Kuwa tayari Kupata Kila Kitu Kinachohitajika
Baraka zitakuja tunapojitahidi kukamilisha jukumu letu binafsi la kujifunza na kupenda injili ya urejesho ya Yesu Kristo.
Programu na shughuli za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho zinazidi kuwa zenye kulenga sana nyumbani na kusaidiwa na Kanisa, kama ilivyoshuhudiwa kwa mfululizo wa mabadiliko yaliyotangazwa katika mikutano mikuu ya hivi karibuni. Rais Russell M. Nelson ametushauri: “Kuna mengi zaidi yanakuja. … kunyweni vidonge vyenu vya vitamini. Pumzikeni. Itakuwa ya kufurahisha.”1
Ninasali kwa ajili ya na kualika msaada wa Roho Mtakatifu tunapotafakari pamoja matokeo kadhaa ya msingi ya mabadiliko haya endelevu katika Kanisa la Bwana lililorejeshwa.
Kujifunza Injili Kunakolenga Nyumbani Kunakosaidiwa na Kanisa
Mimi na Mzee Crag C. Christensen tulikuwa pamoja hivi karibuni katika mkutano wa uongozi wa ukuhani, na alitumia maswali mawili rahisi kusisitiza kanuni ya kuwa wenye kulenga nyumbani na wanaosaidiwa na Kanisa. Alipendekeza kwamba badala ya kurudi majumbani mwetu baada ya mikutanano ya Kanisa Jumapili na kuuliza, “Ulijifunza nini kuhusu Mwokozi na injili yake Kanisani leo?” tungepaswa kuuliza katika mikutano yetu ya Kanisani, “Ulijifunza nini kuhusu Mwokozi na injili Yake wiki hii nyumbani kwako?” Kuitii Siku ya Sabato kwa usahihi, mtaala mpya, na ratiba ya mikutano iliyobadilishwa vyote vinatusaidia kujifunza injili kote nyumbani kwetu na kanisani.
Kila Muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ana jukumu binafsi kujifunza na kuishi mafundisho ya Bwana na kupokea kutoka mamlaka sahihi ibada za wokovu na kuinuliwa. Hatupaswi kutegemea Kanisa kama taasisi kutufundisha au kutuambia kila kitu tunachohitaji kujua na kufanya ili kuwa wafuasi tulioongoka na kuvumilia kishujaa mpaka mwisho.2 Badala yake, wajibu wetu binafsi ni kujifunza kile tunachopaswa kujifunza, kuishi kama tunavyojua tunapaswa kuishi, na kuwa yule ambaye Bwana angetaka tuwe. Na nyumba zetu ni sehemu ya msingi kwa ajili ya kujifunza, kuishi, na kuwa.
Kama mtoto, Joseph Smith alijifunza juu ya Mungu kutoka kwa familia yake. Juhudi zake kugundua mapenzi ya Mungu kwa ajili yake zilisababisha Joseph kuchunguza ukweli miongoni mwa madhehebu mengi tofauti ya Kikristo, kutafakari kwa bidii maandiko, na kusali kwa dhati kwa Mungu. Wakati kijana Joseph Smith aliporudi nyumbani kwake kutoka Kijisitu Kitakatifu mara tu baada ya kutokea kwa Baba na Mwana, alizungumza kwanza na mama yake. Alipokuwa “ameegemea, kwenye sehemu ya kuotea moto, mama [yake] aliuliza kulikuwa na tatizo gani. [Joseph] alijibu, ‘Usijali, sina tatizo lolote—niko sawa.’ [Yeye] kisha alimwambia mama [yake], ‘Nimejifunza mimi mwenyewe’”3 Uzoefu wa Joseph unatoa mpangilio wenye nguvu wa kujifunza ambao kila mmoja wetu anapaswa kuiga. Sisi pia tunapaswa kujifunza wenyewe.
