2010–2019
Kujiandaa kwa Ujio wa Bwana
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


2:3

Kujiandaa kwa Ujio wa Bwana

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni la kipekee na limepewa nguvu na dhamana kukamilisha maandalizi muhimu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana.

Katika wiki mbili zijazo, tutasherehekea Pasaka. Ufufuko unathibitisha utakatifu wa Yesu Kristo na uhalisia wa Mungu Baba. Mawazo yetu yanamgeukia Mwokozi, na tunatafakari “maisha yake yasiyo kifani na utakatifu wa dhabihu Yake kuu isiyo na mwisho.”1 Natumaini sisi pia tunafikiria kuhusu ujio wake ambao unasubiri wakati “atatawala kama Mfalme wa Wafalme na … Bwana wa Mabwana.”2

Wakati fulani huko Buenos Aires, Ajentina, nilishiriki katika mkutano pamoja na viongozi mbalimbali wa imani tofauti tofauti. Upendo wao kwa wengine haukuwa wa kimakosa. Walikuwa na nia katika kupunguza masumbuko na kusaidia watu kuinuka dhidi ya ukandamizaji na umasikini. Nilitafakari juu ya juhudi nyingi za kibinadamu za Kanisa hili, ikijumuisha miradi katika kushirikiana na makundi mbalimbali ya imani yaliyowakilishwa katika mkutano. Nilihisi shukrani kubwa kwa ukarimu wa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao unafanya huduma hiyo kama ya Kristo iwezekane.

Katika wasaa ule, Roho Mtakatifu alithibitisha vitu viwili kwangu. kwanza, kazi ya kuhudumia mahitaji ya kimwili ni muhimu na lazima iendelee. Cha pili kilikuwa hakikutegemewa, lakini kilikuwa chenye nguvu na dhahiri. Kilikuwa ni hiki: zaidi ya huduma isiyo ya kibinafsi, ni muhimu sana kuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana Yesu Kristo.

Wakati atakapokuja, ukandamizaji, na kukosa haki si tu kwamba vitapungua; bali vitakoma.

“ Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. …

“Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu wote mtakatifu, maana dunia itajawa na kumjua Bwana kama vile maji yanavyofunika baharini.”3

Umasikini na mateso si tu vitapungua; bali vitakwisha:

“Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena; wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote.

“Kwa maana huyo Mwana-Kondoo aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemichemi za maji yenye uhai: na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”4

Hata maumivu yaletwayo na huzuni na kifo yataondolewa:

“Katika siku hiyo mtoto mchanga hatakufa hadi amekuwa mzee; na uhai wake utakuwa kama umri wa mti;

Na wakati atakapokufa hatalala, kama tusemavyo duniani, bali atabadilishwa kwa dakika moja kufumba na kufumbua jicho, na kunyakuliwa, na pumziko lake litakuwa tukufu.”5

Hivyo ndivyo, acha tufanye yote tuwezayo kupunguza masumbuko na huzuni sasa, na acha tujitolee zaidi nafsi zetu kwa juhudi sana katika matayarisho yanayohitajika kwa ajili ya siku wakati maumivu na uovu vitakwisha kwa pamoja, wakati “Kristo [ata]tawala Yeye mwenyewe duniani; na … dunia itafanywa upya na kupokea utukufu wake wa paradiso.”6 Itakuwa ni siku ya ukombozi na hukumu. Askofu wa zamani wa Kianglikana wa Durham, Dr. N. T. Wright, ameelezea ipasavyo umuhimu wa Upatanisho wa Kristo, Ufufuko, na Hukumu katika kushinda kutokuwepo kwa haki na katika kuweka vitu vyote sawa.

