Mchungaji Mwema, Mwanakondoo wa Mungu
Yesu Kristo anatuita kwa sauti Yake na kwa jina Lake. Anatutafuta na kutukusanya. Anatufundisha jinsi ya kuhudumia kwa upendo.
Wapenda akina kaka na dada zangu, je, mmewahi wakati wowote kuwa na matatizo ya kukosa usingizi na kujaribu kuhesabu kondoo wa kufikirika? Wakati kondoo mwenye manyoya mengi akiruka uzio, unahesabu: 1, 2, 3, … 245, 246, … 657, 658,…1
Katika swala langu, kuhesabu kondoo kunanifanya nikose usingizi. Nina wasiwasi kumkosa au kumpoteza mmoja, na hilo linanifanya nikose usingizi.
Pamoja na kijana mchunga kondoo ambaye alikuja kuwa mfalme, tunatangaza:
“Bwana ndiye mchungaji wangu; sitapungukiwa na kitu.
“Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza.
“Hunihuisha nafsi yangu.”2
Katika majira haya ya Pasaka, tunasherehekea kwa ajili ya mchungaji mwema, ambaye pia ni Mwanakonoo wa Mungu. Katika majina Yake yote matakatifu, hakuna mengine ambayo ni mema au yenye nguvu. Tunajifunza mengi kutokana na marejeleo ya Mwokozi wetu juu Yake kama Mchungaji mwema na kutoka katika shuhuda za kinabii juu Yake kama Mwanakondoo wa Mungu. Majukumu haya na Alama hizi zinasaidizana kikamilifu—Je ni nani ambaye yu bora kumsaidia kila mwanakondoo kuliko mchungaji Mwema, na ambaye anafaa zaidi kuwa Mchungaji wetu mwema kuliko Mwanakondoo wa Mungu?
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee”, na Mwana pekee wa Mungu alitoa maisha Yake kwa utii bila kusita kwa Baba Yake.3 Yesu anashuhudia, “Mimi ndimi mchungaji mwema: mchungaji mwema hutoa maisha yake kwa ajili ya kondoo.”4 Yesu alikuwa na uwezo wa kutoa maisha Yake na uwezo wa kuyatwaa tena.5 Pamoja na Baba Yake, Mwokozi wetu kwa kipekee anatubariki, vyote kama mchungaji wetu mwema na kama Mwana kondoo wa Mungu.
Kama Mchungaji wetu Mwema,Yesu Kristo anatuita kwa sauti Yake na kwa jina Lake. . Anatutafuta na kutukusanya. Anatufundisha jinsi ya kuhudumia kwa upendo. Acha tufikirie dhamira hizi tatu, kuanzia na Yeye kutuita kwa sauti Yake na kwa jina Lake.
Kwanza, Mchungaji wetu mwema “huwaita kondoo wake kwa jina. … Wanaijua sauti Yake.”6 Na “katika jina lake mwenyewe anakuita, ambalo ni jina la Kristo.”7 Tunapotafuta kwa dhamira ya kweli kumfuata Yesu Kristo, msukumo wa kiungu huja katika kutenda mema, kumpenda Mungu, na kumtumikia Yeye.8 Tunapojifunza, kutafakari, na kusali; tunaporudia tena mara kwa mara maagano ya sakramenti na maagano ya hekaluni; na tunapowaalika wote waje kwenye injili Yake na ibada zake, tunasikiliza sauti Yake.
Katika siku yetu, Rais Russell M.Nelson anatushauri kuliita Kanisa la urejesho kwa jina alililofunua Yesu Kristo—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.9 Bwana alisema, “Chochote mtakacho fanya, mtakifanya katika jina langu; kwa hiyo mtaliita kanisa katika jina langu; na mtamlingana Baba katika jina langu ili aweze kubariki kanisa kwa ajili yangu.”10 Kote ulimwenguni, katika mioyo na nyumba zetu, tunamlingana Baba katika jina la Yesu Kristo. Tunashukrani kwa baraka ya ukarimu kama hii ya kuabudu kunakolenga nyumbani, kunakosaidiwa na Kanisa, mafunzo ya injili, na shughuli za kifamilia zenye siha.
