Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Wazuri Zaidi
Wekeni fokasi yenu ya toba ya kila siku kuwa muhimu kwenye maisha yenu kwamba muweze kutumia ukuhani kwa nguvu kubwa zaidi kuliko hapo kabla.
Kaka zangu wapendwa, inavutia kutazama juu ya mkusanyiko huu mkubwa wa batalioni ya Bwana ya wenye ukuhani. Jeshi lenye nguvu kiasi gani kwa ajili ya wema! Tunawapenda. Tunawaombea. Na tuna shukrani kubwa kwa ajili yenu.
Hivi karibuni nimejikuta nikivutwa kwenye maelekezo ya Bwana yaliyotolewa kupitia Nabii Joseph Smith: “Usiseme lolote bali toba kwa kizazi hiki.”1 Tamko hili limerudiwa mara nyingi kote katika maandiko.2 linachochea swali la kawaida: “Je kila mmoja anahitaji kutubu?” Jibu ni ndiyo.
Watu wengi hufikiria toba kama adhabu—jambo la kuepukwa isipokuwa katika hali za hatari sana. Lakini hisia hii ya kutaabisha husababishwa na Shetani. Yeye hujaribu kutuzuia kutazama kwa Yesu Kristo,3 ambaye anasimama na mikono iliyonyooshwa,4 kwa tumaini na utayari wa kuponya, kusamehe, kusafisha, kuimarisha, na kututakasa sisi.
Neno la toba katika Agano Jipya la Kigiriki ni metanoeo. Kitangulizi meta humaanisha “badiliko.” Kitamatisho ‑noeo kinahusiana na maneno ya Kigiriki ambayo humaanisha “akili,” “ufahamu,” “roho,” na “pumzi.”5
Hivyo, Yesu anapoomba mimi na wewe “tutubu,”6 Anatualika kubadili akili zetu, ufahamu wetu, roho zetu—hata jinsi tunavyopumua. Anatuomba tubadili jinsi tunavyopenda, tunavyofikiri, tunavyotumikia, tunavyotumia muda wetu, tunavyowatendea wake zetu, tunavyowafunza watoto wetu, na hata jinsi tunavyoitunza miili yetu.
Hakuna kinachotoa uhuru zaidi, cha kiungwana zaidi, au cha muhimu zaidi kwa ukuaji wetu binafsi kuliko ilivyo fokasi ya mazoea ya kila siku kwenye toba. Toba siyo tukio; ni mchakato. Ni muhimu kwa furaha na amani ya akili. Inapoambatana na imani, toba hufungua kufikia kwetu kwenye nguvu za Upatanisho wa Yesu Kristo.7
Bila kujali unatembea kwa bidii kwenye njia ya agano, umeteleza au kutoka kwenye njia ya agano, au huwezi hata kuona njia ya agano kutokea ulipo sasa, ninakusihi utubu. Pata uzoefu wa nguvu ya kuimarisha ya toba ya kila siku—ya kufanya vizuri zaidi na kuwa wazuri zaidi kila siku.
Tunapochagua kutubu, tunachagua kubadilika! Tunamruhusu Mwokozi kutubadilisha kuwa toleo zuri zaidi la sisi wenyewe. Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye.8 Tunapochagua kutubu, tunachagua kuwa zaidi kama Yesu Kristo!9
Akina kaka, tunahitaji kufanya vizuri zaidi na kuwa wazuri zaidi kwa sababu tuko vitani. Vita dhidi ya dhambi ni halisi. Mjaribu anazidisha juhudi zake mara tatu zaidi ili kuvuruga shuhuda na kukwamisha kazi ya Bwana. Anawalinda watumishi wake kwa silaha zenye nguvu ili kutuzuia kupata shangwe na upendo wa Bwana.10
Toba ni muhimu katika kuzuia huzuni iliyoletwa na mitego ya mjaribu. Bwana hatarajii ukamilifu kutoka kwetu kwenye hatua hii katika ukuaji wetu wa milele. Lakini anatarajia sisi tuongezeke katika kuwa watakatifu. Toba ya kila siku ndiyo njia ya kuelekea utakatifu, na utakatifu huleta nguvu. Utakatifu binafsi unaweza kutufanya vyombo vyenye nguvu mikononi mwa Mungu. Toba yetu—utakatifu wetu—vitatuwezesha sisi kusaidia katika kukusanya Israeli.
