Jifunze Kucheza Wimbo wa Kidini katika Dakika 10!
Kama haujawahi kucheza kinanda hapo awali lakini daima umekuwa hamu ya kujifunza, hii ndiyo nafasi yako. Kile unachohitaji tu ni kinanda cha muziki. Hata kama hauna nyumbani, unaweza kuchukua makala hii na kwenda nayo hadi mahali ambapo kuna piano au kinanda ili uanze kujifunza.
Somo hili ni rahisi sana na jepesi kiasi kwamba utaweza kucheza wimbo wa injili mwishoni. Kwa kweli, inawezekana wewe kucheza melodi ya wimbo wa injili katika somo hili kwa takriban ndani ya dakika 10!
Tayari? Acha tuanze!
Kujitayarisha Kucheza Kinanda
-
Unapoketi karibu na kinanda na kuweka vidole vyako kwenye kiibodi, sogeza benchi nyuma kiasi kwamba viwiko vyako viwe vimejikunja kidogo tu.
-
Keti katikati ya benchi, lililo katikati ya kiibodi.
-
Keti upande wa mbele kabisa wa benchi hilo na mgongo wako ukiwa wima.
-
Pumzisha miguu yako sakafuni.
-
Keti starehe, ukidumisha mkao mzuri.
-
Hakikisha kuna mwangaza mzuri ili uweze kuona kitabu cha muziki na kiibodi.
-
Simama. Teremsha mikono yako pembeni mwako na uipumzishe. Angalia mkunjo wa asili wa mikono yako, kana kwamba imeshikilia mpira. Unapoketi tena, weka vidole vyako kwenye kiibodi ukidumisha mkunjo wake wa kawaida.
-
Weka mikono yako juu ya kiibodi, ukiacha vidole vyako viguse karibu katikati ya mahali pale pakubwa palipo na vibonyezo vyeupe. Shikilia viganja vyako juu ya kiibodi, lakini usiviweke juu ya vibonyezo au mbao iliyoko chini ya vibonyezo.
-
Bonyeza kibonyezo kwa pedi ya kidole chako chini tu ya ncha ya kidole. Kunja kila kidole chako, ukikiinua kutoka kifundo nyuma ya mkono wako. Unapobonyeza kibonyezo, dumisha viungo vyako vya kidole vikiwa vimekunjwa.
Kucheza kwa Kutumia Nambari za Vidole
Ili kukusaidia kuweka kidole sahihi juu ya kila kibonyezo, vidole vimepewa nambari kama ilivyoonyeshwa hapa. Nambari za vidole zimeandikwa karibu na noti kwenye ukurasa.
Weka mkono wako juu ya na kundi lo lote la vibonyezo vitano, ukishikilia kila kidole juu ya kibonyezo kimoja. Fanya mazoezi ya nambari za vidole kwa kucheza vibonyezo kwa kidole sahihi kama ilivyoonyeshwa. Noti zilizo na mashina yanayoenda juu ni za mkono wa kulia. Noti zilizo na mashina yanayoenda chini ni za mkono wakushoto.
Kucheza “Kuna Mlima wa Kijani Mbali”
Weka mikono yako kwenye kinanda ilivyoonyeshwa chini.
Tumia makundi mawili na matatu ya vibonyezo vyeusi ili kukusaidia kupata mahali sahihi.
Cheza wimbo huu wa injili, ukifuata nambari za vidole kama ilivyoonyeshwa. Noti zilizo na mashina yanayoenda juu ni za mkono wa kulia, na noti zenye shina manayoenda chini ni za mkono wa kushoto. Fanya mazoezi ya wimbo huu wa injili hadi uzoee. Tumia kanuni rahisi za mbinu za kubonyeza zilizoorodheshwa katika orodha ya hoja tisa.
Sasa umetambulishwa katika kucheza kinanda na umejifunza melodi rahisi ya wimbo wa injili. Kucheza nyimbo nyingine za injili, unahitaji kujifunza kanuni kadhaa za msingi kuhusu vipimo vya muziki, sauti, na noti.
Hii ndiyo sehemu bora zaidi: somo ambalo umejifunza tu hivi sasa ni somo la kwanza katika Kozi ya Kiibodi ya Kanisa, inayopatikana katika lugha sita kutoka idara ya Kanisa ya Usambazaji.1 Mpango huu wa maelekezo yaliyo rahisi kufuata unakusaidia kujifunza peke yako au kwenye vikundi. Unaweza hata kushirikisha familia yako nzima katika kujifunza kucheza kinanda kama shughuli ya mkutano wa jioni ya familia nyumbani. Kozi hii inaweza kukamilishwa katika muda wa wiki sita tu.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa masomo ya muziki kibinafsi husaidia kuimarisha malengo ya wanafunzi, kuboresha msimamo wa kitaaluma na ujuzi wa kufikiri mambo yenye kujenga hoja.2
Kwa kujifunza ujuzi wa kucheza muziki, tunakuza vipaji ambavyo Mungu ametupa, tunaongeza maarifa yetu, na kujifunza njia tofauti ambazo tunaweza kutumia maarifa na vipaji hivyo kujenga Ufalme wake.