Injili ya Kweli, Safi, na Rahisi ya Yesu Kristo.
Kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu ni msingi wa mafundisho ya kuhudumu; kujifunza kunakolenga-nyumbani, na kusaidiwa na Kanisa; Ibada ya kiroho ya siku ya Sabato; na kazi ya wokovu.
Kaka na dada zangu wapendwa, ni vigumu kwangu kuamini kwamba ilikuwa miaka 71 iliyopita, mnamo mwaka 1948, kwamba nilikuwa mmisionari kule Uingereza na miaka 44 iliyopita kwamba mke wangu, Barbara na mimi tulikwenda Kanada na familia yetu nilipokuwa rais wa Misheni ya Kanada Toronto. Nikiwa nahudumu huko Aprili 1976, niliitwa kwenye Akidi ya Kwanza ya Sabini, na bila kutarajia mwaka 1985, niliitwa kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Tofauti na miito yangu ya awali ambayo ilijumuisha kupumzishwa baadaye, kupumzishwa kwangu kutoka wito wangu wa Kumi na Wawili sio chaguo bora hivi sasa; hata hivyo, ninaomba kwamba siku hiyo ije tu baada ya kumaliza kazi yote ambayo Bwana ameniita kufanya.
Katika kufikiria kuhusu miaka yangu 43 iliyopita ya utumishi kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka na fursa niliyokuwa nayo ya kuhudumu kwa watoto wa Baba wa Mbinguni, nimekuja kugundua kikamilifu zaidi kwamba Yeye anataka watoto Wake wote kupata amani, shangwe, na furaha katika maisha yao.
Nabii Lehi alifundisha, “Wanaume [na wanawake] wapo, ili wapate shangwe.”1 Kuna sababu nyingi ambazo kwazo amani, shangwe, na furaha zinaweza kutuepuka katika maisha haya, ikiwa ni pamoja na umasikini, vita, majanga ya asili, na vikwazo visivyotarajiwa katika ajira, afya na mahusiano ya familia.
Lakini japo hatuwezi kuzuia misukumo hiyo kutoka nje ambayo inaathiri maisha yetu hapa duniani, tunapojitahidi kuwa wafuasi watiifu wa Bwana Yesu Kristo, tunaweza kupata amani, shangwe, na furaha bila kujali matatizo ya dunia yanayotusumbua.
Mmoja wa watoto wangu wakati mmoja alisema, “Baba, najiuliza iwapo nitaweza kufanikiwa.” Nikajibu, “Yote anayoyataka Baba wa Mbinguni kutoka kwetu ni kufanya vizuri zaidi kadiri tunayoweza kila siku.” Akina kaka na akina dada, fanya vizuri zaidi kadiri unavyoweza kila siku, na kabla hujatambua, utakuja kugundua kwamba Baba yako wa Mbinguni Anakujua na kwamba Anakupenda. Na unapojua hilo—unapojua kwa uhalisia—maisha yako yatakuwa na dhumuni halisi na maana na utajazwa na furaha na amani.
Kama Nuru ya Ulimwengu, Mwokozi alisema, “Kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani .”2
“Yesu Kristo ndilo jina ambalo limetolewa na Baba, na hakuna jina lingine lililotolewa ambalo kwa hilo [sisi] tunaweza kuokolewa;
“Kwa hiyo, wanaume wote [na wanawake] yawalazimu kujichukulia juu yao jina ambalo limetolewa na Baba.”3
Maandiko yanatufundisha kuwa Ibilisi anataka kuwaongoza watu gizani. Kila juhudi yake ni kuzima nuru na ukweli wa Yesu Kristo na injili Yake. Kama Lehi alivyowafundisha watoto wake, ibilisi “anataka wanadamu wote wawe na dhiki kama yeye.”4 Kama “kazi na … utukufu” wa Baba wa Mbinguni ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa [wanaume na wanawake],”.5 “kazi” ya Ibilisi ni kuleta taabu na shida zisizo na mwisho kwa watoto wa Mungu. Dhambi na uasi hufifisha nuru ya Kristo katika maisha yetu. Hii ndiyo sababu hitaji letu ni kukaa katika Nuru ya Kristo, ambayo inaleta amani, shangwe, na furaha.
Miezi 18 iliyopita, Bwana amewapa msukumo Manabii na Mitume Wake kutekeleza baadhi ya marekebisho mazuri. Hata hivyo, nina wasiwasi kwamba malengo ya kiroho ya marekebisho haya yanaweza kupotea katika msisimko kuhusu mabadiliko yenyewe.
