Akidi: Mahali pa Kuwa
Bwana angetaka uwe na akidi imara. Anapowakusanya watoto Wake, wanahitaji mahali pa kuwa na kukua.
Mwaka 2010, Andre Sebako alikuwa mvulana aliyekuwa akitafuta ukweli. Ingawaje hakuwa amewahi kusali kwa dhati hapo awali, aliamua kujaribu. Muda mfupi baadae, alikutana na wamisionari. Walimpa kadi iliyokuwa na picha ya Kitabu cha Mormoni. Andre alihisi kitu na akauliza kama wamisionari wangeweza kumuuzia hicho kitabu. Walimwambia angepata kitabu hicho bila malipo kama angekuja kanisani.1
Andre alihudhuria Tawi la Mochudi kule Botswana, Afrika, lililokuwa limeundwa karibuni, peke yake. Lakini tawi lilikuwa lenye upendo, kundi lenye uhusiano wa karibu lililokuwa na takriban waumini 40.2 Walimkaribisha Andre kwa mikono mikunjufu. Alipokea masomo ya kimisionari na akabatizwa. Ilikuwa ya kupendeza!
Lakini kisha nini? Ni jinsi gani Andre angezidi kushiriki kikamilifu? Ni nani angemsaidia kuendelea katika njia ya agano? Jibu moja kwa swali hilo ni akidi yake ya ukuhani!3
Kila mwenye ukuhani, bila ya kujali hali yake, hunufaika kutokana na akidi imara. Kaka zangu vijana wenye Ukuhani wa Haruni, Mungu anataka muwe na akidi imara, mahali pa kuwepo kwa kila mvulana, mahali ambapo Roho wa Bwana yupo, mahali ambapo washiriki wote wa akidi wanakaribishwa na kuthaminiwa. Bwana anapowakusanya watoto Wake, wanahitaji mahali pa kuwa na kukua.
Kila mmoja wenu nyinyi washiriki wa urais wa akidi mnaongoza njia mnapotafuta msukumo4 na kukuza upendo na undugu miongoni mwa washiriki wote wa akidi. Mnawapa usikivu maalumu wale ambao ni washiriki wapya, ambao hawashiriki kikamilifu, au wale walio na mahitaji maalumu.5 Kwa nguvu za ukuhani, mnajenga akidi imara.6 Na akidi yenye nguvu, iliyoungana inaleta tofauti kubwa sana katika maisha ya mvulana.
Wakati Kanisa lilipotangaza kufokasi upya juu ya kujifunza injili kunakolenga nyumbani,7 baadhi walifikiria juu ya waumini kama Andre na kuuliza, “Itakuwaje kwa vijana wanaotoka katika hali ya familia ambapo injili haifunzwi na ambapo hakuna mazingira ya kujifunza na kuishi injili nyumbani? Je, wataachwa nyuma?”
La! Hakuna anayeweza kuachwa nyuma! Bwana anampenda kila mvulana na kila msichana. Sisi, kama wenye ukuhani, ni Mikono ya Bwana. Sisi ni msaada wa Kanisa kwa juhudi zinazolenga nyumbani. Wakati kuna msaada kidogo nyumbani, akidi za ukuhani na viongozi wengine na marafiki huchunga na kumsaidia kila mmoja na familia jinsi inavyohitajika.
Nimeona hili likitendeka. Nimepata uzoefu wa hili. Wakati nilipokuwa na umri wa miaka sita, wazazi wangu walitalikiana na baba yangu akamuacha mama yangu na watoto watano wadogo. Mama yangu alianza kufanya kazi ili atosheleze mahitaji yetu. Alihitaji ajira ya pili kwa muda fulani, pamoja na elimu ya ziada. Kulikuwa na muda mchache kwake kwa ajili ya kulea. Lakini babu na bibi, wajomba, shangazi, maaskofu, na walimu wa nyumbani walijitokeza kumsaidia malaika mama yangu.
