Wamisionari Wakuu: Hitajika, Barikiwa, na Pendwa
Kuhudumu misheni kama wanandoa inaweza kuwa rahisi, sio ghali sana, na kuleta furaha zaidi kuliko unavyodhania.
“Unaweza kuja kusaidia?”
Ni swali ambalo Gerald na Lorna Malmrose wa Washington, Marekani, walikuwa wamewahi kulijibu mbeleni. Walisema ndio wakati aliyekuwa askofu wao, wakati huo rais wa misheni, aliuliza ikiwa wangeweza kuhudumu naye kule West Indies. Walisema ndio tena wakati rais wao wa kigingi aliwaitia mwito wa kutekeleza misheni ya huduma katika makao makuu ya Kanisa kule Salt Lake City, Utah, Marekani, wakishughulikia tarakilishi na raslimali ya watu.
Wakati ambapo aliyekuwa askofu wao na rais wa misheni, Reid Robinson, aliwaita tena, wakati huu akiwa rais wa kituo cha mafunzo cha mmisionari kilichoko Accra, Ghana, aliwauliza kina Malmroses ikiwa wangeweza kusaidia mara nyingine.
“Tulijua tungeweza kumwamini Bwana,” Mzee Malmrose anasema. “Kwa hivyo tuliamua kumwamini tena.” Walisema ndio, wakajaza fomu za mapendekezo, wakapokea mwito, na punde walikuwa kule Ghana.
Kuhudumu kama Wanandoa
Uzoefu wa kina Malmrose unaonyesha kanuni kadhaa kuhusu wanandoa wazee wanaohudumu misheni ambazo hazieleweki sana.
-
Kuna misheni za aina mbili. (1) Rais wa Kanisa huwaita wanandoa wazee kuhudumu kutoka nyumbani kwao ama mbali kutoka nyumbani. (2) Rais wa kigingi huwaita wamisionari wanandoa wa huduma ya Kanisa kutimiza mahitaji ya eneo lao kwa muda maalum, kati ya saa 8 hadi 32 kila wiki. Kawaida huwa wanaishi na kuhudumu katika eneo lao lakini mara nyingine wanaweza kuhudumu mbali na nyumbani.
-
Marais wa misheni wanahimizwa kutafuta wanandoa ambao wanaweza kutosheleza mahitaji katika misheni zao, na wanandoa wanaweza kudokeza mapendeleo yao. “Hatusemi kuwa wanandoa wanaweza kuteua na kuchagua miito yao ya misheni,” anaeleza Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Mwito bado ni mwito. … [Lakini] tunazungumza na wanandoa wetu wazee kuhusu mapendeleo yao ya huduma, na kila uzingatio unafanywa kuwaruhusu kuhudumu mahali na jinsi wanataka kuhudumu.”1
-
Marais wa misheni hushauriana na wanandoa kuhusu jinsi wanavyoweza kutumia ujuzi na uwezo wao. “Kuwa na uzoefu wa maana kama wanandoa wakubwa,” Rais Robinson anasema, “unahitaji kuwa na nafasi ya kufanya kazi unayoipenda na maeneo ambayo una ujuzi kiasi cha kukufanya uhisi kuwa unahitajika.”
Kwa mfano, Rais Robinson alifahamu kwamba Mzee Malmrose anajua kuzungumza Kifaransa, ina manufaa kwa sababu Waafrika wengi huzungumza Kifaransa. “Nilikuwa na maono akihusika na usafiri na kushughulikia viza,” Rais Robinson anasema. “Lakini wakati aliwasili hapa, nilihisi kuwa huo haukuwa mvuto wake halisi. Kwa hivyo nilimualika atumie ujuzi wake wa tarakilishi. Ametuokolea masaa mengi, mengi sana.” Mzee Malmrose pia husaidia wamisionari, hasa wamisionari wanaozungumza kifaransa, kutayarisha majina na kufanya kazi ya hekalu kwa niaba ya familia zao. Dada Malmrose, msaidizi wa matibabu aliyesajiliwa, alikuwa na jukumu la kufanya kazi na daktari na muuguzi wa misheni.