Pili, Mchungaji wetu Mwema anatutafuta na kutukusanya kwenye zizi lake moja. Anauliza, “Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotelewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?”11
Mwokozi wetu anamfikia mmoja na kwa wale tisini na tisa, mara nyingi kwa wakati mmoja. Tunapohudumia, tunawatambua wale tisini na tisa ambao ni imara na thabiti, hata wakati tuna shauku ya kumpata yule mmoja ambaye amepotea. Bwana wetu hututafuta na kutuokoa kutoka sehemu zote,“12 kutoka pande nne za dunia.13 Anatukusanya kwa agano takatifu na damu Yake ya upatanisho.14
Mwokozi aliwaambia wafuasi wake wa Agano Jipya, “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili.”15 Katika Amerika, Bwana aliyefufuka alishuhudia kwa watoto wa agano wa Lehi, “Na ninyi ni kondoo wangu.”16 Na Yesu alisema bado kondoo wengine wangesikia sauti Yake.17 Ni baraka iliyoje kuwa na Kitabu cha Mormoni kama ushuhuda mwingine kushuhudia sauti ya Yesu Kristo!
Yesu Kristo analialika Kanisa kuwapokea wote wanao sikia sauti Yake18 na kutii amri zake. Mafundisho ya Kristo yanajumuisha ubatizo kwa maji na kwa moto na Roho Mtakatifu.19 Nefi anauliza, “Na sasa, kama Mwanakondoo wa Mungu, akiwa mtakatifu, alihitaji kubatizwa kwa maji, ili kutimiza utakatifu wote, Ee basi, jinsi gani tunahitaji zaidi sisi, tusio watakatifu, kubatizwa, ndio, hata kwa maji!”20
Leo, Mwokozi wetu anatamani kwamba kile tunachofanya na kile tunachookuwa kitawaalika wengine kuja, kumfuata Yeye. Njoo upate upendo, uponyaji, muunganiko, na agano ndani Yake, ikijumuisha ndani ya hekalu takatifu la Mungu, ambapo ibada takatifu za wokovu zinaweza kubariki wanafamilia wote, hivyo kukusanya Israel pande zote za pazia.21
Tatu, wakati “Kama Mchunga wa Israel,”22 Yesu Kristo anaonesha kwa mfano jinsi wachungaji katika Israel wanavyohudumia kwa upendo. Wakati Bwana wetu anapouliza kama tunampenda, kama alivyofanya na Simoni Petro, mwokozi wetu anaomba sana: “Lisha wanakondoo wangu. … Lisha Kondoo Wangu. … Lisha kondoo wangu.”23 Bwana anaahidi kwamba wakati wachungaji Wake wanapolisha kondoo na wana kondoo Wake, wale katika zizi Lake “hawata hofu tena, wala kufadahaika, wala kupungukiwa.”24
Mchungaji wetu mwema anatutahadharisha kwamba wachungaji katika Israeli hawapaswi kusinzia,25 wala kutawanyika au kusababisha kondoo kupotea,26 wala kutafuta njia zetu wenyewe kwa manufaa yetu wenyewe.27 Wachunga kondoo wa Mungu wanatakiwa kuimarisha, kuponya, kufunga kile kilicho vunjika, kuleta tena kile ambacho kilitupiliwa mbali, kutafuta kile ambacho kilipotea.28
Bwana pia anaonya juu ya wachungaji wenye manufaa binafsi, ambao “hawawajali kondoo,“29 na “manabii wa uongo ambao wanawajia katika ngozi ya kondoo, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.“30
Mchugaji wetu mwema hufurahi wakati tunapotumia uhuru wetu binafsi wa kuchagua kwa dhamira na imani. Wale katika zizi lake wana mwangalia Mwokozi wetu kwa shukrani kwa sababu ya dhabihu Yake ya upatanisho. Tunafanya agano kumfuata Yeye, si kwa kukaa tu, si kwa kutokujua, au “kwa kuona aibu” lakini kwa kutamani kwa mioyo yetu yote na akili kumpenda Mungu na jirani yetu, tukibebeana mizigo na kufurahi katika shangwe za wenzetu. Kama Kristo kwa uhuru alivyotoa mapenzi yake kwa ajili ya mapenzi ya Baba, nasi pia kwa heshima kubwa tunajichukulia juu yetu jina Lake. Kwa shangwe tunatafuta kujiunga kwenye kazi Yake ya kukusanya na kuhudumia watoto wote wa Mungu.