Na nilikuwa na akidi. Nina shukrani sana kwa rafiki zangu—kaka zangu—ambao walinipenda na kunisaidia. Akidi yangu ilikuwa mahali pa kuwepo. Baadhi wanaweza kuwa waliniona kama nisiye na uwezo wa kufaulu na nisiyeweza kwa sababu ya hali ya familia yangu. Pengine nilikuwa hivyo. Lakini akidi za ukuhani zilibadilisha hali hizo. Akidi yangu ilinizingira na kubariki maisha yangu bila kipimo.
Kuna wengi kutuzunguka wanaoonekana hawana uwezo wa kufaulu na kuweza vitu. Pengine sisi sote tuko hivyo kwa namna moja au nyingine. Lakini kila mmoja wetu hapa ana akidi, mahali ambapo tunaweza kupokea nguvu na kupeana nguvu. Akidi ni “wote kwa ajili ya mmoja na mmoja kwa ajili ya wote.”8 Ni mahali ambapo tunaelimishana, tunawatumikia wengine, na kujenga umoja na undugu tunapomtumikia Mungu.9 Ni mahali ambapo miujiza hufanyika.
Ningependa kuwaelezea baadhi ya miujiza ambayo ilifanyika katika akidi ya Andre kule Mochudi. Ninaposhiriki mfano huu, tafuta kanuni ambazo huimarisha kila akidi ya ukuhani inayozitumia.
Baada ya Andre kubatizwa, aliandamana na wamisionari wakati walipowafundisha wavulana wengine wanne, ambao walibatizwa pia. Sasa kulikuwa na wavulana watano. Walianza kuimarishana wao kwa wao na kuimarisha tawi.
Mvulana wa sita, Thuso, alibatizwa. Thuso alishiriki injili pamoja na rafiki zake watatu, na punde wakawa tisa.
Wafuasi wa Yesu Kristo mara nyingi hukusanywa kwa njia hii—wachache kwa wakati mmoja, wanapoalikwa na rafiki zao. Siku za kale, wakati Andrea alipompata Mwokozi, kwa haraka alienda kwa kaka yake Simoni na “akampeleka kwa Yesu.”10 Vile vile, punde tu Filipo alipogeuka kuwa mfuasi wa Kristo, alimwalika rafikiye Nathanaeli “njoo uone.”11
Kule Mochudi, mvulana wa 10 alijiunga na Kanisa baada ya muda mfupi. Wamisionari walimpata wa 11. Na mvulana wa 12 alibatizwa baada ya kuona athari za injili katika maisha ya rafiki zake.
Washiriki wa Tawi la Mochudi walijawa na furaha. Wavulana hawa “waliongoka kwa Bwana, na … waliunganishwa na kanisa.”12
Kitabu cha Mormoni kilichangia sehemu kubwa katika uongofu wao.13 Thuso anakumbuka, “Nilianza kusoma Kitabu cha Mormoni … kila nilipopata nafasi, nyumbani, shuleni, kila mahali.”14
Oratile aliletwa kwenye injili kwa sababu ya mfano wa rafiki zake. Anaelezea: “Walionekana kubadilika ghafla. … Nilidhani … ilitokana na kile kitabu kidogo … walichoanza kukibeba kila mahali … shuleni. Niliweza kuona jinsi walivyokuwa wamegeuka kuwa watu wazuri. … [Mimi] pia nilitaka kubadilika.”15
Wavulana hawa wote 12 walikusanywa na kubatizwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya kila mmoja. Kila mmoja alikuwa muumini pekee wa Kanisa katika familia yake. Lakini walisaidiwa na familia yao ya Kanisa, ikimjumuisha Rais Rakwela,16 rais wao wa tawi; Mzee na Dada Taylor,17 wamisionari wanandoa; na waumini wengine wa tawi.
Kaka Junior,18 kiongozi wa akidi, aliwaalika wavulana hawa nyumbani kwake kila jumapili mchana na kuwashauri. Wavulana hawa walijifunza maandiko pamoja na kuwa na jioni ya familia mara kwa mara.
