Mshtuko, Huzuni, na Mpango wa Mungu
Mwandishi anaishi Albania.
Kupitia tukio lililonibananga zaidi maishani mwangu, nilihisi kuwa Baba wa Mbinguni alikuwa nami wakati huo wote.
Ilikuwa asubuhi moja mapema 2008 wakati mama yangu aliponiamsha ili niende shuleni. Nilikuwa na furaha asubuhi hiyo, lakini sikujua kuwa ingegeuka kuwa siku mbaya zaidi maishani mwangu au siku ya mwisho ambayo ningekuwa pamoja naye. Sikumaliza masomo yangu siku hiyo kwani rafiki wa familia yetu alikuja kunichukua na kuniambia kuwa mama yangu alikuwa amejiua. Nilikuwa na miaka 12 tu.
Nilifikiria, “Ni namna gani naweza kuishi bila mama?” Alikuwa rafiki yangu wa dhati.
Nililia kwa miezi kadha. Sikufurahia kwenda shuleni kwa sababu wale watoto wengine walinitendea tofauti na wengine na kunionea huruma. Sikuwa na fununu nilichohitajika kufanya; nilijua ilinibidi nijipe moyo tu kwa ajili ya kila mtu.
Siku moja, miezi mitano au sita baada ya kifo cha mamangu, nilikuwa peke yangu ndani ya chumba changu karibu na dirisha, nikilia, nikijaribu kuelewa sababu ya kuwa hapa. Ghafla nilisikia sauti akilini: “Wewe ni binti yangu, sitakuacha uteseke.” Nilijua alikuwa Mungu. Lakini ilinishangaza kwa sababu sikuwa nikimwamini tena, hasa kwa sababu niliamini ilikuwa Mungu aliyemchukua mama yangu kutoka kwangu. Hata kama sikujua kile Yeye alichomaanisha, nilijihisi salama.
Miaka mitatu baadaye nilienda Roma, Italia, kumtembelea mjomba wangu. Alishinda akinielezea kuhusu kanisa analoshiriki. Jumapili moja, tuliambatana naye. Nitakumbuka daima nikitembea kuelekea kwenye milango ya kanisa mara ya kwanza na hisia ya upendo wa Baba wa Mbinguni wakati nilipoingia ndani. Ilihisi kama nyumbani.
Nilianza kwenda Kanisani kila Jumapili na kila shughuli wakati wa wiki. Nilifurahia kuwa na vijana wa Kanisa. Walinifanya kuwa na furaha sana. Walifikiria na kuamini katika mambo sawa sawa na yale yale kama mimi. Baada ya miezi mitatu, likizo yangu ya majira ya kiangazi ilikwisha na ilibidi nirudi Albania.
Niliporudi nyumbani, nilimwelezea baba yangu kuhusu hisia nilizokuwa nazo na ile furaha niliyohisi wakati huo. Hakufurahia hayo. Aliniambia kuwa hangekubali niendelee kwenda kanisani wala kujifunza zaidi kuhusu kanisa hilo. Kwa hivyo ingenibidi niwe na subira kwa muda wa miaka mitatu iliyokuwa mbeleni hadi wakati ningehitimu miaka 18. Kisha ningeweza kujiamulia na kubatizwa.
Wakati huu nilibarikiwa na watu wengi ambao walinielezea kuhusu walichojifunza kila Jumapili Kanisani. Mmojawapo wa watu wale ilikuwa Stephanie. Alikuwa akiishi Italia wakati mjomba wangu alipojiunga na Kanisa, lakini alikuwa amerudi nyumbani kwao Marekani. Mjomba wangu alifikiri ingekuwa vizuri kwetu kuwasiliana na kila mmoja wetu, kwa hivyo nilimwongeza kama rafiki katika mtandao wa Facebook.
Hata kama hutukuwa tumewahi kukutana katika nafsi zetu, nitakuwa na shukrani daima kwa kunisaidia kujenga imani yangu na kujifunza zaidi kuhusu injili ya Yesu Kristo. Aliniandikia karibu kila Jumapili na kunieleza kila kitu alichojifunza kanisani na kisha angejibu maswali yangu. Alikuwa rafiki mzuri kwangu.
Hatimaye, baada ya miaka ya kuwa na subira, nilibatizwa siku mbili tu baada ya siku yangu ya 18 ya kuzaliwa. Na karibuni nitamsimulia mamangu ile furaha niliyohisi siku ile, kwa sababu nitabatizwa kwa niaba yake. Ninajua atakuwa mwenye fahari kwa ajili ya maisha niliyochagua.
Ninahisi nimebarikiwa na Baba wa Mbinguni kwa sababu alikuwa pamoja nami safari hiyo yote kwa njia yingi sana. Nilihitaji tu kuwa na subira kwa sababu alikuwa na mpango kwangu. Ni Yeye aliyenipa nguvu za kupitia shida zote nilizokabiliana nazo. Alikuwepo kila mara, akinisaidia kuwa na furaha zaidi.