2010–2019
Jenga Ngome ya Mambo ya Kiroho na ya Ulinzi
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Jenga Ngome ya Mambo ya Kiroho na ya Ulinzi

Tunapoishi injili ya Yesu Kristo, tunapotumia upatanisho wa Mwokozi na kusonga mbele kwa imani, tunaimarishwa dhidi ya hila za adui.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, wakati mkutano huu mkuu unakaribia hitimisho, Ninatoa shukrani kwa Baba yetu aliye Mbinguni kwa ushauri, kweli, na ufunuo uliotolewa kwenye mimbari hii kipindi cha siku mbili zilizopita. Tumefundishwa na watumishi wa Mungu walioitwa kuzungumza maneno yake matakatifu. Bwana ametukumbusha katika ufunuo wa siku za mwisho, “Iwe kwa sauti yangu mwenyewe au … sauti za watumishi wangu, yote ni sawa.”1

Nikiangalia mkusanyiko huu wa Watakatifu na kupata picha ya waumini wanaoangalia mkutano mkuu ulimwenguni kote, ninafikiria juu ya mkusanyiko katika kitabu cha Mormoni wakati Yesu Kristo alipowatokea Wanefi baada ya Kusulubiwa Kwake. Aliwafundisha injili na kisha aliwatia moyo, “Nendeni nyumbani kwenu, na mfikirie vitu ambavyo nimesema, na mwulize kutoka kwa Baba, katika jina langu, ili muweze kufahamu.”22

“Nendeni nyumbani kwenu, na mfikirie” ni hatua inayofuata katika kuweka moyoni maneno ya manabii na viongozi wa Kanisa yaliyozungumzwa mahala hapa patakatifu. Nyumba zilizojikita katika kristo ni ngome kwa ajili ya ufalme wa Mungu duniani katika siku ambayo, kama ilivyotabiriwa, ibilisi “atavuma mioyoni mwa watoto wa watu, na awavuruge wakasirikie yale ambayo ni mema.”3

Watu wamejenga ngome kote katika historia kujilinda dhidi ya adui. Mara kwa mara ngome hizo zilikuwa na mnara wa mlinzi ambako walinzi wa usiku—kama manabii—walionya juu ya tishio la majeshi na mashambulizi yanayokuja.

Picha
Thomas Rasband

Katika nyakati za waasisi wa mwanzo wa Utah, babu wa babu yangu Thomas Rasband na familia yake walikuwa baadhi ya walowezi wa kwanza kuingia Bonde la Heber kwenye Milima ya kupendeza ya Wasatch huko Utah..

Mnamo mwaka 1859, Thomas alisaidia kujenga ngome ya Heber, ikijengwa kwa ajili ya ulinzi wao. Lilikuwa jengo la kawaida la magogo, yaliyopangwa moja karibu na lingine, kutengeneza umbo la mzingo wa ngome. Mabanda ya magogo yalijengwa ndani ya ngome yakikingwa na ukuta huo. Jengo lilitoa vyote usalama na kinga kwa ajili ya familia hizo za waasisi wakati wakijiandaa kuwa wenyeji na wakimwabudu Bwana.

Picha
Ngome ya waanzilishi

Ndivyo ilivyo kwetu. Nyumba zetu ni ngome dhidi ya uovu wa ulimwengu. Katika nyumba zetu tunakuja kwa Kristo kwa kujifunza kufuata amri zake, kwa kujifunza maandiko na kusali pamoja, na kwa kusaidiana sisi wenyewe kubaki kwenye njia ya agano. Msisitizo mpya juu ya mafunzo binafsi na ya kifamilia ndani ya nyumba kupitia mtaala wa Njoo, Unifuate umebuniwa “kufanya uongofu wetu kuwa wa kina na kutusaidia kuwa zaidi kama Yesu Kristo.”4 Katika kufanya hivyo tutakuwa kile Paulo alichokiita “viumbe wapya”5 mioyo yetu na nafsi zikiwiana na Mungu. Tunahitaji uimara huo kukabiliana na kukwepa mashambulizi ya adui.

Tunapoishi kwa kujitolea kulikojengwa na imani katika Yesu Kristo, tutahisi uwepo wa amani wa Roho Mtakatifu, anayetuongoza kwenye ukweli, anayetupa msukumo kuishi kwa kustahili baraka za Bwana, na anayetoa ushahidi kwamba Mungu anaishi na anatupenda. Yote haya katika ngome ya nyumba zetu. Lakini kumbukeni, nyumba zetu ni zenye nguvu tu kulingana na nguvu za kiroho za kila mmoja wetu ndani ya kuta.

Rais Russell M. Nelson amefundisha, “Katika siku zijazo, haitawezekama kuendelea kuishi kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi wa mara kwa mara wa Roho Mtakatifu.”6 Kama nabii wa Mungu anayeishi, mwonaji, na mfunuzi katika siku hii, mlinzi wa usiku kwenye mnara wa ngome yetu, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, anaona jinsi adui anavyotusogelea.

