2016
Kutafuta Karama za Kiroho
Aprili 2016


Mpaka Tutakapokutana Tena

Kutafuta Karama za Kiroho

Kutoka The Latter-day Saints Millennial Star, Apr. 23, 1894, 258–61; kuwekwa kwa vituo katika maandiko na herufi kubwa kama kiwango elekezi.

Ni wangapi kati yenu wanatafuta karama hizi ambazo Mungu ameahidi kuteremsha?

hanging lightbulbs

Picha © iStock/Thinkstock

Kila mwanaume na mwanamke katika Kanisa la Kristo anaweza kuwa na karama za Roho wa Mungu kulingana na imani yao na mapenzi ya Mungu. …

Ni wangapi kati yenu … wanatafuta karama hizi ambazo Mungu ameahidi kuteremsha? Ni wangapi kati yenu, ambao mnapomwinamia Baba yenu wa Mbinguni katika mzunguko wa familia au katika sehemu zenu za siri, mnapambana kwa ajili ya karama hizi ili ziteremshwe kwenu? Ni wangapi kati yenu mnamuomba Baba, katika jina la Yesu, ajidhihirishe kupitia nguvu hizi na karama hizi? Au mnaendelea siku hadi siku, kama mlango unavyozunguka kwenye bawaba zake, bila ya kuwa na hisia zozote kuhusu mada, bila ya kutumia imani yoyote, mkitosheka na kubatizwa na kuwa waumini wa Kanisa na kupumzika hapo, mkifikiria kuwa wokovu wenu upo salama kwa sababu mmefanya hivi? …

… Ninajua kuwa ni mapenzi yake Mungu kuwaponya wagonjwa, kuwa ni mapenzi Yake kuteremsha karama ya kuzitambua roho, karama ya hekima, ya maarifa na ya kutoa unabii, na karama zingine zinazoweza kuhitajika. Ikiwa yeyote kati yetu si wakamilifu, ni wajibu wetu kuomba tupate karama ambayo itatukamilisha. Je, mimi nina mapungufu? Niko nayo chungu mzima. Wajibu wangu ni nini? Kuomba kwake Mungu anipe karama ambazo zitasahihisha mapungufu haya. Ikiwa mimi ni mtu mwenye hasira, ni wajibu wangu kuomba ili niwe na hisani, ambayo huvumilia na ni karimu. Je, mimi ni mtu mwenye wivu? Ni wajibu wangu kutafuta hisani, ambayo haina wivu. Na hivyo kwa karama zote za injili. Zimekusudiwa kwa lengo hili. Mtu yeyote hapaswi kusema, “Loo, siwezi kujizuia, ni maumbile yangu.” Hahalalishwi ndani yake, kwa sababu Mungu aliahidi kutoa nguvu kusahihisha mambo haya, na kutoa karama ambazo zitayatokomeza. Kama mtu hana busara, ni wajibu wake kumwomba Mungu ampe busara. Vile vile kwa kila kitu kingine. Huo ndio mpango wa Mungu kuhusu Kanisa Lake. Anataka Watakatifu wake wakamilishwe katika ukweli. Kwa madhumuni haya Yeye hutoa karama hizi na kuwateremshia wale wanaozitafuta, ili wapate kuwepo watu wakamilifu usoni mwa ulimwengu, bila ya kujali udhaifu wao mwingi, kwa sababu Mungu ameahidi kutoa karama ambazo ni muhimu kwa ukamilifu wao.