Alisema: “Mungu ametenga siku ambapo ulimwengu utahukumiwa kwa haki na mtu ambaye amemchagua—na kwa hilli ametoa uthibitisho kwa wote kwa kumfufua mtu huyu kutoka kifo. Ukweli kuhusu Yesu wa Nazareti, na hasa kuhusu ufufuko wake kutoka kifo, ni msingi wa uthibitisho kwamba ulimwengu una mpangilio. Si machafuko; kwamba wakati tukitenda haki katika wakati huu hatupigi miluzi katika kiza, tukijaribu kuimarisha jengo ambalo hatimaye litaanguka, au kutengeneza gari ambalo limeshadhamiriwa kuwa vyuma chakavu. Wakati Mungu alipomwinua Yesu kutoka katika wafu, hilo lilikuwa ni tukio dogo ambalo kwalo kitendo kidogo cha hukumu kilikuwa kimebebwa katika kokwa, mbegu … ya tumaini la uhakika. Mungu alitamka, katika njia yenye nguvu inayoweza kufikirika, kwamba Yesu wa Nazareti kweli alikuwa ni Masihi. … Katika kejeli kuu ya historia, [Yesu] mwenyewe alipitia hukumu isiyo ya haki na ya kikatili, akifikia sehemu ambayo iliwakilisha na kuleta pamoja historia yote ya ukatili wote na kutokuwepo haki, kustahimili machafuko hayo, giza lile, ukatili ule, kutokuwepo kwa haki, ndani yake, na kuchosha nguvu yake.”7

Wakati bado nikiwa kwenye mkutano huko Buenos Aires ambao nimeuzungumzia hapo awali, Roho aliweka dhahiri kwangu kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni la kipekee lililopewa nguvu na kupewa dhamana ya kukamilisha maandalizi muhimu kwa ajili ya Ujio wa Bwana; ndio, lilirejeshwa kwa dhumuni hilo. Je unaweza kupata sehemu yoyote ile watu ambao wanakumbatia kipindi hiki kama kipindi kilichotolewa unabii cha “kipindi cha utimilifu wa nyakati zote,” ambacho Mungu alikikusudia “kujumlisha vitu vyote katika Kristo”?8 kama huipati hapa jamii inayokusudia kukamilisha kile kinachotakiwa kukamilishwa kwa ajili ya wote wanaoishi na waliokufa ili kujiandaa kwa ajili ya siku ile, kama huipati hapa jumuiya iliyo tayari kujitolea muda mwingi na fedha kwa ajili ya ukusanyaji na maandalizi ya watu wa agano kuwa tayari kumpokea Bwana, hutaipata sehemu nyingine yoyote.

Akizungumza na Kanisa mnamo 1831, Bwana alitamka:

“Funguo za ufalme wa Mungu zakabidhiwa kwa mwanadamu duniani, na kutoka huko injili itaenea hata miisho ya dunia. …

“Mlinganeni Bwana, ili ufalme wake uweze kuenea juu ya dunia, ili wakazi wake waweze kuupokea, na kujitayarisha kwa ajili ya siku zijazo, siku ambazo Mwana wa Mtu atashuka kutoka mbinguni, aliyevikwa katika mng’aro wa utukufu wake, kukutana na ufalme wa Mungu ambao umewekwa duniani.”9

Je tunaweza kufanya nini sasa ili kujiandaa kwa siku hiyo? Tunaweza kujiandaa sisi wenyewe kama watu; tunaweza kuwakusanya watu wa Bwana wa agano; na tunaweza kurudisha ahadi ya uukombozi “iliyotolewa kwa mababu” wahenga wetu.10 Yote haya lazima yatokee katika kiwango kidogo kidogo kabla ya Bwana kuja tena.