Akina kaka na akina dada, tunapigana vita na Shetani kwa ajili ya nafsi za binadamu. Mistari ya vita ilichorwa katika maisha yetu kabla ya kuja duniani. Shetani na theluthi moja ya watoto wa Baba yetu wa Mbinguni waligeuka upande kutoka kwenye ahadi Zake za kuinuliwa. Tangu wakati huo, majeshi ya adui yamekuwa yakipigana na wenye imani waliochagua mpango wa Baba.

Shetani anajua siku zake zimekwisha na kwamba muda unazidi kupungua. Akiwa na ustadi na werevu kama alivyo, hataweza kushinda. Hata hivyo, vita yake kwa kila moja ya nafsi zetu inaendelea vikali.

Kwa usalama wetu lazima tujenge ngome ya Mambo ya Kiroho na ya ulinzi kwa ajili ya nafsi zetu wenyewe, ngome ambayo haitaweza kupenywa na mwovu.

Shetani ni nyoka mwerevu, ananyemelea kwenye akili zetu na mioyo yetu wakati ulinzi wetu upo chini, tunapokabiliwa na kukata tamaa, au kupoteza tumaini. Anatulaghai na ubembelezaji, ahadi nyepesi, faraja, au hali ya juu ya muda tunapokuwa chini. Anahalalisha kiburi, ukatili, kukosa uaminifu, kutoridhika, na ukosefu wa maadili, na baada ya muda tunaweza “kufa ganzi”7 Roho anaweza kutuacha. “Na kwa hivyo ibilisi anadanganya nafsi zao, na anawaongoza mbali kwa uangalifu chini kwenye jehanamu.”8

Kinyume chake, mara kwa mara tunamhisi Roho kwa nguvu sana tunapoimba sifa kwa Mungu kwa maneno kama haya:

Ngome imara ni Mungu wetu,

Mnara wa nguvu kamwe haushindwi.

Msaidizi mwenye nguvu ni Mungu wetu.

Juu ya magonjwa katika maisha ana shinda.9

Tunapojenga ngome yenye nguvu za kiroho, tunaweza kuepuka ukaribiaji wa adui, tukimgeuzia migongo yetu, na kuhisi amani ya Roho. Tunaweza kufuata mfano wa Bwana na Mwokozi wetu, ambaye, wakati alipojaribiwa nyikani, alisema, “Rudi nyuma yangu Shetani.”10 Kila mmoja wetu anatakiwa kujifunza kwa uzoefu wa maisha jinsi ya kufanya hivyo.

Lengo hilo la haki linaelezwa vyema katika Kitabu cha Mormoni wakati Kapteni Moroni alipowaandaa Wanefi kukabiliana na mashambulizi kutoka kwa mlaghai, katili, na mpenda madaraka Amalikia. Moroni alijenga ngome kuwalinda Wanefi “Ili waweze kuishi katika Bwana Mungu wao, na kwamba wangeweza kushikilia ile ambayo iliitwa na maadui zao imani ya Wakristo.”11 Moroni alikuwa imara katika imani ya Kristo,”12 na alikuwa mwaminifu “katika kutii amri za Mungu … na kuzuia uovu.”13

Wakati Walamani walipokuja kupigana, walishangazwa na maandalizi ya Wanefi, na walishindwa. Wanefi walimshukuru “Bwana Mungu Wao, kwa sababu ya nguvu yake isiyo na kifani kwa kuwakomboa kutoka mikono ya maadui zao.”14 Walikuwa wamejenga ngome kwa ajili ya ulinzi upande wa nje, na walikuwa wamejenga imani katika Bwana Yesu Kristo upande wa ndani—kwa kina katika nafsi zao.

Ni zipi baadhi ya njia tunazoweza kujiimarisha wenyewe katika nyakati za matatizo, ili tuweze kuwa “vyombo katika mikono ya Mungu kuleta kazi hii kuu”?15 acha tutazame kwenye maandiko.

Sisi ni watiifu. Bwana alimwamuru Baba Lehi kuwarudisha wanawe Yerusalemu “kutafuta kumbukumbu, na kuzileta nyikani.”16 Lehi hakuuliza; hakushangaa kwa nini au kwa jinsi gani. Wala Nefi, ambaye alijibu, “Nitaenda na kutenda vitu ambavyo Bwana ameamuru .”17

Je tunatenda kwa utayari wa kutii wa Nefi? Au tuko zaidi kwenye kutia shaka amri za Mungu kama walivyofanya kaka zake Nefi, ambao kukosa kwao imani hatimaye kuliwageuza mbali na Bwana? Utiifu, ukionyeshwa kwa “utakatifu wa moyo,”18 ndicho hasa Bwana anakitaka kutoka kwetu.

Tunamwamini Bwana, aliyemwambia Yoshua alipokuwa akijiandaa kuwaongoza Waisraeli kwenye nchi ya ahadi, “Uwe hodari na … moyo wa ushujaa; usiogope, wala usifadhaike; kwani Bwana Mungu wako yupo pamoja nawe kokote uendako.”19 Yoshua aliamini maneno hayo na aliwashauri watu, “Jitakaseni wenyewe kwani kesho Bwana atafanya maajabu miongoni mwenu.”20 Bwana aliyatenganisha maji ya Yordani, na miaka 40 ya kutangatanga kwa Waisraeli nyikani ilifika kikomo.