Akina kaka na dada, Yesu Kristo ni Mchungaji wetu mkamilifu. Kwa sababu ametoa maisha Yake kwa ajili yetu, na kwa sasa kwa utukufu amefufuka, Yesu Kristo pia ni Mwanakondoo mkamilifu wa Mungu.31
Mwana kondoo wa dhabihu wa Mungu alingojewa toka mwanzo. Malaika alimwambia Adamu sadaka yake “ni mfano wa sadaka ya Mwana Pekee wa Baba,” ambayo hutualika “kutubu na kumlingana Mungu katika jina la Mwana milele yote.”32
Baba Ibrahimu, ambaye alianzisha baraka za agano kwa ajili ya mataifa yote ya dunia, alipata uzoefu wa nini ilimaanishwa kumtoa mwanae mpendwa.
“Na Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu: naye akasema, Mimi hapa mwanangu. Na akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo: lakini yuko wapi mwana-kondoo …?
“Na Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu.”33
Mitume na manabii waliona kabla na walishangilia katika huduma iliyotayarishwa tayari ya Mwanakondoo wa Mungu. Yohana katika Ulimwengu wa Kale na Nefi katika Ulimwengu Mpya walishuhudia juu ya “Mwanakondoo wa Mungu,”34 “naam, hata Mwana wa Baba wa milele[,] … Mkombozi wa ulimwengu.”35
Abinadi alishuhudia juu ya dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo: “Sisi sote, kama kondoo, tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake; na Bwana amejitwika [maovu] yetu sisi sote.“36 Alma aliita dhabihu kuu na ya mwisho ya Mwana wa Mungu “kitu kimoja ambacho ni muhimu kuliko vyote.” Alma alitia moyo, “Muwe na imani juu ya Mwanakondoo wa Mungu,” “njooni na msiogope.”37
Rafiki mpendwa alishiriki jinsi alivyopata ushuhuda wake wa thamani wa upatanisho wa Yesu Kristo. Alikua akiamini dhambi siku zote ilileta adhabu kubwa, inayobebwa na sisi peke yetu. Alimsihi Mungu ili kuelewa uwezekano wa msamaha mtakatifu. Aliomba ajue jinsi Yesu Kristo anavyoweza kuwasamehe wale wanaotubu, jinsi huruma inavyoweza kutosheleza sheria.
Siku moja sala yake ilijibiwa katika uzoefu wa kubadilisha wa kiroho. Kijana aliyekata tamaa alikuwa akitoka nje ya duka la chakula huku akikimbia akiwa amebeba vifurushi viwili vya chakula alivyoiba. Alikimbia kwenye mtaa wenye shughuli nyingi, akikimbizwa na meneja wa duka, ambaye alimkamata na kuanza kupiga yowe na kupigana. Badala ya hukumu kwa kijana aliyejawa hofu kama mwizi, rafiki yangu alijikuta bila kutegemea amejawa na huruma kubwa sana kwa ajili yake. Bila woga au kushugulika kwa ajili ya usalama wake mwenyewe, alitembea moja kwa moja kuwaelekea wanaume wawili waliokuwa wakipigana. Alijikuta akisema mwenyewe “Nitalipa hicho chakula. Tafadhali mwache aende. Tafadhali niache nilipie hicho chakula.”