Lengo kuu la mpango wa Baba wa Mbinguni ni kwa ajili ya watoto Wake kuwa zaidi kama Yeye. Kwa namna hiyo, Yeye anatupatia fursa muhimu kukua na kuendelea. Msimamo wetu kujifunza na kuishi kulingana na ukweli ni muhimu sana katika ulimwengu ambao upo ”katika vurugu”4 na daima wenye kuchanganyikiwa zaidi na wenye uovu. Hatuwezi kutegemea tu kuhudhuria mikutano ya Kanisa na kushiriki katika programu na kwa hiyo kupokea ujenzi wote wa maadili ya kiroho na ulinzi ambao utatuwezesha “kushinda katika siku ya uovu.”5
“Wazazi wana jukumu takatifu la kuwalea watoto wao kwa upendo na uadilifu.”6 Viongozi wa Kanisa waliopata msukumo wa kiungu, walimu, na shughuli husaidia juhudi za mtu binafsi na familia kukua kiroho. Na ingawa wote tunahitaji msaada kusonga mbele kwenye njia ya agano, wajibu wa mwisho kwa ajili ya kukuza nguvu za kiroho na uthabiti upo juu ya kila mmoja wetu.
Kumbuka jinsi Nephi, mwana wa nabii Lehi, alivyotamani kuona, kusikia, na kujua yeye mwenyewe kwa nguvu ya Roho Mtakatifu vitu ambavyo baba yake alijifunza katika ono la mti wa uzima. Nefi kwa hakika alihitaji na alikuwa amebarikiwa katika ujana wake kwa mfano na mafundisho ya “wazazi wake wema.”7 Bado, kama vile Joseph Smith, alitamani kujifunza na kujua yeye mwenyewe.
Kama yote mimi au ninyi tunayojua kuhusu Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho ni kile watu wengine wanachotufundisha au kutuambia, basi msingi wa ushuhuda wetu Kwake na utukufu wa kazi Yake ya siku za mwisho umejengwa juu ya mchanga.8 Hatuwezi pekee kutegemea au kuazima nuru ya injili na ufahamu kutoka kwa watu wengine—hata wale tunao wapenda na kuwaamini.
Kwa umuhimu huo, Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba kila Mtakatifu wa Siku za Mwisho anahitaji kuelewa yeye mwenyewe “mipango na malengo ya Mungu katika kuja kwetu ulimwenguni.”9
“Tungeweza kusoma na kuelewa yale yote yaliyoandikwa kutoka siku za Adamu, juu ya uhusiano wa binadamu na Mungu na malaika katika hali ya baadae, tungejua machache kuhusu hilo. Kusoma uzoefu wa wengine, au ufunuo uliotolewa kwao kamwe hakuwezi kutupa mtazamo wa uwezo wa kufahamu hali yetu na uhusiano wa kweli kwa Mungu. Ufahamu wa vitu hivi unaweza tu kupatikana kwa uzoefu kupitia ibada za Mungu zilizotolewa kwa lengo hilo.”10
Kuwezesha kukamilishwa kwa lengo hili kuu la kiroho kwa ajili ya watu binafsi na familia ni moja kati ya sababu kuu shughuli na programu za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho zinakuwa zaidi zenye kulenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa katika kipindi hiki muhimu cha maongozi ya Mungu cha utimilifu wa nyakati.
Matokeo ya Kujifunza Kunakolenga Nyumbani Kunakosaidiwa na Kanisa.
Acha nifanye muhtasari wa matokeo machache muhimu ya kujifunza injili kunakoongezeka kuwa kulikolenga nyumbani na kusaidiwa na Kanisa.
Kituo cha mafunzo ya umisionari cha msingi kiko nyumbani kwetu; vituo vya upili vya mafunzo ya umisionari vipo Provo, Manila, Jiji la Mexico, na katika maeneo mengine. Madarasa yetu bora ya kuelimisha ya Shule ya Jumapili yanapaswa kuwa mafundisho ya mtu binafsi na familia zetu katika sehemu zetu za kuishi; yakisaidia japo ni ya upili madarasa ya Shule ya Jumapili yanafanyika katika nyumba zetu za mikutano.