Yeye Hutayarisha Njia
Kama kina Malmrose, wanandoa wengine wanagundua kuwa wanapomwamini Bwana, Yeye hutayarisha njia. Hilo ndilo lililowafanyikia Alvin na Corazon Rieta wa Kawit, Cavite, kule Ufilipino.
“Miaka miwili kabla ya uamuzi wetu wa kuhudumu, tulianza kuweka mipango imara kwa ajili ya biashara ya familia yetu,” Mzee Reita anaeleza. “Mwana na binti yetu walikuwa wamehitimu kutoka chuo kikuu na wangeweza kuchukua usukani kutoka kwetu, lakini tulijiuliza ni nani angesuluhisha shida za kibiashara na wateja wetu wangeona namna gani kuhusu mipango yetu.”
Dada Reita pia alikuwa na wasiwasi kuhusu kumuacha mamake mzee. “Nilikuwa na hofu kuwa tungempoteza tukiwa tungali mbali,” anasema. “Pia nilijisikia mpungufu kwa mwito wa kwenda kufundisha injili.”
Walifanya mashauriano na askofu wao na wanandoa ambao karibuni walikuwa wamehudumu kule Davao. “Wote walitoa ushuhuda wa nguvu kuwa Bwana angeongoza kila wanandoa kujua namna ya kushughulikia mambo yao ya nyumbani, na familia zao, na mahitaji yao ya kifedha ya misheni zao,” Dada Reita anasema.
“Tulipokuwa tukitafuta mwongozo,” Mzee Reita anasema, “hofu zetu zilishughulikiwa—biashara yetu iliendelea vizuri licha ya changamoto, wateja wetu walionyesha furaha na kutuunga mkono, na familia yetu ilikuja pamoja kwa kumchunga mama yetu mgonjwa. Tulianza kuelewa kuwa kwa kweli Bwana angetusaidia.”
Kina Reita sasa wanahudumu katika usaidizi wa washiriki na viongozi kule Ufilipino katika Misheni ya Cagayan de Oro.
Ni Mengi Unayoweza Kufanya
Wanandoa wengine huwaza kuhusu ufinyu wa viungo, lakini siyo Keith na Jennilyn Mauerman wa Utah, Marekani. Miaka kadhaa iliyopita, miezi minne baada ya kufunga ndoa katika hekalu la Los Angeles California, Keith alisajiliwa na kutumwa katika vita. Kiongozi wa kikosi cha wanahewa, alikuwa akitembea mbele ya wanajeshi wengine wakati bomu la kutegwa ardhini lilipuka. Alipoteza miguu yote. Alipowasili nyumbani, Jennilyn alikimbia pembeni kwake.
“Nilijua sikuhitaji kuwa na wasiwasi,” Keith anasema, “kwa sababu tuna ndoa ya milele. Bibi yangu amenisaidia huu muda wote. Bado angali ananihimili kila siku.”
Wakati ambapo Dada Mauerman alistaafu, tuliamua kuhudumu misheni. Lakini hali ya Mzee Mauerman kukatwa viungo viwili vya mwili inaleta tashwishwi? “Sikuzote kuna mambo siwezi kufanya,” anasema, “lakini kuna mambo mengi sana ninayoweza kufanya, tulijua kungekuwepo na nafasi kwetu.”
Walipokuwa wakijaza fomu zao za mapendekezo, alichagua sehemu iliyoonyesha kuwa alikuwa amehudumu katika jeshi. Punde walipokea simu kutoka Ofisi ya Kanisa ya Uhusiano wa Kijeshi. “Nilikuwa na Kitambulisho ambacho kingetuwezesha kuingia katika kambi za kijeshi, kwa hivyo walituuliza idhini ya kutupendekeza kuhudumu misheni ya uhusiano wa kijeshi.”
