Historia ya Kanisa
Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda


“Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda,” Historia za Ulimwengu: Rwanda (2020)

“Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda,” Historia za Ulimwengu: Rwanda

Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda

Mnamo mwaka 2002 Nelson na Sapna Samuel walihama kutoka Bangalore, India, hadi Kigali, Rwanda. Ingawa kulikuwa na washiriki wachache wa rekodi wanaoishi Rwanda katika miaka ya 1980 na 1990, akina Samuel hawakupata mtu mwingine yeyote wa kuabudu naye walipofika mara ya kwanza. Walifanya mikutano yao wenyewe kwa miaka kadhaa kabla ya Watakatifu wengine wa Siku za Mwisho kuja Rwanda.

Mnamo mwaka 2007 Nelson na Sapna walitoa nyumba yao iwe mahali pa kukusanyikia kwa ajili ya kikundi kidogo lakini kilichokuwa kinakua cha Watakatifu huko Kigali. Mwanzoni, mikutano ilikuwa midogo kiasi kwamba mtu anayebariki sakramenti angeweza kutaja kimya kimya jina la kila mtu ambaye angeshiriki wakati alipokuwa akiumega mkate. Tukimhesabu mtoto mchanga wa akina Samuel, kulikuwa na washiriki 10 katika kikundi hicho kidogo. Jean Pierre Ndikumana, Mtakatifu wa Siku za Mwisho wa Kikongo anayefanya kazi kama daktari huko Butare, alisafiri kwa basi kwa masaa manne hadi manane kila wiki kwenda kwenye ibada. Muumini mwingine wa Kikongo anayeitwa Justin pia alihudhuria. Eric na Kathy Hyde, wanandoa wa Kimarekani, walikuwa na binti na mwana ambao walikuwa vijana pekee wa Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kundi. Na Fabien Hatangimbabazi, ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa alipokuwa akizuru Marekani na ambaye alikuwa Mnyarwanda wa kwanza wa kundi hilo, alihudumu katika mahakama kuu ya nchi hiyo.

Ingawa kusitishwa kwa usajili wa makanisa mapya nchini Rwanda kulisimama katika njia ya kuzindua kazi rasmi ya umisionari au kupata nyumba ya mikutano, Watakatifu walitamani kuona tawi likiundwa. Na walipoendelea kukutana, Bwana aliwakusanya Watakatifu wengine wa asili ya Rwanda kutoka sehemu mbalimbali za dunia hadi Kigali. Yvonne Martin, ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa huko Scotland, alifika Novemba 2007 na kuanza kushiriki injili na rafiki zake. Jean Marie na Agathe Rumanyika, ambao walikuwa wamekutana na wamisionari huko Missouri kabla ya shughuli za kibiashara kuwarudisha Kigali, walikuja kwa wakati na kutoa nyumba yao, na baadaye, hoteli yao ili kuandaa mikutano wakati kikundi hicho kilipokuwa kikubwa kuliko nafasi katika nyumba ya akina Samuel. Ruth Opar, mmisionari aliyerejea na rais wa zamani wa Muungano wa Usaidizi ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa nchini Kenya, alirudi kuona kama Kigali pangekuwa mahali pazuri pa kuishi na familia yake. Tawi la Kigali lilianzishwa mnamo Machi 16, 2008. Baadaye mwezi huo Joshua Opar—mume wa Ruth na askofu wa zamani—alihamia kwenye tawi pamoja na watoto wao.

Agosti hiyo waumini wa tawi walisafiri kwenda Ziwa Muhazi, takriban saa moja nje ya Kigali, ili kufanya ubatizo wa kwanza nchini humo. Rafiki wa Yvonne Martin aitwaye Damascene Ruhinyura na Mercy Opar, binti wa Ruth na Joshua, wakawa watu wa kwanza kubatizwa nchini humo.

Kwa muda wa miaka miwili iliyofuata, tawi dogo lilipambana na hitaji kubwa la kufundisha na kubatiza. Muda si mrefu walikuwa wakibatiza waongofu 10 wapya kila mwezi. Miongoni mwa waliobatizwa walikuwa John Hakizimana, Eric Habiyaremye, Dady Paul Hakizimana, Vincent Munanira, na wengine ambao kila mmoja alikuwa amepoteza familia zao katika ghasia za kikabila za mwanzoni mwa miaka ya 1990 na walikuwa wameishi mitaani au katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima kwa zaidi ya muongo mmoja. Vijana hawa waliunda msingi wa akidi ya kwanza ya Ukuhani wa Haruni katika Tawi la Kigali. “Vijana hawa walipojifunza kuwatumikia kaka na dada zao,” Rais wa Tawi Eric Hyde alisema, “waligundua kwamba walikuwa sehemu ya familia iliyowapenda, na walikuwa na pa kufikia.”

Chapisha