Mafundisho na Maagano 2021
Julai 25. Kwa nini Niwe Mtiifu kwa Amri za Mungu? Mafundisho na Maagano 81–83


“Julai 25. Kwa nini Niwe Mtiifu kwa Amri za Mungu? Mafundisho na Maagano 81–83,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2021 (2020)

“Julai 25. Kwa nini Niwe Mtiifu kwa Amri za Mungu?” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2021

wasichana wakiimba

Julai 25

Kwa nini Niwe Mtiifu kwa Amri za Mungu?

Mafundisho na Maagano 81–83

ikoni ya kushauriana kwa pamoja

Shaurianeni kwa Pamoja

Ikiongozwa na mshiriki wa urais wa akidi au wa darasa; takribani kwa dakika 10–20

Mwanzoni mwa mkutano, rudieni kwa pamoja Dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni au Dhima ya Wasichana. Kisha ongoza majadiliano kuhusu vitu kama vifuatavyo, na panga njia za kutenda juu ya kile mnachojadiliana (mnaweza kuamua katika mkutano wa urais ni vitu gani vya kujadili):

  • Akidi au darasa letu. Tunaweza kufanya nini ili kujenga umoja miongoni mwa washiriki wa akidi au darasa? Je, ni malengo gani tunahitaji kuyashughulikia pamoja?

  • Wajibu wetu au majukumu. Tunafanya nini ili kushiriki injili? Ni uzoefu upi tumeupata kwa kufanya kazi ya hekalu na historia ya familia?

  • Maisha yetu. Ni kwa jinsi gani tumeuona mkono wa Bwana katika maisha yetu? Ni nini kimetupatia mwongozo wa kiungu katika kujifunza kwetu maandiko wiki hii?

Mwishoni mwa somo, kama inafaa, fanya yafuatayo:

  • Shuhudia juu ya kanuni zilizofundishwa.

  • Wakumbushe washiriki wa akidi au darasa kuhusu mipango na mialiko iliyotolewa wakati wa mkutano.

ikoni ya kufundisha mafundisho

Fundisha Mafundisho

Ikiongozwa na kiongozi mtu mzima au kijana; takribani kwa dakika 25–35

Jiandae Binafsi Kiroho

Tunaweza kuhisi nyakati zingine kwamba amri za Mungu zinazuia uhuru wetu na kuweka ukomo kwenye haki yetu ya kujiamulia. Ukweli ni kwamba amri hukuza uhuru wetu. Katika Mafundisho na Maagano 82:8–10 tunajifunza kwamba amri hutusaidia kuelewa matakwa ya Mungu, na tunapozitii, matendo yetu “yatageuka [kwetu] kwa ajili ya wokovu [wetu].” Kwa kweli, tunapomtii Mungu, “Anafungwa” ili kutupatia baraka zote Alizotuahidi (mistari 9–10). Ni kwa jinsi gani Baba wa Mbinguni amekubariki kwa kadiri ulivyotii amri Zake? Ili kujiandaa kufundisha, unaweza kusoma ujumbe wa Mzee Dale G. Renlund “Kujaa Tele kwa Baraka” (Liahona, Mei 2019, 70–73) au tafakari baadhi ya nyenzo katika makala ya Mada za Injili “Utiifu” (topics.ChurchofJesusChrist.org).

msichana akijifunza

Mifano ya kale ya watumishi waaminifu wa Mungu inaweza kututia moyo sisi kuishi kwa uaminifu hivi leo.

Jifunzeni Pamoja

Washiriki wa akidi yako au darasa lako wanaweza wakawa wanakumbana na ugumu wa kutii baadhi ya amri. Kuwasaidia wao kuelewa kwa nini utiifu ni muhimu kunaweza kuwatia moyo. Andika kichwa cha habari cha muhtasari huu ubaoni, na waalike washiriki wa akidi au darasa kushiriki majibu. Unaweza kuwaomba watafute uelewa wa ziada katika Mafundisho na Maagano 82:8–10, ambao wanaweza kuwa wameusoma wiki hii. Kisha chagua shughuli moja au zaidi zilizopo hapa chini ili kuwasaidia kuelewa vyema kwa nini ni muhimu siku zote kumtii Mungu, hata kama kufanya hivyo ni vigumu.

  • Inaweza kuwa rahisi sana kutii amri pale tunapoelewa sababu ya kufanya hivyo. Ili kujifunza kwa nini Mungu ametupatia amri, washiriki wa akidi au darasa wanaweza kupitia marejeo ya maandiko katika “Nyenzo Saidizi” (au mengine unayoyafikiria). Maandiko haya yanatusaidiaje wakati tunapoona ni vigumu kutii amri? Kama sehemu ya mjadala huu, mnaweza kusoma pamoja sehemu iliyo na kichwa cha habari “Nne, usisahau ‘kwa nini’ ya injili” katika ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Usinisahau” (Liahona, Nov. 2011, 122).

