2010–2019
Upatanisho wa Yesu Kristo
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


2:3

Upatanisho wa Yesu Kristo

Upatanisho wa Mwokozi si tu usio na mwisho katika uwezo lakini wa kibinafsi katika kuufikia.

Katika msimu huu wa mwaka tunasherehekea hasa na kutafakari juu ya Upatanisho wa Mwokozi. Kwa hakika ni mafundisho ya kiungu, yenye kupanua akili, yenye shauku zaidi ambayo dunia au ulimwengu huu umewahi kuyajua. Ni kile ambacho huleta tumaini na lengo katika maisha yetu.

Ni nini basi Upatanisho wa Yesu Kristo? Kwa namna moja, ni mfululizo wa matukio ya kiungu ambayo yalianza katika Bustani ya Gethsemane, yakaendelea msalabani, na kufikia kilele kwa Kufufuka kwa Mwokozi kutoka kaburini. Ulisababishwa na upendo usioelezeka kwa kila mmoja wetu. Ulihitaji kiumbe asiye na dhambi; ambaye alikuwa na uwezo usio na kikomo dhidi ya vitu vya asili—hata kifo; ambaye alimiliki uwezo usio na mipaka wa kuteseka kwa ajili ya dhambi na maradhi yetu yote; na ambaye, kwa hakika, alishuka chini ya vitu vyote.1 Hii ndiyo ilikuwa misheni ya Yesu Kristo—huu ulikuwa Upatanisho Wake.

Ni nini basi lilikuwa lengo lake? Ilikuwa kutuwezesha kurudi katika uwepo wa Mungu, kuwa zaidi kama Yeye, na kupokea shangwe timilifu. Hili lilifanyika kwa kushinda vizuizi vinne:

  1. Kifo cha kimwili

  2. Kifo cha kiroho kilichosababishwa na Adamu na dhambi zetu

  3. Mateso na unyonge wetu

  4. Udhaifu na mapungufu yetu

Lakini ni jinsi gani Mwokozi anaweza kutimiza hili bila ya kukiuka sheria za haki?

Kuanguka bila kizuizi kutoka kwenye ndege

Fikiria kwa muda mtu anayezingatia kuruka bila mwavuli anafanya uamuzi wa pupa na kuruka kwa hiari kutoka kwenye ndege ndogo. Baada ya kufanya hivyo, kwa haraka anagundua upumbavu wa vitendo vyake. Anataka kutua salama, lakini kuna kizuizi—sheria ya mvutano. Anazungusha mikono yake kwa mwendo wa kushangaza, akiwa na tumaini la kupaa, lakini hakuna mafanikio. Anaweka mwili wake katika mkao wa kuelea au kunyiririka ili kupunguza mshuko, lakini sheria ya mvutano ina hasira na haina huruma. Anajaribu kutoa hoja kwa sheria hii ya msingi ya asili: “Ilikuwa ni makosa. Sitarudia tena.” Lakini kilio chake kinafikia masikio yasiyosikia. Sheria ya mvutano haifahamu huruma; haifanyi upekee. Kwa bahati, hata hivyo, mtu huyo ghafla anahisi kitu fulani mgongoni. Rafiki yake ndani ya ndege, alipoona muda huo wa upumbavu, alikuwa ameweka mwavuli hapo kabla tu ya kuruka. Anatafuta ugwe wa mwavuli na kuuvuta. Akiwa ametulia, anaelea salama hadi chini. Tunaweza kuuliza, “Je, sheria ya mvutano ilikiukwa, au mwavuli ule ulifanya kazi kulingana na sheria ili kusababisha kutua salama?”

Kutumia mwavuli kutua salama

Tunapotenda dhambi, tunakuwa kama yule mtu mpumbavu aliyeruka kutoka kwenye ndege. Haijalishi chochote tunachofanya sisi wenyewe, ni kuanguka tu kunakotusubiri. Tunatawaliwa na sheria ya haki, ambayo, kama sheria ya mvutano, inashurutisha na haisamehi. Tunaweza kuokolewa tu kwa sababu Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake, kwa neema anatupatia mwavuli wa kiroho wa aina fulani. Tukiwa na imani katika Yesu Kristo na kutubu (ikimaanisha kwamba tunafanya sehemu yetu na kuuvuta ugwe wa mwavuli), ndipo nguvu za ulinzi za Mwokozi zinafunguliwa kwa niaba yetu na tunaweza kutua kiroho bila kujeruhiwa.

Hili linawezekana tu, hata hivyo, kwa sababu Mwokozi alishinda vizuizi vinne ambavyo vinaweza kuzuia maendeleo yetu ya kiroho.