Vituo vya historia ya Familia sasa vipo katika nyumba zetu. Msaada wa ziada kwa ajili ya kazi ya utafiti wa historia za familia zetu pia unapatikana katika nyumba zetu za mikutano.
Madarasa muhimu ya maandalizi ya hekaluni yanatokea katika nyumba zetu; yakisaidia japo ni ya upili madarasa ya maandalizi ya hekaluni pia yanaweza kufanyika kila baada ya muda fulani katika nyumba zetu za mikutano.
Kufanya nyumba zetu kimbilio ambapo tunaweza “kusimama katika mahali patakatifu”11 ni muhimu katika siku za mwisho. Na kama kulivyo muhimu kujifunza kulikolenga nyumbani na kunakosaidiwa na kanisa kwa ajili ya nguvu zetu za kiroho na ulinzi leo, kutakuwa hata muhimu zaidi katika siku za baadaye.
Kujifunza Kunakolenga Nyumbani-Kunakosaidiwa na Kanisa na Maandalizi ya Hekakuni
Tafadhali fikiria jinsi kanuni ya “kulenga nyumbani kunakosaidiwa na Kanisa” inavyotumika katika maandalizi yetu binafsi na ustahiki wetu kupokea ibada takatifu na maagano katika nyumba ya Bwana.
Naam, maandalizi ya kuhudhuria hekaluni hufanyika vizuri nyumabani kwetu. Lakini waumini wengi wa Kanisa hawana uhakika kuhusu nini kinaweza na hakiwezi kusemwa kuhusu uzoefu wa hekaluni nje ya hekalu.
Rais Ezra Taft Benson alielezea kwa nini kutokuwa na uhakika huku kupo:
“Hekalu ni mahali patakatifu, na ibada katika hekalu ni za sifa takatifu. Kwa sababu ya utakatifu wake wakati mwingine tunasita kusema chochote kuhusu hekalu kwa watoto na wajukuu wetu.
“Kama matokeo, wengi hawajengi nia ya kweli kwenda hekaluni, au wakati wanapokwenda, wanafanya hivyo bila ufahamu wa kutosha kuwaandaa kwa ajili ya wajibu na maagano wanayoingia.
“Ninaamini ufahamu sahihi au uelewa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaanda vijana wetu kwa ajili ya hekalu … [na] itakuza ndani yao hamu ya kutafuta baraka zao za ukuhani kama vile Ibrahimu alivyotafuta zake.”12
Miongozo miwili ya msingi inaweza kutusaidia kufanikisha ufahamu sahihi uliosisitizwa na Rais Benson.
Muongozo #1. Kwa sababu tunampenda Bwana, siku zote tunapaswa kuzungumza kuhusu nyumba Yake takatifu kwa heshima. Hatupaswi kutoa au kuelezea alama maalumu zinazohusisha maagano tunayopokea katika ibada maalumu takatifu hekaluni. Wala hatupaswi kujadili taarifa takatifu ambazo kwazo tunaahidi hekaluni kutozitoa.
Muongozo #2. Hekalu ni nyumba ya Bwana. Kila kitu katika hekalu kinatuelekeza kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Tunaweza kujadili malengo ya msingi na mafundisho na kanuni zinazohusiana na ibada na maagano ya hekaluni.
Rais Howard W. Hunter alishauri: “Na tushiriki pamoja na watoto wetu hisia za kiroho tunazokuwa nazo hekaluni. Na tuwafundishe kwa bidii zaidi na bila woga vitu tunavyoweza kusema kwa usahihi kuhusu malengo ya nyumba ya Bwana.”13
Katika vizazi vyote, kutoka Nabii Joseph Smith mpaka Rais Russell M. Nelson, malengo ya kimafundisho ya ibada na maagano ya hekaluni yamefundishwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa Kanisa.14 Hazina kubwa ya nyenzo ipo katika machapisho, video, na mifumo mingine ili kutusaidia kujifunza kuhusu ibada za mwanzo, endaumenti, ndoa, na ibada zingine za kuunganisha.15 Taarifa pia zinapatikana kuhusu kumfuata mwokozi kwa kupokea na kuheshimu maagano ili kushika sheria ya utiifu, sheria ya dhabihu, sheria ya injili, sheria ya usafi wa kimwili, na sheria ya kuweka wakfu.16 Waumini wote wa Kanisa wanapaswa kuwa na uzoefu wa nyenzo bora zinazopatikana kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org.