Kaka Junior aliwachukua kwenda kuwatembelea waumini, watu waliokuwa wakifundishwa na wamisionari, na yeyote yule ambaye alihitaji kutembelewa. Wavulana wote 12 walipanda nyuma ya gari la Kaka Junior. Aliwapeleka katika nyumba tofauti wakiwa wawili au watatu na kuwachukua baadaye.
Japokuwa wavulana hawa walikuwa tu wanajifunza kuhusu injili na hawakuhisi kwamba walijua mengi, Kaka Junior aliwaambia washiriki jambo moja au mawili waliyoyafahamu pamoja na watu waliowatembelea. Wavulana hawa wenye ukuhani walifundisha, walisali, na kusaidia kulichunga Kanisa.19 Walitimiza majukumu yao ya ukuhani na kupata uzoefu wa shangwe inayotokana na kuhudumu.
Andre alisema, “Tulicheza pamoja, tulicheka pamoja, tulilia pamoja, na tukawa ndugu.”20 Kwa hakika, wao hujiita “Kundi la Ndugu.”
Pamoja waliweka lengo la kuhudumu misheni. Kwa kuwa walikuwa waumini pekee katika familia zao, walikuwa na changamoto nyingi za kushinda, lakini walisaidiana kukabiliana nazo.
Mmoja baada ya mwingine, wavulana hao walipokea wito wa misheni. Wale walioenda kwanza waliandika barua kwenda nyumbani kwa wale waliokuwa wakijitayarisha, wakishiriki uzoefu na kuwatia moyo waweze kuhudumu. Kumi na mmoja kati ya wavula wale walihudumu misheni.
Wavulana hawa walishiriki injili pamoja na familia zao. Akina mama, dada, kaka, marafiki, pamoja na watu waliowafundisha katika misheni zao, waliongolewa na kubatizwa. Miujiza ilifanyika na maisha ya watu wengi yalibarikiwa.
Naona baadhi yenu mkifikiria kwamba pengine muujiza kama huu unaweza tu kutokea katika mahali kama Afrika, shamba lenye rutuba ambapo ukusanyaji wa Israeli unaharakishwa. Hata hivyo, ninashuhudia kwamba kanuni zilizotumika katika Tawi la Mochudi ni za kweli mahali popote. Popote ulipo, akidi yako inaweza kukua kupitia kuamshwa na kushiriki injili. Wakati mfuasi mmoja anapomtafuta rafiki, mmoja anaweza kuwa wawili. Wawili wanaweza kuwa wanne. Wanne wanaweza kuwa wanane. Na wanane wanaweza kuwa kumi na wawili. Matawi yanaweza kuwa Kata.
Mwokozi alifundisha, “Walipo wawili au watatu [au zaidi] waliokusanyika pamoja katika jina langu, … tazama, mimi nitakuwa katikati yao.”21 Baba wa Mbinguni anatayarisha akili na mioyo ya watu walio karibu nasi. Tunaweza kufuata misukumo, kunyosha mkono wa urafiki, kushiriki ukweli, kualika wengine kusoma Kitabu cha Mormoni, na kuwapenda na kuwasaidia wanapokuja kumfahamu Mwokozi wetu.
Imepita karibu miaka 10 tangu Kundi hili la Ndugu kutoka Mochudi walipoanza safari yao pamoja, na wangali bado kundi la ndugu.
Katlego alisema, “Twaweza kuwa tumetenganishwa na umbali, lakini bado tupo kwa ajili ya kila mmoja.”22
Ni ombi langu kwamba tutakubali mwaliko wa Bwana wa kuunganishwa Naye katika akidi zetu za ukuhani ili kwamba kila akidi iweze kuwa mahali pa kuwepo, mahali pa kukusanyika, na mahali panapokua.
Yesu Kristo ni Mwokozi wetu, na hii ni kazi Yake. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.