Cha kwanza, na cha cha muhimu kwa ajili ya ujio wa Mwokozi, ni uwepo wa watu katika dunia waliojiandaa Kumpokea katika ujio Wake. Yeye amesema kwamba wale waliobakia duniani katika siku ile “hata kuanzia mdogo wao [hata] mkubwa wao, … watajawa na kumjua Bwana, na wataona jicho kwa jicho, na watapaza sauti zao, na kwa sauti wataimba pamoja wimbo huu mpya, wakisema: Bwana ameirejesha tena Sayuni. … Bwana amevijumuisha vitu vyote katika kimoja. Bwana ameishusha Sayuni kutoka juu. Bwana ameiinua Sayuni kutoka chini.”11

Katika nyakati za kale, Mungu aliuchukua Kwake mji wa wenye haki wa Sayuni.12 Kinyume chake, katika siku za mwisho Sayuni mpya itapokelewa na Bwana katika Ujio Wake.13 Sayuni ni walio wasafi wa moyo, watu wa moyo mmoja na wazo moja, walioishi katika haki bila masikini miongoni mwao.14 Nabii Joseph Smith alisema “Tunapaswa kuifanya kazi ya kuijenga Sayuni kuwa ndilo jambo kuu zaidi kwetu.”15 Tunaijenga Sayuni katika nyumba zetu, kata, matawi na vigingi kupitia umoja, tabia za kiungu, na hisani.16

Lazima tukubali kwamba ujenzi wa Sayuni hutokea katika nyakati za misukosuko—“siku ya ghadhabu, siku ya kuteketezwa kwa moto, siku ya ukiwa, ya kulia, ya kilio, na ya maombolezo; na kama tufani itakuja juu ya uso wote wa dunia, asema Bwana.”17 Hivyo, kukusanyika katika vigingi huwa “kwa ajili ya ulinzi, na makimbilio wakati wa tufani, na ghadhabu wakati itakapomiminwa pasipo kuchanganywa juu ya dunia yote.”18

Kama ilivyokuwa katika nyakati za kale, sisi tunakutana pamoja mara kwa mara, kufunga na kuomba, na kuzungumza mmoja na mwingine kuhusu ustawi wa nafsi [zetu]. Na … Kushiriki mkate na [maji], kwa ukumbusho wa Bwana Yesu.”19 Kama Rais Russell M. Nelson alivyofafanua katika mkutano mkuu wa Oktoba iliyopita, “Kusudi la muda mrefu la Kanisa ni kuwasaidia waumini wote kuongeza imani yao katika Bwana wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake, kuwasaidia wao katika kufanya na kushika maagano yao na Mungu, na kuimarisha na kuunganisha familia zao.”20 Vivyo hivyo, alisistiza umuhimu wa maagano ya hekaluni, kuitakasa Sabato, na kusherehekea kila siku kwenye injili, kulikolenga nyumbani na kusaidiwa na mtaala wa kujifunza uliounganishwa kanisani. Tunataka kujua kuhusu Bwana, na tunataka kumjua Bwana.21

Juhudi za msingi katika kuijenga Sayuni ni kukusanyika kwa watu wa Bwana wa agano waliotawanyika kitambo.22 “Tunaamini katika kukusanyika kiuhalisi kwa Israeli na katika urejesho wa Makabila Kumi.”23 Wale wote watakaotubu, kuamini katika Kristo, na kubatizwa ni watu Wake wa agano.24 Bwana mwenyewe alitoa unabii kwamba kabla ya ujio Wake, injili ingehubiriwa kote ulimwenguni25 “kuwakomboa watu [Wake], ambao ni wa nyumba ya Israeli,”26 “na kisha mwisho utakuja.”27 Unabii wa Yeremia unatimia:

“Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, [ambapo] [hawatasema] tena, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;

“Lakini Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao.”28

Rais Neslon amesisitiza mara nyingi kwamba “kukusanyika kwa [Israeli] ni kitu muhimu zaidi kinachotokea duniani hivi leo. Hakulinganishwi na chochote katika ukubwa, hakulinganishwi na chochote katika umuhimu, hakulinganishwi na chochote katika utukufu. Na kama utachagua, … unaweza kuwa sehemu kubwa ya hilo.”29 Watakatifu wa siku za mwisho mara zote wamekuwa wamisionari. Mamia kwa maelfu wameitikia wito wa umisionari tangu mwanzo wa Urejesho; makumi ya maelfu sasa wanatumikia. Na, kama Mzee Quentin L. Cook alivyotoka kufundisha, sote tunaweza kushiriki katika njia rahisi na za kawaida, kwa upendo, kuwaalika wengine kujiunga nasi kanisani, kutembelea nyumba zetu, kuwa sehemu ya mduara wetu. Uchapishwaji wa kitabu cha Mormoni ilikuwa ni ishara kwamba kukusanyika kumeanza.30 Kitabu cha Mormoni chenyewe ni chombo cha kukusanyia na cha uongofu.