Joseph F. Smith alisema: “Injili ya kweli, safi na rahisi ya Yesu Kristo imerejeshwa. Tunawajibika kwa kuitunza hapa duniani.”6 Aliongeza kwamba injili ya kweli, safi, na rahisi ni “mafundisho ya kuokoa ya Kristo.”7
Katika Makala ya Imani, Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba “kwa njia ya Upatanisho wa Kristo, wanadamu wote wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili.”8
Kanuni za kwanza za injili ni imani katika Bwana Yesu Kristo, toba, ubatizo, kipawa cha Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho. Kaka wa Joseph Hyrum alifundisha: “Zihubiri tena [na tena]: utaona kwamba siku baada ya siku mawazo mapya na nuru ya ziada kuzihusu itafunuliwa kwako. Unaweza kuongeza juu yake … ili kuzielewa kwa uwazi. Kisha utaweza kuzifanya kueleweka wazi zaidi kwa wale unaowafundisha.”9
Njia bora zaidi za sisi kuona madhumuni ya kiroho ya Kanisa ni kuishi mafundisho ya kweli, safi, na rahisi ya Kristo na pia kutekeleza amri mbili kuu za Mwokozi: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote. … Nawe mpende jirani yako kama nafsi yako.”10
Utiifu wa amri hizo mbili unaleta njia ya kupata amani na furaha zaidi. Tunapompenda na kumtumikia Bwana na kuwapenda na kuwatumikia jirani zetu, kwa uhalisia tutahisi furaha zaidi ambayo huja kwetu kwa njia bora zaidi.
Kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu ni msingi wa mafundisho ya kuhudumu; kujifunza kunakolenga-nyumbani, kunakosaidiwa na Kanisa; Ibada ya kiroho ya siku ya Sabato; na kazi ya wokovu kwa pande mbili za pazia inayopata msaada katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama na akidi za wazee. mambo yote haya yamejikita juu ya amri takatifu ya kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu. Je, kunaweza kuwa na kitu muhimu zaidi, cha msingi zaidi, na rahisi zaidi kuliko hicho?
Kuishi mpango wa injili wa kweli, safi, na rahisi kutatupa muda zaidi wa kutembelea wajane, wagane, yatima, wapweke, wagonjwa, na masikini. Tutakuwa na amani, shangwe, na furaha katika maisha yetu wakati tunapomtumikia Bwana na jirani zetu.
Mabadiliko ya siku ya Sabato ambayo yanasisitiza kujifunza injili na kusoma kulikolenga nyumbani, kunakosaidiwa na Kanisa ni fursa ya kufanya upya roho yetu na kujitolea kwetu kwa Mungu ndani ya kuta za nyumba zetu. Ni nini kingeweza kuwa rahisi zaidi, cha msingi, na cha kupendeza? Akina kaka na akina dada, je mnaweza kuona kwamba kujifunza na kufundisha injili katika familia zetu ni njia muhimu ya kuwa na shangwe na furaha katika maisha yetu?
Akiongelea juu ya Sabato, Mwokozi alisema, “Kwani amini hii ndiyo siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutoka katika kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu Sana.”11 Aliongeza, “Ili shangwe yako iweze kuwa timilifu … [kupitia] kufurahi na sala … [mnapaswa] kufanya mambo haya kwa shukrani, pamoja na mioyo na nyuso zenye furaha … [na] kwa moyo wenye furaha na uso mchangamfu.”12
Tafadhali zingatia maneno muhimu katika ufunuo huu: shangwe, kushangilia, shukrani, mioyo yenye furaha, furaha, moyo, na uso mchangamfu. Inaonekana kwangu kama kuitii siku ya Sabato kunapaswa kuleta tabasamu katika nyuso zetu.
Tunapohudumia kwa hali ya juu na takatifu, tafadhali fikiria ilivyo muhimu kiasi gani kwamba tunamsalimia kila mtu anayekuja kwenye mikutano yetu ya Kanisa, hasa waumini wapya na wageni. Sote tunapaswa kufurahia kuimba nyimbo na kusikiliza kwa makini maneno ya sala ya sakramenti kwa moyo mkunjufu na akili kunjufu.
