Ujumbe wa Matumaini kwa Wale Ambao Wamefungwa Jela
Nuru ya Mungu inaweza kuwa sehemu ya siku zako za baadae.
Miaka mingi iliyopita, nilikuwa natembelea gereza moja nilikutana na mtu aliyeitwa Eric. Alikuwa amefungwa jela kwa miaka 17. Katika wakati huu, Eric mara chache sana alikosa kwenda kanisani. Aliomba mara kwa mara na wenzake na aliwasaidia watu wengi kujifunza kuhusu maandiko. Nilipokutana na Eric, alikuwa akiteseka kutokana na changamoto kali za kiafya. Niliweza kuongea naye katika chumba chake cha hospitali pale gerezani.
Tulipokuwa tukiongea, Eric aliniambia jinsi gani alikuwa mwenye shukrani kwa waumini wengi waliokuwa wamemsaidia kwa miaka mingi. Alishiriki ushuhuda na imani yake katika Yesu Kristo. Kisha, katika sauti ya kunong’ona alisema bado palikuwa na siku nyingi ambapo alijisikia kusahaulika na mpweke. Tuliongea kwa muda mrefu, tukasali pamoja, na tukaachana kama marafiki. Saa chache baadae, nilijua kwamba Eric ameaga dunia.
Safari ya Eric maishani ilikuwa ngumu. Lakini hatimaye alikuja kumjua na kumpenda Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo, na yeye mwenyewe. Na kwamba hili ndilo muhimu. Katika umilele, sifikiri kama itakuwa muhimu wapi au jinsi gani tulikuja kumjua Yesu. Kile kitakachokuwa muhimu ni kile kila mmoja wetu alichokifanya na maisha yetu baada ya kumpata Yeye.
Hali na chaguzi ambazo zimekufikisha kufungwa kwako jela hazipaswi kueleza sifa bainifu za maisha yako Unaweza kuwa umefanya makosa, makubwa na madogo. Unaweza kuwa umetenda kosa la jinai mara moja au mara nyingi. Hii ni sehemu ya yaliyopita kwako, lakini yaliyopita hayaamui ubaadae wako. Unayo nguvu ya kufanya chaguzi ambazo zitaalika furaha, hata katika wakati mgumu.
Utambulisho Wako wa Kweli
Dada Joy D. Jones, Rais Mkuu wa Msingi, ametembelea gereza mara nyingi. Wakati fulani alinisimulia hadithi hii.
“Ninakumbuka mara ya kwanza nilipotembelea gereza jirani na ninapoishi. Nilipoongea na kikundi cha wafungwa, nilihisi kama nilikuwa katika nafasi takatifu kwa sababu nilijua kwa dhati walitaka kubadilika na kuja kwa Kristo. Tulizungumzia kuhusu utambulisho wetu wa kiungu kama watoto wa Mungu.
“Wakati mmoja, niliwaambia kuhusu mjukuu wangu wa kike wa miaka miwili aliyekuja kwangu siku moja, akitabasamu. Kwa shauku kubwa akatangaza, ‘Bibi, mimi ni mtoto wa Mungu!’ Kisha mtu mmoja kimya kimya akasema, ‘nashangaa maisha yangu yangekuwaje leo kama mtu angeniambia wakati nilipokuwa mdogo kwamba nilikuwa mtoto wa Mungu.’
“Habari njema ni kwamba sisi sote ni watoto wa Mungu,” Dada Jones aliendelea, “iwe tumejifunza tukiwa watoto au baadae katika maisha. Kwamba kamwe hujachelewa. Huja sahaulika. Mungu anakujua. Yeye anakupenda. Mwanawe, Yesu Kristo, ni Mwokozi wetu. Alilipia adhabu ya dhambi za kila mmoja wetu. Kwa sababu ya hilo, Yesu anaelewa maisha yetu kiukamilifu, na tunaweza kusamehewa kabisa dhambi zetu. Yeye alisema, ‘Ndio, wanaweza kusahau, lakini sitakusahau. … Tazama, nimekuchora viganjani mwa mikono yangu; kuta zako daima ziko mbele yangu’ (1 Nefi 21:15–16).”
Kuamini kwamba wewe, na kila unayemjua, kuwa ni mtoto wa Mungu inaweza kuwa chanzo cha nguvu ya ndani. Unapoukubali ukweli huu na kuacha uyaongoze maisha yako, utapata amani kuu zaidi na kuwa mfano mwema kwa wengine.
Kujenga Upya Imani.
Kokote katika maisha inaweza kuwa vigumu kujua jinsi ya kuamini, lakini unaweza daima ukamwamini Baba yako wa Mbinguni. Maandiko yanatufundisha kwamba Mungu anakujua wewe kiukamilifu. Yeye anakupenda na hawezi kudanganya.1 Kama kuwaamini wengine—ikijumuisha na Mungu—ni vigumu kwako, omba kwa ajili ya hilo. Muulize Baba yako wa Mbinguni, “Je, Unanipenda? Je, Ninaweza Kukuamini?” Kisha sikiliza jibu. Linaweza kuja kama hisia za amani au wazo tulivu. Linaweza likachukua muda. Lakini Mungu ata jibu maombi yako.