  • Wakati wale unaowafundisha wanapoelewa mfano mkamilifu wa Mwokozi wa utiifu, wanaweza kutiwa moyo kumtii Mungu kikamilifu zaidi. Ni wakati gani Yesu kristo alimtii Baba yake, hata katika nyakati ngumu? (Ona Mathayo 4:1–11; Luka 22:39–44). Mifano ya wanaume na wanawake ambao walikuwa watiifu inaweza kupatikana katika Waebrania 11. Huenda akidi yako au darasa lako linaweza kuchagua mojawapo ya mifano hii—au mingineyo wanayoijua, ikiwa ni pamoja na ya familia zao—na kushiriki kile kinachowahamasisha kuhusu watu hawa. Kwa nini walichagua kumtii Bwana? Ni kwa jinsi gani Mwokozi hutusaidia wakati tunapochagua kuwa watiifu?

  • Ili kuwasaidia washiriki wa akidi au darasa kuona amri kama baraka na si kama mzigo, unaweza kushiriki mafundisho ya Mzee D. Todd Christofferson yanayopatikana katika “Nyenzo Saidizi.” Unaweza kuonesha au kuchora picha ya ngazi na kuwaomba wale unaowafundisha kujaza kila kipandio katika ngazi kwa amri ambayo inaweza kuwa ngumu kwa kijana kuielewa au kuitii. Ni kwa jinsi gani maneno ya Mzee Christofferson yanaweza kumsaidia yule anayekabiliana na ugumu wa kutii amri?

  • Baadhi ya video zinazofundisha kuhusu utiifu zinaweza kupatikana katika ChurchofJesusChrist.org na katika app ya Gospel Library (ona “Nyenzo Saidizi”). Unaweza kumpangia majukumu kila mshiriki wa akidi au darasa kuangalia mojawapo ya video hizi kabla ya mkutano na waje wakiwa wamejiandaa kushiriki kile walichojifunza kuhusu utiifu. Labda akidi au darasa linaweza kupanga video yao wenyewe kuhusu kutii amri za Mungu. Kisha wanaweza kupanga shughuli ya kutengeneza video na kuishiriki katika mtandao wa kijamii.

Tenda kwa Imani

Wahimize washiriki wa akidi au darasa kutafakari na kuandika kile watakachokifanya ili kutenda juu ya misukumo ambayo wameipokea leo. Ni kwa jinsi gani somo la leo linahusiana na malengo binafsi ambayo wameyaweka? Kama watapenda, washiriki wa akidi au darasa wanaweza kushiriki mawazo yao.

Nyenzo Saidizi

  • 1 Nefi 17:3; Mosia 2:41; Mafundisho na Maagano 130:20–21 (Tunabarikiwa kwa utiifu wa amri)

  • Kumbukumbu la Torati 10:12–13; Yohana 14:15; 1 yohana 5:1–3 (Tunatii amri kwa sababu tunampenda Mungu)

  • Mafundisho na Maagano 93:20 (Utiifu huturuhusu kupokea utimilifu wa Mungu)

  • Obedience,” katika Sura ya 3 ya Preach My Gospel (2019), 75

  • Mzee D. Todd Christofferson alifundisha: “Baadhi huona tu dhabihu na vikwazo katika utiifu wa amri za agano jipya na lisilo na mwisho, lakini wale wanaouishi uzoefu— wanaojitoa bure na kikamilifu kwenye maisha ya agano—hupata uhuru na utimilifu mkubwa. Wakati tunapoelewa kikamilifu, tunatafuta amri nyingi zaidi, na siyo chache. Kila sheria mpya au amri tunayojifunza na kuiishi ni sawa na kusonga katika kipandio cha ngazi kinachofuatia au hatua katika ngazi ambayo hutusaidia sisi kupanda juu zaidi na zaidi. Kwa kweli, maisha ya injili ni maisha mazuri” (“The Power of Covenants,” Liahona, Mei 2009, 23).

  • Video “The Sting of the Scorpion,” “Stay within the Lines,” “A Secure Anchor,” “Shower of Heavenly Blessings,” “Blessed and Happy Are Those Who Keep the Commandments of God,” ChurchofJesusChrist.org

Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

Mwokozi aliwaalika wanafunzi wake kushuhudia, na walipofanya hivyo, Roho aligusa mioyo yao. Wakati unapofundisha, alika washiriki wa akidi au darasa kushiriki shuhuda zao za umuhimu wa kutii amri.