Bwana na Bi Mauerman walipewa mwito katika kambi ya kijeshi kule North Carolina, Marekani. Mzee Mauerman anakumbuka: “Ishara iliyokuwa kwenye lango ‘Fort Bragg, Nyumbani kwa Wanajeshi wa Angani.’ Wakati mlinzi alipotusalimia kwa wito wa wanajeshi wa angani ‘Pita Ndani!’ ilikuwa mara ya kwanza nilikuwa nimeisikia kwa miaka mingi. Nilijihisi nyumbani, hata kama sikuwa nimeshawahi kuwa Fort Bragg. Nilijua misheni yetu ilitufaa kikamilifu na kuwa Bwana alinijali.”
“Tulifundisha masomo kuhusu kujitegemea na kuwa imara na kuhusu kuimarisha ndoa,” Dada Mauerman anasema. “Mwanzoni hatukuwa tunataka kushiriki simulizi yetu, lakini tuligundua kuwa kuishiriki kulileta tofauti kubwa. Wanajeshi na wapenzi wao walitutazama na kusema, ‘Ikiwa mnaweza fanya hivyo, pia sisi tunaweza.’”
Kina Mauerman walikuwa na tukio chanya kule North Carolina kiasi cha kuwa walitaka kuhudumu tena. Siku hizi wao husafiri takriban maili 40 (64 km) kutoka nyumbani kwao kule Orem hadi Mji wa Salt Lake mara mbili kwa wiki kwenda kuhudumu katika Ofisi ya Kanisa ya Uhusiano wa Kijeshi. Wao pia huwafunza wanandoa wamisionari katika kituo cha mafunzo kule Provo, ambako wanagundua kuwa karibu tu kila kikundi kinajumlisha mtu ambaye amepambana na vikwazo ili kuweza kuhudumu.
Lugha za Ulimwengu Mzima
Waliitwa katika Misheni ya Brazil Cuiabá, Randy na Lou Ellen Romrell wa Utah walikuwa na wasiwasi. Ingawaje Mzee Romrell alikuwa amehudumu kule Brazili kama mmisionari akiwa kijana, alikuwa kidogo amesahau Kireno. Na Dada Romrell hakuelewa kireno. Kusoma na jitihada, hata hivyo, ilisaidia ujuzi wa Mzee Romrell kurejea na wa Dada Romrell kuimarika. Na hata wa ukulele.
“Sikuwa na mpango kamili wa kuileta,” Dada Romrell anasema, “lakini Mzee Romrell alikuwa na msukumo wa kufanya hivyo, na ni ajabu kuona kile ambacho imefanya. Tunapowafundisha wachunguzi na kushughulikia kurejesha katika uhudhuriaji kamili na ushirika, ni furaha kuitumia kufanya watu waimbe nyimbo za kidini. Tunajifunza lugha, na nyimbo za kidini huleta roho wa nguvu pamoja nazo.”
Hata kama ujuzi wake wa Kireno bado ungali unakua, Dada Romrell tayari ni mweledi katika muziki. “Muziki huleta watu pamoja,” anasema. “Hata kama siwezi kuelewa kila wanachosema tunapowatembelea, tunapoimba, tunaungana.” Walipoalikwa kuzungumza shuleni kuhusu sikukuu ya Marekani ya Kutoa Shukrani, kina Romrell waliimba nyimbo za kidini za kutoa shukrani—ikipambwa na ukulele. Na Dada Romrell pia hutumia ala ya muziki ya kawaida, kinanda, kupamba nyimbo za kidini kanisani.
Na Kireno? “Hata ikiwa wewe si mweledi, kujifunza maneno machache kunasaidia,” anasema. “Kwa kusema tu jambo na kuwasalimia watu kuna umuhimu mkubwa sana. Wajulishe kuwa unajifunza. Ifanya iwe rahisi na mtegemee Roho.” Na Roho, kama ilivyo, ni lugha nyingine ambayo kila mtu anaweza kushiriki.
Kuhudumu Nyumbani
Paul na Mar Jean Lewis kutoka Utah walikuwa tayari wamehudumu misheni tatu pamoja (Hekalu la Palmyra New York; Hekalu la Hong Kong Uchina; Serbia, na Slovenia na vyuo). Walikuwa wakijitayarisha kuhudumu misheni nyingine wakati rais wao wa kigingi aliuliza, “Mnaweza kuwa na hamu ya kuhudumu papa hapa katika kigingi chetu, mkisaidia misheni tunamoishi?”
