Njoo, Unifuatei: Mafundisho na Maagano 18–19
Thamani ya Kila Nafsi
Kwa nini sisi ni wa thamani sana kwa Baba yetu wa Mbinguni?
Hivi karibuni nilijisikia kujiunganisha tena na familia ambayo mwenza wangu na mimi tuliifundisha wakati tukiwa wamisionari wadogo karibia miaka 40 iliypoita huko Brussels, Ubelgiji. Ni muda mrefu umepita tangu niongee na yeyote miongoni mwao.
Kupitia maajabu ya siku hizi ya teknolojia, niliunganishwa na mama wa familia hii kwenye mtandao wa kijamii. Niliweza kuwa na maongezi ya kupendeza ya video na mama. Tulikumbushana kuhusu matukio matakatifu tuliyoshiriki pamoja nao miaka mingi iliyopita wakati familia yake ilipokuwa ikijifunza kuhusu injili ya urejesho.
Hakuwa katika afya nzuri, na mazingira yalikuwa yamemtenganisha na familia yake. Tulipokuwa tukiongea, nilihisi upendo wa kina ambao Baba wa Mbinguni na Mwokozi walio nao kwa dada huyu mwema. Nilihisi thamani yake kuu ya milele, ingawa kwa kiasi fulani ameteleza kutoka Kanisani. Nilieleza upendo wangu kwake na nikamshuhudia kwamba Mungu anampenda na kwamba anamjali. Machozi yalitujaa machoni wakati tulipoelezana upendo wetu kwa kila mmoja. Tulijiahidi kuwasiliana mara kwa mara. Nilishukuru sana kwa Mungu mjua yote na mwenye upendo kwa kunishawishi kumfikia mpendwa rafiki yangu huyu siku ile.
“Kwa nini” ya upendo wa Mungu
Wakati Nefi alipoulizwa maswali na malaika kuhusiana na upendo wa Mungu, kwa unyenyekevu alijibu, “Najua kwamba anawapenda watoto wake; walakini sijui maana ya vitu vyote” (1 Nefi 11:17). Mara kwa mara nimejiuliza jinsi gani Nefi alikuja kuelewa ukweli huu rahisi, mzuri: Mungu anawapenda watoto wake. Ni wazi kwamba alijua mafundisho ya Kristo kama yalivyofundishwa na “wazazi wake wema” (1 Nefii 1:1). Lakin yeye pia alijua “kwa nini “ ya Mwokozi. Na hiyo “kwa nini” ni kitu gani? …
Kwa nini Mungu alikuwa radhi kumwachia Mwanawe atumike kama dhabihu? Kwa nini alituleta sisi hapa ili tuthibitishwe na kujaribiwa? Kwa sababu, kama ilivyofundishwa katika ukweli mzuri ulio sawa, “Thamani ya nafsi ni kubwa machoni pa Mungu” (Mafundisho na Maagano 18:10).
Kwa nini sisi ni wa thamani kubwa hivyo Kwake? Kiasilia, kwa sababu sisi tu watoto Wake Anatupenda. Katika mistari michache ijayo, Yeye anaelezea zawadi kuu iliyotolewa kwa kila mmoja wetu kwa sababu ya upendo Wake kwetu- Mwanawe wa Pekee, Yesu Kristo. Alimtuma Mwanawe ili ateseke hadi “mauti katika mwili; kwa hiyo aliteseka maumivu ya watu wote, ili kwamba watu wote waweze kutubu na kuja kwake. Na amefufuka tena kutoka kwa wafu, ili apate kuwaleta watu wote kwake kwa masharti ya toba” (Mafundisho na Mafundisho na Maagano 18:11–12). Ametuambia, “Hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu”.
Toba na Shangwe
Si ajabu Baba wa Mbinguni anajisikia shangwe kubwa tunapotubu. Utayari wetu wa kutubu ni ushahidi wa shukrani yetu ya dhati kwa ukuu na kutolinganishwa kwa zawadi ya Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu. Ni kwa na kupitia Yesu Kristo pekee kwamba tunaweza kuwa wenye kustahili kusimamma kwa kujiamini katika uwepo wa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 121:45).
Rais Russell M. Nelson alielezea: “Watu wengi sana wanafikiria toba kama adhabu—kitu cha kukwepa isipokuwa katika hali iliyo mbaya sana. Lakini hisia hii ya kuwa unaadhibiwa inazalishwa na Shetani. Yeye hujaribu kutuzuia kutazama kwa Yesu Kristo, ambaye anasimama na mikono iliyonyooshwa, akitumaini na kuwa tayari kutuponya, kutusamehe, kutusafisha, kutuimarisha, na kututakasa sisi.
“Hakuna kinachotoa uhuru zaidi, cha kiungwana zaidi, au cha muhimu zaidi kwa maendeleo yetu binafsi kuliko ilivyo fokasi ya mazoea ya kila siku kwenye toba. Toba siyo tukio; ni mchakato. Ni muhimu kwa furaha na amani ya akili. Inapoambatana na imani, toba hufungua kufikia kwetu kwenye nguvu za Upatanisho wa Yesu Kristo.1
Umealikwa Kusaidia
Mara nyingi katika ufunuo wa siku za mwisho, Bwana anawaalika watoto Wake watumishi Wake ili wamsaidie Yeye na Mwanawe kazi ya wokovu na kuinuliwa (ona Mafundisho na Maagano 18:14). Fikiria hilo! Katika hali yetu ya kutokamilika, Mungu wa dunia hii alileta mwaliko kwetu sisi tuwasaidie watoto Wake, walio na thamani kuu, ili warudi kwake Yeye. Yeye anajua kazi ina changamoto Kutakuwa na wengi ambao hawataukubali mwaliko wetu wa “kumsikiliza Yeye” Hata hivyo, Yeye anasisitiza kwamba Yeye ni Mungu wa yule “mmoja.” “Na kama itabidi kwamba unapaswa kufanya kazi siku zako zote katika kuitia toba kwa watu hawa, na kuleta, japo iwe nafsi moja kwangu, shangwe yako itakuwa kuu kiasi gani pamoja naye katika ufalme wa Baba yangu!” (Mafundisho na Maagano 6:15; msisitizo umeongezwa.
