Kukua katika Kanuni ya Ufunuo
Ninakuhimizeni kuchukua hatua muhimu ili kumsikia Bwana vyema na kwa mara nyingi zaidi ili kwamba muweze kupokea wongofu ambao Yeye anataka kuwapa.
Mnamo Septemba 30, 2017, kufuatia kikao cha jioni cha mkutano mkuu; nilisimama hospitalini ili kumjulia hali mpendwa mshirika mwenza wa akidi Mzee Robert D. Hales. Alikuwa amelazwa hospitalini hapo tangu alipopata shambulizi la moyo siku chache kabla.
Tuliongea sana, na alionekana kupata ahueni. Alikuwa akipumua mwenyewe, kitu ambacho kilikuwa ni dalili nzuri.
Jioni hiyo, hata hivyo, Roho aliongea moyoni na akilini mwangu kwamba ninapaswa kurudi hospitalini pale Jumapili. Wakati wa kikao cha Jumapili asubuhi cha mkutano mkuu, ule msukumo mkubwa ulirudi. Nilihisi napaswa kuacha kula chakula cha mchana na haraka niwahi pembeni mwa kitanda cha Mzee Hales mara kikao cha asubuhi kitakapokwisha, na hicho ndicho nilichofanya.
Nilipofika, niliweza kuona kwamba Mzee Hales hali yake ilibadilika na kuwa mbaya zaidi. Kwa huzuni, alifariki dakika 10 baada ya kufika kwangu, lakini ninashukuru kwamba nilikuwa kando yake pamoja na mke wake kipenzi, Mary, na watoto wao wa kiume wawili wakati alipoyaaga maisha haya.
Ni shukrani iliyoje kwamba minong’ono ya Roho Mtakatifu ilinishawishi kufanya kitu ambacho vinginevyo pengine nisingeweza kukifanya. Na jinsi gani ni mwenye shukrani kwa ajili ya uhalisi wa ufunuo na kwamba mbingu kwa mara nyingine zimefunguka.
Mwaka huu fokasi yetu kwa mafunzo binafsi na ya darasani itakuwa kwenye Mafundisho na Maagano. Huu “ufunuo matakatifu na matamko yenye mwongozo wa kiungu” yanaweza kubariki wale wote wanaojifunza na kuyafanyia kazi maelekezo yake matukufu. Yanawaalika “watu wote po pote walipo kuisikiliza sauti ya Bwana Yesu Kristo,”1 kwani hakika “sauti ya Bwana ni kwa watu wote” (Mafundisho na Maagano 1:2).
Hatari, Giza, Udanganyifu
Dhoruba za kimwili na kiroho ni sehemu ya maisha ya hapa duniani, kama vile COVID-19 janga la dunia lilivyotukumbusha. Kuhusu muda kabla ya Ujio Wake wa Pili, Mwokozi alitabiri zitakuwa siku za taabu kuu. Yeye alisema, “Patakuwa na njaa, na maradhi, na matetemeko ya ardhi, mahali mbali mbali” (Joseph Smith—Mathayo 1:29).
Kuchanganyika kwa taabu za jinsi hii ni ongezeko la giza na udanganyifu ambavyo vimetuzunguka. Kama Yesu alivyowaambia Wafuasi Wake, “Maovu yangeongezeka” kabla ya kurudi Kwake (Joseph Smith—Mathayo 1:30).
Shetani ameyapanga majeshi yake na anaghadhibika dhidi ya kazi ya Bwana na wale miongoni mwetu tuliojiingiza katika kazi hii. Kwa sababu ya ongezeko la hatari tunazokabiliana nazo, uhitaji wetu wa mwongozo wa kiungu haujawahi kuwa mkuu zaidi, na jitihada yetu ya kusikia sauti ya Yesu Kristo—Mpatanishi wetu, Mwokozi, na Mkombozi—kamwe haijawahi kuwa ya muhimu zaidi.
Kama nilivyosema muda mfupi baada ya kuitwa kuwa Rais wa Kanisa, kwamba Bwana yuko tayari kufunua mawazo Yake kwetu sisi. Hiyo ni moja ya baraka zake kubwa kwetu sisi.2
Katika siku yetu, Yeye ameahidi, “Ikiwa utaomba, nawe utapokea ufunuo juu ya ufunuo, maarifa juu ya maarifa” (Mafundisho na Maagano 42:61).
Ninajua Yeye atajibu kusihi kwetu.
Ni kwa jinsi gani Tunamsikia Yeye
Kujua jinsi Roho anavyozungumza ni muhimu sana leo. Ili kupokea ufunuo binafsi, ili kupata majibu, na ili kupokea ulinzi na maelekezo, tukumbuke utaratibu ambao Nabii Joseph Smith ameuweka kwa ajili yetu.