“Sisi ni wageni hapa, kwa hivyo ilikuwa nafasi nzuri sana,” Dada Lewis anasema. “Tunahudumu na wale vijana wazee wamisionari na kina dada, tuna uhusiano wa karibu na rais wa misheni, huwa tunahudhuria mikutano ya wilaya na zoni, na tunafanya kazi na viongozi wa kata wa umisionari.” Wao pia huwatembelea wachunguzi na wale ambao hawahudhurii kikamilifu.
“Tumekutana na watu wazuri sana ambao hatungeweza kupata kuwajua kwa njia nyingine,” Dada Lewis anasema, “pamoja na wale ambao wamepotea njia. Kuwaona wakirudi, wakipokea maagizo, na kwenda katika hekalu ni baraka kubwa.”
“Wanandoa wengi, wanapofikiria kuhusu kuhudumu misheni, wana wasiwasi kuhusu kile watakachofanya na nyumba yao, gari lao au watakachokosa katika familia zao,” Mzee Lewis anasema. “Tumeweza kuishi nyumbani kwetu na kuendesha gari letu. Tunatiwa moyo kuhudhuria shughuli za familia, muradi tu zisiingiliane na majukumu yetu ya kimisionari. Na hata tulikuwa hapa kwa kuzaliwa kwa mjukuu wetu.”
Baraka za Familia
Kwa upande mwingine, Jill na Kent Sorensen, ambao wanatoka katika kigingi hicho pia wanasema mojawapo ya njia mwafaka za kuimarisha familia yao imekuwa kuhudumu mbali na nyumbani. Dada Sorensen anasema, “Mojawapo ya visingizio vikuu ambavyo wanandoa hutoa kama sababu ya kukosa kwenda ni wajukuu, watoto waliofunga ndoa na walio na matatizo, mabinti wanaotarajia kujifungua, wazazi wakongwe—unaweza kuvitaja. Familia ni kipaumbele, na unawakosa kila siku. Lakini kuhudumu misheni kunatoa ujumbe wa nguvu kuwa kazi ya umisionari ni muhimu pia.”
Kando na, Mzee Sorensen anasema, “kuna njia nyingi sana za kuwasiliana kwa vile hivi sasa waweza kuwajulia hali wakati wowote.”
Safari ya kina Sorensen ya umisionari ilianza miaka mitatu iliyopita, wakati askofu wao aliwauliza kuandaa mikutano ya mafunzo kila mwezi kwa ajili ya wanandoa ambao wana dhana za kutoa huduma ya umisionari. “Baada ya kuizungumzia kila mara,” Dada Sorensen anasema, “ilibidi twende sisi wenyewe!” Walipokea mwito wa kuhudumu katika Visiwa vya Cook, ambako mababu wa Jill walihudumu miaka 50 iliyopita.
Siku hizi, miongoni mwa majukumu mengine, wameombwa kufundisha masomo ya Biblia katika shule.
“Sisi huzungumza kumhusu Kristo akiwa mwamba,” Mzee Sorensen anasema. “Sisi huwapa wanafunzi mawe ndogo kuwasihi wabaki imara kama mwamba katika Kristo. Sasa kila tuendapo, watu husema, ‘Imara kama Mwamba!’ Wakati wanapotuona.”
Njoo Utoe Msaada
Ikiwa una dhana za kuhudumu misheni kamilifu au misheni ya huduma ya Kanisa, kila mmoja wa wanandoa hawa watakuuliza swali kama lile ambalo Rais Robinson aliwauliza Gerald na Lorna Malmrose: “Mnaweza kuja kusaidia?” Na watakueleza kuwa, haijalishi jinsi unavyoshiriki, ahadi hii ni ya kweli: Mnahitajika, mnaweza kuchangia, na mtabarikiwa na upendo.