1. Kifo. Alishinda kifo kupitia Ufufuo Wake mtukufu. Mtume Paulo alifundisha: “Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.”2

2. Dhambi. Mwokozi alishinda dhambi na hatia kwa wale wote ambao wanatubu. Nguvu Zake za kusafisha ni za kina na pana kwamba Isaya aliahidi, “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji.”3

Mara kwa mara, nimekutana na Watakatifu wema ambao wanapata wakati mgumu kujisamehe, ambao bila hatia lakini kimakosa wameweka vikwazo juu ya nguvu za ukombozi za Mwokozi. Pasi na kujua, wamegeuza Upatanisho usio na mwisho kuwa wenye mwisho ambao kwa namna fulani unapungukia dhambi au udhaifu wao maalumu. Lakini ni Upatanisho usio na mwisho kwa sababu unajumuisha na kuwekea mipaka kila dhambi na udhaifu, vile vile kila dhuluma au maumivu yanayosababishwa na wengine.

Truman Madsen alisema maneno haya ya kufariji:

“Kama kuna baadhi yenu ambao mmedanganywa kwamba mmevuka mipaka, … kwamba mnayo sumu ya dhambi ambayo inafanya isiwezekane kwenu kamwe kuwa kile ambacho mngeweza kuwa—basi nisikilizeni.

“Ninashuhudia kwamba hauwezi kuzama mbali zaidi na nuru na akili kubwa ya Yesu Kristo inapoweza kufikia. Ninashuhudia ya kwamba ilimradi kuna cheche moja ya hiari ya kutubu na kufikia, Yeye yupo hapo. Yeye hakushuka tu chini kufikia hali yako; Alishuka chini ya hali hiyo, ’ili Aweze kuwa katika vyote na ndani ya vitu vyote, nuru ya ukweli.’ [Mafundisho na Magano 88:6.]”4

Sababu moja ya umuhimu wa kuelewa Upatanisho wa Mwokozi na athari zake zisizo na mwisho ni kwamba kwa kuongezeka kwa uelewa huja ongezeko la hamu ya kujisamehe pamoja na kusamehe wengine.

Ingawaje tunaweza kuamini katika nguvu za Kristo za kusafisha, swali mara nyingi huibuka: “Ni kwa jinsi gani nitajua kama nimesamehewa dhambi zangu?” Kama tutahisi Roho, basi huo ni ushahidi wetu kwamba tumesamehewa, au kwamba mchakato wa kusafishwa unaendelea. Rais Henry B. Eyring alifundisha, “Kama umehisi ushawishi wa Roho Mtakatifu … , unaweza kuchukulia hilo kama ushahidi kwamba Upatanisho unafanya kazi katika maisha yako.”5

Barabara iliyofika mwisho

Baadhi wameuliza, “Lakini ikiwa nimesamehewa, kwa nini ningali nahisi hatia?” Pengine katika neema ya Mungu kumbukumbu hiyo ni onyo, “ishara ya simama” ya kiroho ya aina fulani ambayo, angalau kwa muda, hupaza sauti wakati majaribu ya ziada yanapotukabili: “Usielekee katika njia hiyo. Unajua uchungu inayoweza kusababisha.” Kwa namna hii, inatumika kama kinga, si adhabu.

Je, inawezekana basi kukumbuka dhambi zetu na kutokuwa na hatia?

Alma alikumbuka dhambi zake, hata miaka mingi baada ya kutubu. Lakini alipomlilia Yesu kwa ajili ya rehema, alisema, “Sikukumbuka uchungu wangu tena; ndio, sikuteseka na ufahamu wa dhambi zangu tena.”6

Ni kwa jinsi gani aliweza kukumbuka dhambi zake lakini hakuwa na uchungu au hatia? Kwa sababu tunapotubu, tuna “zaliwa kwa Mungu.”7 Tunakuwa, jinsi maandiko yanavyosema, “viumbe wapya”8 katika Kristo. Kwa ukweli kamili sasa tunaweza kusema, “Mimi si yule mwanaume au mwanamke aliyetenda dhambi zile za zamani. Mimi ni kiumbe kipya na aliyebadilika.”

