2010–2019
Kuwa na Baraka Tele
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


2:3

Kuwa na Baraka Tele

Baraka nyingi ambazo Mungu anataka kutupatia zinahitaji matendo kwa upande wetu—matendo yanayotegemea imani yetu katika Yesu Kristo.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanatamani kumbariki kila mmoja wetu.1 Swali kuhusu namna ya kupata na kupokea baraka hizo limekuwa mada ya mdahalo wa kithiolojia na mjadala kwa karne nyingi.2 Baadhi wanashikilia kauli kwamba baraka zinapatikana kweli; tunazipokea tu kupitia kuzifanyia kazi. Wengine wanatoa hoja kwamba Mungu tayari amechagua yule Atakayembariki na kwa namna gani—na kwamba maamuzi haya hayawezi kubadilika. Misimamo yote miwili ina dosari kimsingi. Baraka kutoka mbinguni hazipatikani kwa kiherehere kukusanya “kuponi za matendo mema,” au kwa kusubiri bila matumaini kuona kama tutashinda bahati nasibu ya baraka. La, ukweli una tofauti ndogo sana lakini unafaa zaidi kwa ajili ya uhusiano baina ya Baba mpendwa wa Mbinguni na wale wanaoweza kuwa warithi Wake—sisi. Ukweli uliorejeshwa unaonyesha kwamba baraka kamwe hazichumwi tu, lakini matendo yaliyochochewa na imani kwa upande wetu, yote ya awali na endelevu, ni muhimu.3

Lundo la kuni

Tunapofikiria jinsi ambavyo tunaweza kupokea baraka kutoka kwa Mungu, acha tufananishe baraka kutoka mbinguni na lundo la kuni. Fikiria katikati ya tuta dogo la vijiti vya kuwashia moto, likiwa na tabaka la punje za mbao juu yake. Vijiti vinafuata, kisha vigogo vidogo, na hatimaye magogo makubwa. Lundo hili la kuni lina chanzo kikubwacha moto, chenye uwezo wa kutoa mwangaza na joto kwa siku kadhaa. Piga taswira ya njiti moja ya kiberiti yenye ncha ya fosforasi kando ya lundo hili la kuni.4

Lundo la kuni pamoja na kiberiti

Ili nishati iliyo ndani ya lundo la kuni itolewe, ncha ya njiti inahitaji kuwashwa na vijiti vya kuwashia moto kuwaka. Tuta dogo la vijiti vya kuwashia moto litashika moto kwa haraka na kusababisha lundo la kuni kuchomeka. Mara tu mwako huu unapoanza, unaendelea hadi kuni zote zimechomeka au moto unapokosa oksijeni.

Lundo la kuni likichomeka

Kuwasha njiti na kuwasha vijiti vidogo vya kuwashia moto ni matendo madogo ambayo yanawezesha nishati ifaayo ya kuni kutokea.5 Ni mpaka njiti inapowashwa, hakuna kinachotokea, bila kujali ukubwa wa lundo la kuni. Ikiwa njiti itawashwa bila kuwasha vijiti vidogo vya kuwashia moto, kiasi cha mwangaza na joto kinachotolewa na njiti peke yake ni kidogo sana na nishati ya mwako ndani ya kuni inasalia ndani yake. Kama oksijeni haitapatikana kwa wakati wowote, mwako hautokei.

Katika njia sawa na hiyo, baraka nyingi ambazo Mungu anataka kutupatia zinahitaji matendo kwa upande wetu—matendo yanayotegemea imani yetu katika Yesu Kristo. Imani katika Mwokozi ni kanuni ya matendo na nguvu.6 Kwanza tunatenda kwa imani; kisha nguvu inakuja—kulingana na mapenzi ya Mungu na muda Wake. Utaratibu huu ni muhimu.7 Matendo yanayohitajika, hata hivyo, daima ni madogo yanapolinganishwa na baraka ambazo hatimaye tunapokea.8