Kwanza, tunajizamisha wenyewe kwenye maandiko. Kwa kufanya hivyo tunafungua akili zetu na mioyo kwenye mafundisho na ukweli wa Mwokozi. Maneno ya Kristo “yanatuambia [sisi] mambo yote ambayo [sisi] tunapaswa kufanya” (2 Nefi 32:3), hususani katika siku hizi zisizo na uhakika na zenye mabadiliko ya ghafla.
Halafu tunaomba. Maombi yanahitaji moyo wa kujituma, kwa hiyo tunajinyenyekeza mbele za Mungu, tafuta mahali pa ukimya ambapo mara kwa mara tunaweza kwenda, na kumimina mioyo yetu Kwake.
Bwana anasema, “Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa; bisheni, nanyi mtafunguliwa” (Mafundisho na Maagano 88:63).
Kumsogelea Bwana kunaleta faraja na kutiwa moyo, matumaini na uponyaji. Hivyo basi, tunaomba katika jina lake kuhusu hofu zetu na udhaifu wetu, shauku zetu na wapendwa wetu, miito na maswali yetu.
Kisha tunasikiliza.
Kama tutabaki juu ya magoti yetu kwa muda baada ya kumalizika kwa maombi, mawazo, hisia, na maelekezo yatakuja katika mawazo yetu. Kuandika mawazo hayo kutatusaidia kukumbuka ni hatua gani Bwana angetaka tuchukue.
Tunaporudia mchakato huu, katika maneno ya Nabii Joseph Smith, tuta “kua katika Kanuni ya Ufunuo.”3
Kuwa wenye Kustahili Kupokea Ufunuo
Kutakasa uwezo wetu wa kutambua minong’ono ya Roho Mtakatifu na kuongeza kiwango chetu cha kupokea ufunuo kunahitaji ustahiki. Ustahiki hauhitaji ukamilifu, lakini unahitaji kwamba tujitahidi kuongezeka katika usafi.
Bwana anatarajia jitihada za kila siku, maboresho ya kila siku, na toba ya kila siku. Ustahiki unaleta usafi, na usafi unatustahilisha kwa ajili ya Roho Mtakatifu. Tunapomchukua “Roho Mtakatifu kama kiongozi [wetu]” (Mafundisho na Maagano 45:57), tunakuwa wenye kustahili ufunuo binafsi.
Kama kuna kitu kinachotuzuia sisi kufungua mlango wenye maelekezo ya mbinguni, yawezekana tukahitaji kutubu. Toba inaturuhusu kufungua mlango huo ili tuweze kusikia sauti ya Bwana mara kwa mara na kwa uwazi zaidi.
“Utaratibu uko wazi,” alifundisha Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Kama kuna kitu tunafikiria, kuona, kusikia, au kufanya ambacho kinatuweka mbali na Roho Mtakatifu, basi tunapaswa kuacha kufikiria, kukiona, kukisikiliza au kukifanya kitu hicho. Kama kile kimedhamiriwa kuburudisha, kwa mfano, kinatutenga kutoka kwa Roho Mtakatifu, basi kwa hakika aina hiyo ya burudani haitufai sisi. Kwa sababu Roho hawezi kustahimili utovu wa adabu, kisicho adilifu, au uchafu, basi ni dhahiri mambo ya jinsi hii siyo kwa ajili yetu sisi.”4
Tunapoongezea juu ya usafi na utiifu kwa kufunga, kutafuta kwa bidiii, kujifunza maandiko na maneno ya manabii walio hai na kazi ya hekaluni na historia ya familia, mbingu zitafunguka. Bwana, katika kuturudishia, atatimiza ahadi Yake: “Nitakupa Roho wangu, ambaye ataiangaza akili yako” (Mafundisho na Maagano 11:13).
Huenda tukahitaji kuwa wavumilivu, lakini Mungu atasema nasi katika njia Yake mwenyewe, na katika wakati wake mwenyewe.
Roho wa Uelewa
Ayubu alitamka, “Imo roho ndani ya mwanadamu na pumzi za Mwenyezi huwapa akili” (Ayubu 32:8). Katika mwaka huu mpya, ninakuhimiza kuchukua hatua stahiki ili kumsikia Bwana vyema zaidi na mara kwa mara ili ukapokee uongofu ambao Yeye anataka kukupatia.
Kabla ya kufariki Mzee Hales ile siku ya Oktoba 2017, alikuwa ameandaa hotuba kwa ajili ya ule mkutano mkuu hotuba ambayo hakuweza kuitoa. Katika hiyo hotuba, aliandika, “Imani yetu inatuandaa sisi kuwa katika uwepo wa Bwana.”5
Wakati tunapopokea ufunuo, tunautumia muda katika uwepo wa Mungu wakati anapotufunulia mawazo Yake, mapenzi Yake, na sauti Yake (ona Mafundisho na Maagano 68:4). Na tuiweke imani yetu katika vitendo, tukiliita jina Lake, tukiishi tukiwa wenye kustahili ahadi Yake ya mwongozo wa kiungu, na kutendea kazi mwongozo tunaopokea.