Unaweza kujiuliza mwenyewe, “Je, ninaweza kufanya nini ili kumsaidia mtu kuja kwa Kristo, kutubu, na kubarikiwa na dhabihu yake ya kulipia dhambi?”
Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitoa ushauri huu kuhusu kushiriki katika kazi ya wokovu na kuinuliwa: “Elewa kwamba si kazi yako wewe kuwaongoa watu. Huo ni wajibu wa Roho Mtakatifu. Wajibu wako ni kushiriki yaliyo moyoni mwako na kuishi kulingana na imani yako.
“Hivyo, usikatishwe tamaa kama mtu asipokubali ujumbe wa injili mara moja. Huko sio kushindwa binafsi.
“Hiyo ni kati ya mtu binafsi na Baba wa Mbinguni.
“Kazi yako ni kumpenda Mungu na jirani zako, watoto Wake.
“Amini, penda, tenda.
“Fuata njia hii, na Mungu atafanya kazi ya miujiza kupitia wewe ya kubariki watoto wake wa thamani.”2
Pande Zote Mbili za Pazia.
Mwaliko wa kuja kwa Kristo kupitia toba haujabakishwa kwa ajili ya wale ambao wanaishi duniani tu. Wafu wanaotubu watakombolewa, kupitia utiifu wa ibada za nyumba ya Mungu” (Mafundisho na Maagano 138:58). Kazi ya hekaluni na historia ya familia ni vipengele muhimu vya kuwakusanya Waisraeli waliotawanyika pande zote za pazia. Tunaweza kujisikia shangwe kuu tunapofanya kazi kwa ajili ya wale waliokwenda kwenye ulimwengu wa roho wakijua kwamba katika ulimwengu ule, kama Rais Wilford Woodruff (1807–98) alivyosema, “kutakuwa na wachache sana, kama atakuwepo, ambaye hataikubali Injili.”3 Pasipo shaka, wataitazamia kwa hamu siku ambayo ibada okozi zitafanywa kwa ajili yao katika nyumba ya Bwana.
Mzee Dale G. Renlund wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Tunapokusanya historia za familia zetu na kwenda nazo hekaluni kwa niaba ya mababu wetu, Mungu anatimiza nyingi ya baraka hizi zilizoahidiwa kwa wakati mmoja pande zote mbili za pazia. Vile vile, tunabarikiwa tunapowasaidia wengine katika kata na vigingi vyetu kufanya vivyo hivyo. Waumini ambao hawakai jirani na hekalu pia hupokea baraka hizi kwa kushiriki katika kazi ya historia za familia, kukusanya majina ya wahenga wao kwa ajili ya ibada za hekaluni ili zipate kufanywa.”4
Inapendeza kujua kwamba Baba yetu wa Mbinguni anampenda kila mmoja wa watoto Wake wote. Sisi ni wa thamani kubwa Kwake. Kila mmoja wetu analo jukumu takatifu la kuwatumikia watoto Wake walio pande zote mbili za pazia na kuwasaidia kufikia stahiki yao kuu.
Wasaidie Waone Thamani Yao
Ninawaalika ninyi kuwafikia wale ambo wamekuwa sehemu ya maisha yako na pengine wamesahaulika kwa muda. Waendee wale ambao wameondoka kwenye njia ya agano. Watumikie wale walio na shida ya upendo kama wa Kristo. Jiunganishe na wale walio upande mwingine wa pazia kupitia kazi za hekaluni na historia za familia, ikijumuisha kuorodhesha. Wasaidie wengine kuona upendo wa Mungu kupitia wewe?Kama ilivyoahidiwa, rafiki yangu mpendwa wa kibelgiji pamoja nami tulizungumza kila Jumapili kwa zaidi ya miezi minne. Nilimwalika kupakua programu ya Maktaba ya Injili. Rais wa tawi wa eneo lake alifahamishwa kuhusu yeye, na wamisionari walimtembelea na kumpa baraka za ukuhani. wiki iliyofuata kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 30, alishiriki kwenye mkutano wa Sakramenti. Mara ya mwisho tulipozungumza, alijawa na shangwe ya kuuunganishwa na mwili wa Kanisa la Yesu Kristo.
Mwishoni mwa maongezi na mpendwa rafiki yangu Mbelgiji, aliniambia kwamba msichana wake mkubwa bado alikuwa anajihusisha na Kanisa. Mara moja nilimfikia binti yake huyo kwa njia ya video. Akanitambulisha kwa kila mmoja wa watoto wake wanne warembo, kisha akaniambia kwamba wamisionari walikuwa wanakuja hapo usiku ule kwa ajili ya kula chakula. Ni baraka iliyoje kuona kwamba bado alikuwa muumini mwaminifu wa Kanisa.
Nilipokuwa naongea naye, nilielewa, kwa kiwango kidogo, ujumbe wa andiko hili: “Na sasa, kama shangwe yako itakuwa kubwa kwa hiyo nafsi moja ambayo umeileta kwangu katika ufalme wa Baba yangu, itakuwa shangwe kubwa namna gani kwako kama utazileta nafsi nyingi kwangu!” (Mafundisho na Maagano 6:16).
Thamani ya kila nafsi ni kuu!