Fikiria kile kilichotokea wakati nyoka wa moto, wanaoruka walikuja miongoni mwa Waisraeli wa kale wakiwa njiani kuelekea katika nchi ya ahadi. Kuumwa na nyoka wenye sumu kulisababisha kifo. Lakini mtu aliyeumwa angeweza kupona kwa kutazama nyoka wa shaba aliyetengenezwa na Musa na kuwekwa juu ya mti.9 Je, inachukua nguvu kiasi gani kutazama kitu fulani? Wote waliotazama walipata nguvu za mbinguni na walipona. Waisraeli wengine walioumwa walikataa kumtazama yule nyoka wa shaba na walikufa. Pengine walikosa imani ya kutazama.10 Pengine hawakuamini kwamba kitendo rahisi kama hiki kingeweza kuchochea uponyaji ulioahidiwa. Au pengine walishupaza mioyo yao kwa hiari yao na kukataa ushauri wa nabii wa Mungu.11

Kanuni ya kuwezesha baraka zinazotoka kwa Mungu ni ya milele. Kama wale Waisraeli wa kale, sisi pia lazima tufanyie kazi imani yetu katika Yesu Kristo ili tuweze kubarikiwa. Mungu amefunua kwamba “kuna sheria, isiyotenguliwa iliyowekwa mbinguni kabla ya misingi ya ulimwengu huu, ambapo juu yake baraka zote hutoka—Na kama tunapata baraka yoyote kutoka kwa Mungu, ni kutokana na utii kwa sheria ile ambayo juu yake hutoka.”12 Kwa kusema hayo, hauwezi tu kuchuma baraka—dhana hiyo si kweli—lakini unahitaji kuwa mwenye kustahili kuipata. Wokovu wetu unakuja tu kupitia fadhili na neema za Yesu Kristo.13 Ukubwa wa dhabihu Yake ya Upatanisho humaanisha kwamba lundo la kuni halina kikomo; matendo yetu duni yanakaribia sufuri yakilinganishwa. Lakini si sufuri, na yana umuhimu; katika giza, njiti iliyowashwa inaweza kuonekana kutoka mbali. Kwa kweli, yanaweza kuonekana mbinguni kwa sababu matendo madogo ya imani yanahitajika kuwasha ahadi za Mungu.14

Ili kupokea baraka unayotaka kutoka kwa Mungu, tenda kwa imani, na kuwasha njiti ya kisitiari ambayo kwayo baraka ya mbinguni hutegemewa. Kwa mfano, mojawapo ya madhumuni ya sala ni kupata baraka ambazo Mungu alikuwa tayari anataka kutupatia lakini hilo hutendeka chini ya masharti ya kuziomba.15 Alma alilia kwa ajili ya huruma, na uchungu wake ukaondolewa; hakuteseka tena na ufahamu wa dhambi zake. Shangwe yake ilizidi uchungu wake—yote kwa sababu alilia kwa imani katika Yesu Kristo.16 Nishati ya kuwezesha inayohitajika kwetu ni kuwa na imani ya kutosha katika Kristo kumuomba Mungu kwa dhati kupitia sala na kukubali mapenzi Yake na muda Wake kwa ajili ya jibu.

Mara nyingi, nishati inayohitajika kwa ajili ya baraka inahitaji zaidi ya kutazama au kuomba tu; matendo endelevu, ya kujirudia yaliyojawa na imani, yanahitajika. Katikati ya karne ya 19, Brigham Young alielekeza kundi la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuchunguza na kufanya makao Arizona, eneo kavu Amerika ya Kaskazini. Baada ya kufika Arizona, kundi liliishiwa maji na kuwa na wasiwasi kwamba wangeangamia. Walimsihi Mungu awape msaada. Baada ya muda mfupi mvua na theluji ilianguka, na kuwapa nafasi ya kujaza mitungi yao kwa maji na kunywesha mifugo yao. Wakiwa na shukrani na nguvu mpya, walirudi katika Jiji la Salt Lake wakisherehekea wema wa Mungu. Waliporudi, walitoa ripoti ya safari yao kwa Brigham Young na kutoa hitimisho lao kwamba Arizona ilikuwa haikaliki.