Pia muhimu katika maandalizi kwa ajili ya Ujio wa Pili ni juhudi okozi kwa niaba ya mababu zetu. Bwana aliahidi kumtuma nabiii Eliya kabla ya Ujio wa Pili, “siku iliyo kuu na ya kuogofya ya Bwana,”31 “kufunua … ukuhani” na “kupanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizotolewa kwa mababu.”32 Eliya alikuja kama ilivyoaihidiwa. Tarehe ilikuwa Aprili 3, 1836; sehemu ilikuwa ni Hekalu la Kirtland Ohio. Katika sehemu hiyo na katika wakati huo, kweli alitunuku ukuhani ulioahidiwa, funguo kwa ajili ya ukombozi wa wafu na kuunganishwa kwa waume, wake, na familia katika vizazi vyote na katika milele yote.33 Bila hili, lengo la uumbaji lisingekuwa na maana, na kwa namna hiyo dunia ingepigwa kwa laana au “kuharibiwa kabisa.”34

Katika mkutano wa kidini wa vijana kabla ya kuwekwa wakfu Hekalu la Roma Italia, mamia ya vijana wa kiume na wa kike waliohudhuria walionyesha kwa Rais Nelson kadi walizoziandaa zikiwa na majina ya mababu zao. Walikuwa tayari kuingia hekaluni kufanya ubatizo kwa niaba ya hao mababu mara tu litakapofunguliwa. Ilikuwa ni wakati wa shukrani kuu, lakini mfano mmoja wa juhudi endelevu za kujenga Sayuni kwa ajili ya vizazi ambavyo vimetangulia.

Wakati tukijitahidi kuwa na bidii katika kuijenga Sayuni, ikijumuisha sehemu yetu katika kusanyiko la wateule wa Bwana na kuwakomboa wafu, lazima tukumbuke kwamba hiyo ni kazi ya Bwana na Yeye anaifanya. Yeye ni Bwana wa shamba la mizabibu, na sisi ni watumishi Wake. Anatutaka tufanye kazi katika shamba la mizabibu kwa juhudi zetu “kwa mara hii ya mwisho” na Anafanya kazi pamoja nasi.35 Ingewezekana kuwa sahihi zaidi kusema kwamba Anaturuhusu kufanya kazi pamoja Naye. Kama Paulo alivyosema, “Mimi nilipanda, Apollo akatia maji, bali mwenye kukuza ni Mungu.”36 Ni yeye ambaye anaharakisha kazi Yake katika wakati wake.37 Tukiweka juhudi zetu zisizo kamilifu—vitu vyetu “vidogo”— Bwana huleta vitu vikubwa.38

Kipindi hiki kikuu na cha mwisho cha maongozi ya Mungu kinajijenga imara kufikia kilele chake—Sayuni katika dunia, ikiunganishwa na Sayuni kutoka juu katika ujio wa kitukufu wa Mwokozi. Kanisa la Yesu Kristo limepewa dhamana ya kuandaa—na linaandaa—ulimwengu kwa ajili ya siku hiyo. Na hivyo, Pasaka hii, acha tusherehekee hasa Ufufuo wa Yesu Kristo na yale yote unayotabiri: ujio Wake kutawala kwa miaka elfu moja ya amani, hukumu ya haki na haki kamilifu kwa wote, kutokufa kwa wote waliowahi kuishi juu ya dunia hii, na ahadi ya uzima wa milele. Ufufuo wa Kristo ni hakikisho la mwisho kwamba yote yatawekwa sawa. Acha tuwe katika kazi ya kuijenga Sayuni ili kuharakisha siku hiyo. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.