Bwana alimfundisha Joseph Smith “kwamba haki za ukuhani zimeungana na hazitenganishwi na nguvu za mbinguni, na kwamba nguvu za mbinguni haziwezi kudhibitiwa wala kutawaliwa isipokuwa tu kwa kanuni za haki.”11
Tunajua nini kitatupatia kufikia kwa kiasi kikubwa nguvu za mbinguni. Tunajua pia nini kitazuia ukuaji wetu—kile tunachopaswa kuacha kufanya ili kuongeza kufikia kwetu nguvu za mbinguni. Akina kaka, kwa sala tafuta kuelewa kile kinachosimama kwenye njia yako ya toba. Tambua kile kinachokuzuia kutubu. Na kisha, badilika! Tubu! Sote tunaweza kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.12
Kuna njia maalumu ambazo kwazo tunaweza kujiboresha. Moja ni jinsi tunavyoitunza miili yetu. Ninasimama kwa heshima na hofu ya muujiza wa mwili wa mwanadamu. Ni uumbaji wa ajabu, muhimu kwa ukuaji wetu polepole kuelekea hatma ya uwezekano wetu mtakatifu. Hatuwezi kukua bila mwili. Katika kutupatia zawadi ya mwili, Mungu ameturuhusu kuchukua hatua muhimu kuelekea kuwa zaidi kama Yeye.
Shetani anaelewa hili. Anaghadhabika kwenye ukweli kwamba ukengeufu wake wa maisha kabla ya kuja duniani ulimnyima ustahiki wa kudumu wa fursa hii, ukimuacha kwenye hali ya kudumu ya wivu na chuki. Hivyo mengi, kama si yote, ya majaribu anayoweka katika njia yetu hutusababisha kutumia vibaya miili yetu au miili ya wengine. Kwa sababu Shetani ana huzuni kwa kukosa mwili, anataka tuwe na huzuni kwa sababu ya miili yetu.13
Mwili wako ni hekalu lako binafsi, lililojengwa kuipa hifadhi roho yako ya milele.14 Utunzaji wako wa hekalu hilo ni muhimu. Sasa, ninawauliza, akina kaka, je, mnavutiwa zaidi katika kuvaa na kuiweka nadhifu miili yenu ili kuvutia ulimwengu kuliko mnavyofanya kumpendeza Mungu? Jibu lenu linatuma ujumbe wa moja kwa moja Kwake kuhusu hisia zenu kuhusiana na zawadi Yake kuu kwenu. Katika unyenyekevu huu kwa miili yetu, akina kaka, nafikiri tunaweza kufanya vizuri zaidi na kuwa wazuri zaidi.
Njia nyingine tunayoweza kufanya vizuri zaidi na kuwa wazuri zaidi ni jinsi tunavyowaheshimu wanawake katika maisha yetu, tukianza na wake zetu na mabinti zetu, mama zetu na dada zetu.15
Miezi iliyopita, nilipokea barua ya kuvunjika moyo kutoka kwa dada mpendwa. Aliandika: “[Mimi na binti zangu] tunahisi tupo katika mashindano makali kwa umakini usiogawanyika wa waume zetu na wana wetu, kwa taarifa mpya za michezo za masaa 24 ya siku 7, michezo ya video, taarifa mpya za soko la hisa, [na] mchanganuo na kutazama kusiko na kikomo kwa michezo ya kila mchezo wa kufikirika. Ni kana kwamba tunapoteza viti vyetu vya mbele kwa waume na wana wetu kwa sababu ya viti vyao vya mbele vya kudumu kwa [burudani na michezo].”16
Akina kaka, jukumu lako la kwanza na la juu zaidi kama mwenye ukuhani ni kumpenda na kumtunza mke wako. Kuwa kitu kimoja na yeye. Kuwa mwenza wake. Fanya iwe rahisi kwake kutaka kuwa wako. Hakuna vivutio vingine katika maisha vinapaswa kuchukua kipaumbele juu ya kujenga uhusiano wa milele na yeye. Si chochote kwenye TV, kwenye simu, au kompyuta ni muhimu kuliko ustawi wake. Tengeneza orodha ya jinsi unavyotumia muda wako na wapi unatoa zaidi nguvu zako. Hilo litakuambia wapi moyo wako upo. Omba ili moyo wako upatanishwe na moyo wa mke wako. Tafuta kumpa furaha. Tafuta ushauri wake na sikiliza. Mchango wake utaboresha utendaji wako.
