huo, alifikiri majukumu yake Kanisani yalikuwa yamekwisha.
Kisha aliitwa kama Rais wa Wasichana. “Kisha nilisema, ‘Jamani, rais, sasa nitafanya nini tena?’ Lakini kwa sababu sasa nilikuwa na uelewa, niliweza kupata nyenzo kutoka Kitabu cha Maelekezo cha Kanisa,” alisema, na “nilijaribu kujifunza zaidi kuhusu nini Rais wa Wasichana anatakiwa kufanya.”
Mnamo 2011, Stacy na mume wake, ambaye walioana mnamo 2010 walihamia sehemu nyingine pamoja na watoto wao nane. Kumbukumbu zao za uumini zilipelekwa kwenye kata nyingine. Alitumaini angepata mapumziko kutoka kutumikia. Lakini aliitwa kwenye Urais wa Darasa la Watoto. Baadaye, aliitwa kuwa Rais wa Darasa la Watoto kwenye wilaya ya Eldoret.
Stacy alifanya kazi kwa bidii kuwafundisha viongozi wa Madarasa ya Watoto kwenye matawi manne ya wilaya, Eldoret, Langas, Huruma na Sosiani.
Kisha aliitwa kuwa rais wa Muungano wa Usaidizi wa wilaya. “Sasa Bwana anatarajia nijifunze kitu kutoka hapo,” anakumbuka akitafakari hilo. “Sasa nilikubali changamoto.”
Stacy si tu alipokea msaada kutoka kwa wanawake wengine ambao walikubali miito kama washauri wake na katibu; mume wake na watoto pia walimsaidia. Mume wake alimsaidia kufika alipohitajika kutembelea, na watoto wake vijana walifua nguo na kupika.
Wakati alipoitwa kama rais wa Muungano wa Usaidizi wilayani, Stacy na mumewe walikuwa na mkutano na watoto wao. “Sasa nimepewa wito huu,” Stacy alisema, “ kila mtu tunapaswa kusaidiana. Ninahitaji sana msaada wenu, kwa sababu muda mwingi nitakuwa ninatoka kwenda kwenye mafunzo. Nitapigiwa simu kila mara tuna matatizo haya.”
Stacy ambaye alikuwa na biashara ya duka lake mwenyewe kwa miaka mingi, aliwaleta viongozi wengine wa Muungano wa Usaidizi pamoja kujadili matatizo ambayo akina dada walikuwa wanakabiliana nayo, ikijumuisha kukimu mahitaji ya familia zao. Alianzisha mafunzo ya jinsi ya kutengeneza sabuni au kupika sambusa kwa ajili ya kuuza na pia jinsi ya kutumia rasilimali kwa busara. Wakati Stacy akijifunza namna ya kujitolea muda wake na vipaji, Bwana alimfanya kuwa baraka kwenye maisha ya wengine.