Shuhuda za imani katika mikutano yetu ya kufunga na ushuhuda inaongozwa na washiriki wa uaskofu, ambao wanashiriki ushuhuda mfupi unaolenga kwenye mpango wa furaha na injili ya kweli, halisi, na rahisi ya Kristo. Wengine wote wanapaswa kufuata mfano huo. Tunapaswa kukumbuka kwamba kuna sehemu zingine sahihi za kusimulia hadithi au kushiriki habari za safari. Tunapozifanya shuhuda zetu kuwa rahisi na zinazolenga juu ya injili ya Kristo, Yeye atatoa upya wa kiroho pale tunaposhiriki shuhuda zetu pamoja na wengine.
Kuhudumu kwa ufanisi kunatazamwa vizuri kupitia lensi iliyofokasi kwenye kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu. Ilielezwa kiurahisi, tunahudumu kwa sababu tunampenda Baba yetu wa Mbinguni na watoto Wake. Juhudi zetu za kuhudumu zitafanikiwa zaidi kama tutafanya huduma kuwa rahisi. Furaha zaidi inatoka katika mambo rahisi ya maisha, hivyo tunahitaji kuwa waangalifu kutofikiria kwamba kuna mengi ya kuongezwa kwenye marekebisho tuliyoyapokea ili kujenga imani na shuhuda imara katika mioyo ya watoto wa Mungu.
Hebu tuache kufanya mambo kuwa magumu kwa mikutano ya ziada, matarajio, au mahitaji ya ziada. Rahisisha. Ni katika urahisi huo kwamba utapata amani, shangwe, na furaha niliyokuwa nikiizungumzia.
Kwa miaka mingi malengo ya uongozi wa Kanisa, kama ilivyoelezwa katika Kitabu Kitabu cha Mwongozo 2 ni matokeo ambayo ni wazi na rahisi, kutoka kwayo nanukuu:
“Viongozi wanamuhimiza kila muumini kupokea ibada zote muhimu za ukuhani, kutunza maagano yanayohusiana nazo, na kuwa mwenye kustahili kuinuliwa na uzima wa milele. …
“Watu wazima: Muhimizeni kila mtu mzima awe mwema kustahili kupokea ibada za hekaluni. Wafundisheni watu wazima wote kuwatambua mababu zao na kufanya ibada za hekalu kwa niaba yao.
“Vijana: Saidieni kumuandaa kila mvulana kupokea ukuhani wa Melkizedeki, kupokea ibada za hekaluni, na kustahili kutumikia misheni. Saidieni kumuandaa kila msichana kustahili kufanya na kushika maagano matakatifu na kupokea ibada za hekaluni. Waimarisheni vijana kupitia ushiriki katika kazi zenye maana.
“Waumini wote: Wasaidieni viongozi wa ukuhani na viongozi wa vikundi saidizi, mabaraza ya kata, kata na wamisionari wa muda wote, na waumini kufanya kazi kwa kushirikiana katika jitihada za kuokoa watu binafsi, kuimarisha familia na vitengo vya Kanisa, kuongeza shughuli za kikuhani, na kukusanya Israeli kupitia uongofu, uhifadhi, na kurudisha wasioshiriki kikamilifu. Wafundisheni waumini kujitafutia wenyewe na familia zao na kuwasaidia maskini na wenye uhitaji katika njia ya Bwana.”13
Utumishi wangu Kanisani umenibariki kwa uzoefu mkubwa na maalumu wa kiroho. Mimi ni shahidi kwamba Bwana analiongoza Kanisa Lake kukamilisha malengo Yake. Nimepokea muongozo mtakatifu zaidi ya uwezo wangu. Furaha ya kuishi injili kwangu imekuwa na kiini kwenye mafundisho ya kweli, safi, na rahisi ya Yesu Kristo.
Nimehudumu chini ya funguo na mwongozo wa manabii na Marais sita wa Kanisa, kuanzia Spencer W. Kimball hadi Russell M. Nelson. Ninashuhudia kwamba kila mmoja wao alikuwa na ni nabii aliyechaguliwa na Mungu. Wametufundisha kanuni muhimu kuhusu Kanisa na injili na mafundisho ya Kristo. Rais Nelson anaipeleka kazi ya Bwana mbele kwa kasi kubwa. Ninasema “kwa kasi” kwa sababu ndiye pekee kati ya Mitume ambao wana umri mkubwa kuliko mimi, na ninakuwa na wakati mgumu kwenda naye sambamba! Mimi ni shuhuda kwamba funguo za ukuhani na roho ya kinabii ya Mungu vipo naye. Rais Nelson anafundisha injili ya kweli, safi, na rahisi ya Yesu Kristo. Ninatoa ushuhuda wangu kwamba Yesu ni Kristo na hili ni Kanisa Lake—juu yake ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.