Tunasimamia ukweli, kama alivyofanya nabii Abinadi katika Kitabu cha Mormoni. Alikamatwa, akaletwa mbele ya Mfalme Nuhu na makuhani wake waovu, Abinadi alifundisha Amri Kumi na alihubiri kwa nguvu kwamba Kristo “angeshuka miongoni mwa watoto wa watu, na … kuwakomboa watu wake.”21 Kisha, kwa imani ya kina ndani yake, alitangaza, “Ee Mungu, pokea nafsi yangu,”22 na Abinadi “aliteseka kifo kwa moto.”23

Picha
Hekalu la Roma Italia

Tunafanya na kurudia tena maagano yetu kwa kupokea sakramenti na kwa kuabudu hekaluni. Sakramenti ni kiini cha ibada yetu ya Jumapili, ambapo tunapokea ahadi ya “daima kuwa na Roho wake pamoja na [sisi].”24 pamoja na ibada hiyo takatifu tunaahidi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo, kumfuata, na kuchukua wajibu wetu katika kazi hii takatifu kama alivyofanya. Hekaluni, tunaweza “kuweka kando vitu vya ulimwengu huu”25 na kuhisi uwepo wa Bwana na amani ipitayo uwezo wa kibinadamu. Tunaweza kufokasi juu ya mababu zetu, familia zetu, na uzima wa milele katika uwepo wa Baba. Ndiyo maana Rais Nelson alisema hivi karibuni huko Roma, “Mema ambayo yatakuja kutokana na hekalu hili ni yasiyo pimika kwa ukubwa au wingi.”26

Hatuna budi kuwa na uadilifu katika yote ambayo tunayafanya. Hatuna budi kukuza utambuzi na nidhamu ili kwamba tusiwe kila mara tunaamua kipi ni chema na kipi si chema. Hatuna budi kuweka moyoni maneno ya Petro, Mtume wa mwanzo wa Kanisa ambaye alionya, “ Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.,”27

Tunapo imarisha kwa bidii ngome zetu, tunakuwa kama Yesu Kristo, kama wafuasi wake wa kweli, pamoja na nafsi zetu katika ulinzi wake.

Ushuhuda wako wa Yesu Kristo ndiyo ngome yako binafsi, ulinzi kwa ajili ya nafsi yako. Wakati babu yangu na waasisi wenzake walipojenga ngome ya Heber, waliweka gogo moja kwa wakati mmoja mpaka ngome ilipokuwa na “umbo imara kwa pamoja”28 na walikuwa wamelindwa. Ndivyo ilivyo kwa ushuhuda. hatua kwa hatua tunapata ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu anapozungumza na roho zetu wenyewe, akifundisha “ukweli katika sehemu za ndani.”29 Tunapoishi injili ya Yesu Kristo, tunapotumia upatanisho wa Mwokozi na kusonga mbele kwa imani, bila woga, tunaimarishwa dhidi ya hila za adui. Shuhuda zetu zinatuunganisha na mbingu, na tuna barikiwa na “ukweli wa vitu vyote.”30 Na, kama waasisi walivyolindwa na ngome, tumezingirwa kiusalama katika mikono ya upendo ya Mwokozi.

Nabii Etheri alifundisha, “Kwa hivyo, yeyote aaminiye katika Mungu angeweza kwa uhakika kutumaini ulimwengu bora, ndio, hata mahali katika mkono wa kulia wa Mungu, tumaini ambalo huja kutokana na imani, hutengeneza nanga kwa roho za watu, ambayo ingewafanya kuwa imara na thabiti, wakizidi sana kutenda kazi njema, wakiongozwa kumtukuza Mungu.”31

Kaka na dada zangu wapendwa, Nawaacheni na baraka zangu msonge mbele kwa kujiamini katika Bwana na injili Yake. Wekeni mikono yenu kuwazunguka wale wanao jikwaa na, kwa nguvu za Roho ndani yenu, waongozeni kwa upendo kurudi kwenye ngome ya mambo ya kiroho na ya ulinzi. Tafuteni “kuwa kama Yesu”32 katika yale yote mnayofanya; epukeni uovu na majaribu; tubuni, kama tulivyoonywa jana na nabii wetu mpendwa; kuweni wakweli katika moyo; kuweni waadilifu na wasafi; onesheni huruma na hisani; na mpendeni Bwana Mungu wenu kwa kujitolea kwa mfuasi wa kweli.

Ushuhuda wetu wa injili ya Yesu Kristo, nyumba zetu, familia zetu na uumini wetu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho utakuwa ngome yetu binafsi ya ulinzi kutuzunguka na kutukinga kutokana na nguvu ya mwovu. Juu ya hili natoa ushahidi wangu wa dhati katika jina la Bwana na Mwokozi wetu, hata Yesu Kristo, amina.

Chapisha