3. Mateso na Unyonge. Alma alitabiri kwamba Kristo “atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina.” Kwa nini? “Ili moyo wake ujae rehema, … ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao.”9

Anawezaje kutimiza hili? Wakati mwingine Yeye huondoa masumbuko, wakati mwingine Yeye hutuimarisha tuweze kuvumilia, na wakati mwingine Yeye hutupatia mtazamo wa milele ili tuweze kuelewa asili yake ya muda. Baada ya Joseph Smith kuteseka katika Gereza la Liberty kwa takriban miezi miwili, hatimaye alilia kwa sauti,“Ee Mungu, uko wapi?”10 Badala ya kutoa msaada wa papo kwa hapo, Mungu alijibu, “Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi; na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu.”11

Joseph sasa alielewa kwamba uzoefu huu mgumu ulikuwa nukta tu katika taswira ya milele. Akiwa na ono hili kubwa, aliwaandikia Watakatifu kutoka kwenye gereza lile lile, “Ndugu wapendwa, kwa furaha na tufanye mambo yote yaliyo katika uwezo wetu; na ndipo tusimame imara, kwa uhakika mkubwa, kuuona wokovu wa Mungu.”12 Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, tunaweza kuwa na mtazamo wa milele ambao unaleta maana kwa majaribu yetu na tumaini kwa ajili ya faraja yetu.

4. Udhaifu na Mapungufu. Kwa sababu ya Upatanisho Wake, Mwokozi ana nguvu za kuwezesha, wakati mwingine zikiitwa neema,13 ambazo zinaweza kutusaidia kushinda udhaifu wetu na mapungufu na hivyo kutusaidia katika jitihada zetu za kuwa kama Yeye.

Moroni alifundisha hivyo: “Ndio, mje kwa Kristo na mkamilishwe ndani yake, … kwamba kwa neema yake mngekamilishwa katika Kristo.”14 Kunaonekana angalau njia au namna mbili za kupata nguvu hizo za kuwezesha ambazo zinaweza kutusafisha—hata kutukamilisha—sisi.

Kwanza, ibada za kuokoa. Maandiko yanatueleza, “Katika ibada hizo, nguvu za uchamungu hujidhihirisha.”15 Wakati mwingine, twaweza kufikiria juu ya ibada kama orodha ya kupimia—inayohitajika kwa ajili ya kuinuliwa; lakini katika ukweli kila moja inafungulia nguvu ya kiungu ambayo inatusaidia sisi kuwa zaidi kama Kristo. Kwa mfano:

  • Wakati tunapobatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, tunafanywa kuwa wasafi—na hivyo kuwa watakatifu zaidi kama Mungu.

  • Kwa kuongezea, kupitia Roho Mtakatifu, akili zetu zinaweza kuangazwa na mioyo yetu kulainishwa ili tuweze kufikiria na kuhisi zaidi kama Yeye.

  • Na wakati tunapounganishwa na wenza wetu, tunarithi haki ya “enzi, falme, himaya, na nguvu”16 kama karama kutoka kwa Mungu.

Njia ya pili kwa ajili ya nguvu hizi zenye kuwezesha ni karama za Roho. Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, tunastahili kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na karama za kiroho zinazoambatana nacho. Karama hizi ni tabia za kiungu; kwa hivyo, kila wakati tunapopata karama ya Roho, tunakuwa zaidi kama Mungu. Hakika hii ndiyo sababu maandiko yanatuamuru mara nyingi kwamba tutafute karama hizi.17

Rais George Q. Cannon alifundisha: “Mtu yeyote hapaswi kusema, ‘Oh, siwezi kujizuia; ni asili yangu.’ Hawezi kuhalalishwa kwa hilo, kwa sababu Mungu ameahidi … kutoa karama ambazo zitakomesha [udhaifu wetu]. … Ikiwa yeyote kati yetu si mkamilifu, ni wajibu wetu kuomba tupate karama ambayo itatukamilisha.”18

Kwa kifupi, Upatanisho wa Mwokozi unatupatia uhai badala ya kifo, “taji ya maua badala ya majivu,”19 uponyaji badala ya maumivu, na ukamilifu badala ya udhaifu. Ni kiuasumu cha mbinguni kwa ajili ya vizuizi na shida za ulimwengu huu.

Katika wiki ya mwisho ya Mwokozi ya maisha ya duniani, Alisema “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”20 Kwa sababu Mwokozi alitimiza Upatanisho Wake, hakuna nguvu au tukio au mtu wa nje—dhambi au kifo au talaka—ambayo inaweza kutuzuia sisi tusiweze kuinuliwa, kwa sharti kwamba tunatii amri za Mungu. Kwa ufahamu huo, tunaweza kusonga mbele tukiwa tumechangamka na uhakika kamili kwamba Mungu yu nasi katika tamanio hili la kimbingu.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Upatanisho wa Mwokozi si tu usio na mwisho katika uwezo lakini wa kibinafsi katika kuufikia—kwamba si tu unaturudisha katika uwepo wa Mungu bali pia kutuwezesha kuwa kama Yeye—lengo kuu la Upatanisho wa Kristo. Kwa hilo ninatoa ushahidi wangu wa shukrani na wa hakika katika jina la Yesu Kristo, amina.