Brigham Young

Baada ya kusikiliza ripoti hiyo, Brigham Young alimuuliza mwanaume aliyekuwa chumbani mawazo yake kuhusu safari hiyo na muujiza ule. Mwanaume huyo, Daniel W. Jones, kwa maneno machache alijibu, “Ningelijaza, na kuendelea, na kusali tena.” Kaka Brigham aliweka mkono wake juu ya Kaka Jones na kusema, “Huyu ndiye mwanaume atakayeongoza safari ijayo kwenda Arizona.”17

Daniel W. Jones

Sote tunaweza kukumbuka nyakati ambazo tumeendelea na kusali tena—na baraka zikaja. Uzoefu wa Michael na Marian Holmes unadhihirisha kanuni hizi. Michael na mimi tulihudumu pamoja kama Sabini wa Eneo. Siku zote nilifurahia wakati wowote alipoitwa kusali katika mikutano yetu kwa sababu upendo wake wa dhati kwa mambo ya kiroho ulikuwa bayana; alijua jinsi ya kunena na Mungu. Nilipenda kumsikiliza akisali. Mapema katika ndoa yao, hata hivyo, Michael na Marian hawakuwa wakisali au kuhudhuria kanisani. Walijishughulisha na watoto watatu wadogo na kampuni ya ujenzi yenye mafanikio. Michael hakuhisi kwamba alikuwa mcha Mungu. Jioni moja, askofu wao alienda nyumbani kwao na kuwatia moyo waanze kusali.

Baada ya askofu kuondoka, Michael na Marian waliamua kwamba wangejaribu kusali. Kabla ya kwenda kulala, walipiga magoti kando ya kitanda chao na, kwa wasiwasi, Michael akaanza. Baada ya maneno machache ya sala yasiyo stadi, Michael ghafla alinyamaza, na kusema, “Marian, siwezi kufanya hili.” Aliposimama na kuanza kuondoka, Marian alimshika mkono, akamvuta na kumrudisha kupiga magoti, na kusema, “Mike, unaweza kufanya hili. Jaribu tena!” Akiwa ametiwa moyo, Michael alimalizia sala yake fupi.

Familia ya Holmese walianza kusali kila mara. Walikubali mwaliko wa jirani kuhudhuria kanisani. Walipoingia kanisani na kusikia wimbo wa kufungua mkutano, Roho aliwanong’oneza, “Hii ni kweli.” Baadae, bila kuonekana na bila kuombwa, Michael alisaidia kuondoa taka kutoka kwenye nyumba ya mikutano. Alipokuwa akifanya hivyo, alihisi msukumo dhahiri, “Hii ni nyumba Yangu.”

Michael mdogo pamoja na Marian Holmes

Michael na Marian walikubali miito ya Kanisa na kuhudumu katika kata na kigingi chao. Waliunganishwa wao wenyewe, na watoto wao 3 waliunganishwa kwao. Watoto zaidi walifuatia, na kufikia idadi ya 12. Michael na Marian Holmese walihudumu kama rais wa misheni na mwenza wake—mara mbili.

Michael na Marian Holmes leo

Sala ya kwanza liyotatizika ilikuwa kitendo kidogo lakini kilichojawa na imani ambacho kilichochea baraka za mbinguni. Familia ya Holmese walilisha miale ya imani kwa kuhudhuria kanisani na kuhudumu. Ufuasi wao wa kujitolea kwa miaka mingi umesababisha moto mkubwa ambao unatia msukumo hadi siku ya leo.