Ikiwa unahitaji kutubu kwa sababu ya jinsi ambavyo umewatendea wanawake walio karibu nawe, anza sasa. Na kumbuka kwamba ni jukumu lako kuwasaidia wanawake katika maisha yako kupokea baraka zitokanazo na kuishi sheria ya Bwana ya usafi wa kimwili. Kamwe usiwe sababu kwamba mwanamke ameshindwa kupokea baraka zake za hekaluni.
Akina kaka, sote tunahitaji kutubu. Tunahitaji kutoka kwenye kochi, kuweka rimoti chini, na kuamka kutoka kwenye usingizi wetu wa kiroho. Ni muda wa kuvaa silaha zote za Mungu ili tuweze kujihusisha katika kazi ya muhimu zaidi duniani. Ni muda wa “kuingiza mundu [zetu], na kuvuna kwa nguvu, akili na uwezo [wetu] wote.”17 Majeshi ya uovu hayajawahi kughadhibika kwa nguvu kuliko yanavyofanya leo. Kama watumishi wa Bwana, hatuwezi kuwa tumelala wakati vita hii ikiendelea.
Familia yako inahitaji uongozi na upendo wako. Akidi yako na wale katika kata au tawi lako wanahitaji nguvu yako. Na wote wanaokutana na wewe wanahitaji kujua vile mfuasi wa kweli wa Bwana anavyoonekana na anavyotenda.
Kaka zangu wapendwa, mlichaguliwa na Baba yetu kuja duniani katika wakati huu muhimu kwa sababu ya ushujaa wenu kiroho kabla ya kuja duniani. Ninyi ni kati ya wanaume wazuri, mashujaa zaidi ambao wamewahi kuja duniani. Shetani anajua ninyi ni nani na mlikuwa nani kabla ya kuja duniani, na anaelewa kazi inayopaswa kufanyika kabla ya Mwokozi kurudi. Na baada ya milenia ya kujaribu sanaa yake ya hila, adui ana uzoefu na harekebishiki.
Kwa shukrani, ukuhani tulionao ni imara zaidi kuliko ulivyo werevu wa adui. Ninawasihi muwe wanaume na wavulana ambao Bwana anataka muwe. Wekeni fokasi yenu ya toba ya kila siku kuwa muhimu kwenye maisha yenu kwamba muweze kutumia ukuhani kwa nguvu kubwa zaidi kuliko hapo kabla. Hii ndiyo njia pekee utajiweka wewe mwenyewe na familia yako salama kiroho katika siku zijazo zenye changamoto.
Bwana anahitaji wanaume wanaojikana ambao wanaweka ustawi wa wengine juu ya ustawi wao. Anahitaji wanaume ambao kwa makusudi hujitahidi kusikia sauti ya Roho kwa ufasaha. Anahitaji wanaume wa agano ambao hutunza maagano yao kwa uadilifu. Anahitaji wanaume waliojitolea kujiweka wenyewe wasafi kimwili—wanaume wenye kustahili wanaoweza kuitwa dakika yoyote kutoa baraka kwa mioyo misafi, akili safi, na mikono iliyo tayari. Bwana anahitaji wanaume wenye tamaa ya kutubu—wanaume wenye ari ya kutumikia na kuwa sehemu ya batalioni ya Bwana ya wenye ukuhani wanaostahili.
Ninawabariki muwe wanaume hao. Ninawabariki kwa ujasiri wa kutubu kila siku na kujifunza jinsi ya kutumia nguvu yote ya ukuhani. Ninawabariki kuonyesha upendo wa Mwokozi kwa wake zenu na watoto na kwa wote wanaowafahamu. Ninawabariki mfanye vizuri zaidi na kuwa wazuri zaidi. Na ninawabariki kwamba mnapofanya juhudi hizi, mtapata uzoefu wa miujiza katika maisha yenu.
Tumejiingiza katika kazi ya Mwenyezi Mungu. Yesu ndiye Kristo. Sisi ni watumishi Wao. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.