Kama nyongeza kwa kujua ambaye unaweza kumuamini, ni muhimu kuwa mtu ambaye unaweza kuaminika. Inaweza isiwe sawa kwako kuwa na mawasiliano na wale ambao umewadhuru. Lakini bado unaweza kuangalia matukio yaliyopita kwa uzoefu wa mtazamo wao, kujenga huruma juu yao, na kusali kuhusu wao. Unaweza kuchagua kuwa mtu wa kuaminiwa katika mahusiano mapya unayoanzisha
Ninaweza kuwa barabara ndefu. Ninashukuru kwa utiaji moyo huu kutoka kwa Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Endelea kupenda. Endelea kujaribu. Endelea na uaminifu. Endelea kuamini. Endelea kukua. Mbingu zinakushangilia leo, kesho, na milele.”2
Kulea Wakati Umefungwa Jela
Unaweza ukashawishika kufikiria kuwa huwezi kuwa mzazi wakati wa majira yako ya kufungwa jela. Pinga kufikiri huku. Wakati wo wote inapowezekana, tafuta njia za kuisaidia familia na watoto wako.
Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Kanisa wamehimiza jinsi ilivyo muhimu kufundishana injili katika familia zetu. Jiulize mwenyewe, “Je, ninawezaje kuisaidia familia yangu kupokea baraka za injili?” Hapa kuna mawazo manne:
-
Unaweza daima kuomba kwa ajili ya familia yako. Maombi ni aina ya kazi yenye nguvu kiroho ambayo haizuiliwi na kuta au umbali.
-
Kama unaruhusiwa kuwasiliana na watoto wako, tafuta njia sahihi ya kuelezea upendo wako. Wafundishe kuhusu masomo ya kiroho unayojifunza.
-
Fanya juhudi ya kujiunganisha na marafiki wa kuaminika. Jenga uhusiano na wale ambao wangekuwa na ushawishi mzuri kwa familia yako.
-
Badilika kwa ajili ya mema. Kila jitihada unayofanya ili kujiboresha mwenyewe na kuwajibika kwa chaguzi zako zitakusaidia kuwa baba au mama bora.
Kusonga Mbele
Nabii wetu leo, Rais Russell M. Nelson, alisema kwamba lengo la maisha haya ni kujitayarisha kuonana na Mungu kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo. “Na tunafanya hivyo pale tunapotubu kila siku na kupokea utakaso Wake, uponyaji, na nguvu za kuimarisha,” alifundisha. “Ndipo tunaweza kujisikia amani na shangwe endelevu, hata katika nyakati za dhoruba.”3
Toba ni sehemu muhimu ya uponyaji. Inaanza unaposali kwa dhati kwa Mungu, ukimwambia kile ulichofanya vibaya na kuomba msamaha Wake. Utaanza kujisikia mwenye amani unapojifunza zaidi kuhusu injili na kufuata mfano wa Yesu Kristo. Hisia hizi, na mabadiliko ya tabia yako, ni ushahidi kwamba unaanza kupona.
Viongozi wa Kanisa wako hapo ili kukusaidia kutembea njia hii ya kurudi kwa Mungu. Kupitia kwa Yesu Kristo, daima itakuwa inawezekana kurudi kwa Baba yako wa Mbinguni. Ingawa waweza kujisikia umesamehewa na Mungu mapema kabla ya kusamehewa na familia, jumuiya, au hata waumini wa Kanisa, usivunjike moyo. Endelea kusonga mbele. Amini katika ahadi za Mungu na ratiba Yake.
Mungu Atakusaidia Upone
Kumbuka kwamba kila aina ya uponyaji—ikijumuisha kutokana na kutawaliwa na mazoea mabaya, unyanyasaji, au kiwewe kingine—unachukua muda. Biblia inatuambia hadithi ya Yesu kumponya mtu mwenye ulemavu wa kuona ambaye uoni wake ulirudi kwa hatua. Kwanza aliwaona “watu kama miti, inayojongea.” Ndipo Yesu “akaweka tena mikono yake juu ya macho yake,” na kwamba mtu yule mwishowe akaweza kuona kila kitu wazi wazi (Marko 8:24–25). Vivyo hivyo, wakati Yesu alipomponya mwanamke ambaye alikuwa akitokwa na damu, ilikuwa baada ya kuteseka kwa tatizo hilo la kiafya kwa miaka 12 (ona Marko 5:25–34). Hadithi hizi zinatukumbusha kwamba uponyaji wa kimwili, kiroho, na kiakili mara nyingi hutokea baada ya muda kupita. Kama unahisi kuwa uponyaji wako hautokei haraka kama ambavyo ungependa, jaribu kutambua mafanikio madogo madogo uliyonayo. Omba na kuongea na Mungu kuhusu hisia zako, ukijumuisha na kumshukuru Yeye kwa maendeleo yoyote uliyoyaona.
Iwe tayari wewe ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Sikuza Mwisho, unayejifunza zaidi kuhusu injili, au unayerudi katika uanachama Kanisani, tafadhali jua kwamba tunakujali. Bila kujali zamani ilivyokuwa, au jinsi gani urefu wa barabara ulivyo hapo mbeleni, siku zako za baadae zinaweza kujazwa na mwanga wa Mungu. Njia ya injili inatupatia nguvu. Inatuletea faraja. Inatuelekeza kwenye furaha zaidi katika maisha haya na shangwe katika umilele.
Baba yako wa Mbinguni na Yesu Kristo wanajua na wanakupenda kiukamilifu. Kamwe hawatakuacha. Kamwe hawatakuumiza. Kamwe hawatakusahau.