Familia kubwa ya Holmes

Moto, hata hivyo, lazima upate nguvu ya mara kwa mara ya oksijeni ili kuni hatimaye iweze kutoa uwezo wake kamili. Kama ilivyodhihirishwa na Michael na Marian Holmes, imani katika Kristo inahitaji matendo endelevu ili mwako uendelee. Matendo madogo huongeza uwezo wetu wa kutembea katika njia ya agano na kuelekeza hadi kwenye baraka kuu zaidi ambazo Mungu anaweza kutoa. Lakini oksijeni inatiririka tu ikiwa kitamathali tunasonga kwa miguu yetu. Wakati mwingine tunahitajika kutengeneza upinde na mshale kabla ya ufunuo kuja kuhusu ni wapi tutafute chakula.18 Wakati mwingine tunahitaji kutengeneza vifaa kabla ya ufunuo kujua kuhusu namna tutakavyojenga merikebu.19 Wakati mwingine, kufuatia maelekezo ya nabii wa Bwana, tunahitajika kuoka keki ndogo kwa kutumia kiasi kidogo cha mafuta na unga ili kupokea chupa ya mafuta yasiyoisha na kiasi cha unga kisichoisha.20 Na wakati mwingine tunahitajika “kusimama imara, na kujua kuwa [Mungu ni] Mungu” na kuamini katika wakati wake.21

Wakati unapopokea baraka yoyote kutoka kwa Mungu, unaweza kuhitimisha kwamba umetii sheria fulani ya milele inayosimamia upokeaji wa baraka hiyo.22 Lakini kumbuka kwamba sheria “isiyotenguliwa iliyowekwa” haitegemei wakati, ikiwa na maana kwamba baraka huja kulingana na ratiba ya Mungu. Hata manabii wa kale waliokuwa wakitafuta nyumba yao ya mbinguni23 “wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali … [na] kuzishangilia … na kukiri .”24 Ikiwa baraka inayotarajiwa kutoka kwa Mungu haijatolewa—bado—hauhitaji kushikwa na wazimu, ukijiuliza ni kipi cha ziada unahitajika kufanya. Badala yake, sikiliza ushauri wa Joseph Smith wa “kwa furaha kufanya mambo yote yaliyo katika uwezo [wako] ; na ndipo … tusimame imara, kwa uhakika mkubwa, kuona … mkono [wa Mungu] … ukifunuliwa.”25 Baadhi ya baraka zimewekwa akiba hadi baadae, hata kwa ajili ya watoto wa Mungu wanaostahimili kwa ujasiri.26

Miezi sita iliyopita mpango unaolenga-nyumbani, na unaosaidiwa na Kanisa wa kujifunza mafundisho, kuimarisha imani, na kuimarisha watu binafsi na familia ulitambulishwa. Rais Russell M. Nelson aliahidi kwamba mabadiliko hayo yanaweza kutusaidia kunusurika kiroho, kuongeza shangwe yetu ya injili, na kuongeza kina cha uongofu wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.27 Lakini ni juu yetu sisi kudai baraka hizi. Kila mmoja wetu anawajibika kufungua na kusoma Njoo, Unifuate Kwa—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia, pamoja na maandiko na nyenzo zingine za Njoo, Unifuate.28 Tunahitaji kuzijadili pamoja na familia na marafiki zetu na kupanga siku yetu ya Sabato kuwasha moto wa kisitiari. Au tunaweza kuziacha nyenzo hizo zikiwa zimelundikwa katika nyumba zetu na nishati muhimu ikiwa imenaswa ndani yake.

Ninakualika uamshe kwa uaminifu nguvu ya mbinguni ili uweze kupokea baraka maalum kutoka kwa Mungu. Fanyia kazi imani ya kuwasha njiti na kuwasha moto. Toa oksijeni inayohitajika wakati ukimngoja Bwana kwa subira. Kwa mialiko hii, ninaomba kwamba Roho Mtakatifu atawaongoza na kuwaelekeza, ili ninyi, kama yule mtu mwaminifu anayeelezewa katika Mithali, muweze “kuwa na baraka tele.”29 Ninashuhudia kwamba Baba yenu wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, wanaishi, wanajali ustawi wenu, na wanafurahia kuwabariki, katika jina la Yesu Kristo, amina.