Akishawishiwa na Roho Mtakatifu na kujazwa na upendo ambao kamwe hajawahi kuuhisi, rafiki yangu alisema, “Yote niliyotaka kufanya ilikuwa ni kumsaidia na kumwokoa kijana.” Rafiki yangu alisema alianza kumwelewa Yesu Kristo na Upatanisho Wake—jinsi gani na kwa nini pamoja na upendo wa kweli na mkamilifu kwa hiari yake angeweza kutoa dhabihu kuwa Mwokozi na Mkombozi wake, na kwa nini alimtaka Yeye awe hivyo.38
Ndio maana tunaimba:
Ona, Mchungaji Mwema anatafuta,
Anatafuta wanakondoo waliopotea,
Awarudisha kwa shangwe,
Wakiokolewa kwa gharama kama hiyo isiyo na mwisho.39
Kama Mwana kondoo wa Mungu, Mwokozi wetu anajua wakati tunapohisi upweke, kupungukiwa, mashaka, au woga. Katika ono, Nefi, aliona nguvu za Mwanakondoo wa Mungu, “[zikishuka] juu ya watakatifu wa kanisa la Mwanakondoo, na juu ya watu wa agano wa Bwana.” Ingawa “walitawanyika kote usoni mwa dunia; … na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”40
Ahadi hii ya matumaini na faraja inajumuisha siku yetu.
Je wewe ni muumuni pekee wa Kanisa katika familia yako, shule, mahali pa kazi, au jamii? Je Tawi lako wakati mwingine hujihisi dogo au limetengwa? Je umehamia kwenye sehemu mpya, pengine kwenye lugha au desturi usiyoifahamu? Pengine hali ya maisha yako imebadilika, na vitu ambavyo kamwe hukufikiria vinawezekana sasa vinakukabili? Mwokozi wetu anatuhakikishia, vyovyote tulivyo, kwa hali zozote tulizo nazo, katika maneno ya isaya: “Yeye atawakusanya wanakondoo kwa mkono wake, na kuwachukua kifuani mwake, na kwa ukarimu kuwaongoza wale ambao ni wadogo,”41
Akina kaka na akina dada, mchungaji wetu Mwema anatuita kwa sauti yake na kwa jina Lake. Anatafuta, anakusanya, na anakuja kwa watu Wake. Kupitia nabii Wake anayeishi na kila mmoja wetu, anawaalika wote kupata amani, lengo, uponyaji, na furaha katika utimilifu wa injili Yake ya urejesho na kwenye njia Yake ya agano. Kupitia mfano, Anawafundisha wachungaji wa Israeli kuhudumia katika upendo Wake.
Kama Mwanakondoo wa Mungu, utumishi wake mtakatifu ulichaguliwa kabla na ulifurahiwa na mitume na manabii. Upatanisho wake, usio na mwisho na wa milele, ni kitovu kwenye mpango wa furaha na lengo la uumbaji. Anatuhakikishia kwamba anatubeba karibu na moyo Wake.
Wapendwa akina kaka na dada zangu, hebu tutamani kuwa “wafuasi wanyenyekevu wa Mungu na Mwanakondoo,”42 pengine siku moja majina yetu yapate kuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha mwanakondoo,43 ili tuimbe wimbo wa Mwanakondoo,44 ili tualikwe kwenye chukula cha jioni cha Mwanakondoo.45
Kama Mchungaji na Mwanakondoo, Anaita: njoo tena “kwenye elimu ya kweli … ya Mkombozi [wako], …mchungaji [wako] mkuu na wa kweli.”46 Anaahidi kwamba “kwa rehema yake [sisi] tunaweza [kuwa] wakamilifu katika Kristo.”47
Wakati huu wa majira ya Pasaka, tunamsifu Yeye:
“Mwenye kustahili sifa ni Mwanakondoo!”48
“Hosana kwa Mungu na Mwanakondoo!“49
Ninashuhudia juu Yake, Mchungaji wetu Mkamilifu, Mwanakondoo mkamilifu wa Mungu. Anatuita kwa jina letu, katika jina Lake—hata jina takatifu na tukufu la Yesu Kristo—amina.