Hata Kama Unaona Haya
Mwamini Bwana, Naye atakubariki katika juhudi zako za kueneza injili.
Nilipokuwa rais mpya wa misheni kule Brazili, nilikuwa nikiwasaili wazee fulani. Nilimuuliza mmoja aniambie kuhusu yeye mwenyewe.
“Mimi ni mwenye haya sana,” alisema. Alikuwa na wasiwasi kuwa kuona haya kwake kulikuwa kunaathiri uwezo wake wa kuhudumu.
Nilimuuliza, “Unafikiri Bwana anaweza kukusaidia kuwa mmisionari mzuri kwa njia yoyote?”
“Ninaamini Bwana anaweza kufanya chochote.”
“Basi mwache akusaidie. Unafikiri unaweza kufanya hivyo?”
“Ninaweza,” alisema.
Inabidi nikiri kuwa alipokuwa akiondoka, nilifikiri, “Barabara, natumai atafanikiwa.”
Wiki zilipita na punde wamisionari wale wale wakaja kwenye usaili tena. Wakati huu mwenzake yule mzee mwenye kuona haya alisema, “Rais, sijui ulichomwambia lakini hakika kilileta tofauti. Amekuwa mweledi katika kuzungumza na watu.” Na hivyo nilikuwa na shauku ya kuonana naye tena.
Alipoingia ofisini mwangu, alitazama chini miguuni mwake.
“Nina habari njema,” alisema. “Mimi bado ni mwenye haya, lakini nilimwomba Bwana anisaidie. Kisha nikafungua kinywa changu na nikaanza kuzungumza. Na unajua nini? Mimi hufanya hivyo kila wakati sasa. Hata huwa sikumbuki ninayosema. Cha ajabu ni kuwa watu wanafurahia. Wanahisi Roho. Wanajihusisha nami na yale ninayowaeleza.”
Nilishangaa sana kuona jinsi ambavyo mmisionari huyu alivyobadilika alipoweka imani yake katika Bwana. Alikuja kuwa chombo kikuu katika kuleta furaha kwa watu wengi.
Kushinda Hofu
Tunaposhiriki injili, mara nyingine sisi huwa na wasiwasi. Lakini kama mmisionari huyu mwenye haya alivyodhihirisha, Bwana atatuongoza tukimwamini. Roho Mtakatifu atatusaidia kujua la kusema (ona 2 Nefi 32:2–3), na wakati watu wanapohisi Roho, mara nyingi wao hujibu kwa njia chanya. Wengi huvutiwa sana na kile tunachoamini na hutaka kujua zaidi.
Furaha Kubwa
Nina ushuhuda kuwa Baba wa Mbinguni atatuongoza katika juhudi zetu za kushiriki injili, na katika njia hiyo tutasikia furaha kubwa. Kwa kweli, furaha hiyo itakuwa nasi sio tu kwa sasa bali katika ulimwengu ujao. (Ona M&M 18:16.) Hiyo ni sababu mzuri ya kutoka nje ya eneo lako la faraja na kufanya jambo, hata ikiwa wewe ni mwenye haya.