Rais Russell M. Nelson alisisitiza uwiano muhimu kati ya asili takatifu ya ibada za hekaluni na taarifa za thamani kuhusu mahekalu zilizo chapishwa na Kanisa ambazo ni sahihi, za kufaa, na zinazopatikana kwa kila mtu. Alieleza: “Ninapendekeza kwamba waumini … wasome maneno katika Kamusi ya Biblia ambayo yana uhusiano na hekalu , kama vile ‘Mpako,’ ‘Agano,’ ‘Dhabihu,’ na ‘Hekalu.’ Mtu anaweza pia kutaka kusoma Kutoka, sura za 26–29, na Mambo ya Walawi sura ya 8. Agano la Kale, pamoja na vitabu vya Musa na Ibrahimu katika Lulu ya Thamani Kuu, vinasisitiza asili ya kazi ya hekalu na asili ya mwendelezo wa ibada zake.”17
Kwa hivyo, fikiria kwamba mwanao au binti yako anauliza, “Mtu fulani shuleni aliniambia kwamba nguo za ajabu zinavaliwa hekaluni. Je! Hilo ni kweli? Video fupi inapatikana kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org yenye kichwa cha habari “Nguo Takatifu za Hekaluni.” Nyenzo hii bora inaelezea jinsi toka nyakati za kale wanaume na wanawake wamekumbatia muziki wa kale, aina tofauti za sala, nguo zenye maana ya kidini, ishara za mikono, na matambiko kuonesha hisia zao za ndani zaidi za moyo wa ibada kwa Mungu. Hivyo, Kanisa linasaidia maandalizi yaliyolenga nyumbani kwa ajili ya baraka zenye utukufu za hekaluni kupitia maelekezo ya msingi na nyenzo za kustaajabisha kama vile video hii. Taarifa nyingi zenye manufaa tele zinapatikana kwako.18
Tunapojitahidi kutembea katika unyenyekevu wa Roho wa Bwana,19 tutabarikiwa kuelewa na kufikia katika nyumba zetu uwiano muhimu kati ya kile kinachofaa na kisichofaa kujadiliwa kuhusu ibada na maagano matakatifu ya hekaluni.
Ahadi na Ushuhuda
Nadhani baadhi yenu mnaweza kuwa mnajiuliza kama kujifunza kwenu injili kwa kweli kunaweza kuwa kwenye kulenga nyumbani na kunakosaidiwa na Kanisa. Pengine wewe ni muumini pekee wa Kanisa katika nyumba yenu, au una mwenza asiyesaidia, au ni mzazi pekee, au unaishi peke yako kama mseja au Mtakatifu wa Siku za Mwisho aliyetalikiwa, na unaweza kuwa na maswali kuhusu jinsi kanuni hizi zinavyotumika kwako. Mnaweza kuwa ni mume na mke mkiangaliana na kuulizana , “Tunaweza kufanya hili?”
Ndiyo, mnaweza kufanya hili! Ninaahidi kwamba baraka zinazowezesha zitatiririka ndani na kuwa wazi katika maisha yenu. Milango itafunguka. Nuru itaangaza. Uwezo wako utaongezwa kuvumilia kwa bidii na kwa subira.
Ninashuhudia kwamba baraka za fidia zitakuja tunapojitahidi kukamilisha jukumu letu binafsi la kujifunza na kupenda injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Kwa kweli tunaweza “kujitayarisha kupokea kila jambo linalohitajika.”20 Ninaahidi hivyo na kushuhudia katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.