2016
Kupima Baraka huko Madagaska
Aprili 2016


Maelezo Mafupi Kuhusu Vijana Wazima

Kupima Baraka huko Madagaska

Licha ya mageuzi makubwa ya kisiasa na hali ngumu za kiuchumi nchini mwake, Solofo anategemea baraka zinazotokana na kuishi kulingana na injili.

lemur and baobab tree

Picha: ya juu imetolewa na Solofo Ravelojaona; ya chini © iStock/Thinkstock

Baada ya mkewe kuteseke kutokana na kuharibika kwa mimba yao ya kwanza, Solofo Ravelojaona alihisi kuwa maombi yao yalijibiwa mwaka mmoja baadaye kwa mimba yao ya pili. Yeye na mkewe, Hary Martine, wanachukulia kuzaliwa kwa binti yao kuwa mojawapo ya baraka zao kubwa zaidi. Solofo anaeleza, “Kwa sababu tulimwomba Mungu na akatupatia, tulimpatia jina ambalo, kwa Kimalagasi, linamaanisha ‘jibu la Mungu.’”

Solofo with his daughter

Solofo, kijana mkubwa kutoka Madagaska, anaamini kuwa Mungu hujibu maombi na kwa wakati wake anawabariki waaminifu. “Maisha ni magumu,” anasema Solofo, “na wakati watu wanapokosa kupata kile wanachotaka, wengine huanza kujiuliza, ‘Ni kwa nini hili limenitokea?’ Wanaweza kuacha Kanisa au kuwa na shaka na imani yao kwa Mungu. Lakini tunapoishi kulingana na injili na kusoma maandiko, inakuwa rahisi. Unapoishi kulingana na injili, kwa kweli unaweza kuona baraka.”

Kuishi katika nchi yenye shida kubwa, kama vile umaskini uliokithiri, kukosekana kwa utengamano serikalini, miundombinu dhaifu, na maafa, ni wazi kwa nini Solofo anasema maisha ni magumu. Lakini kwake, baraka ambazo kuishi kulingana na injili huleta zinashinda taabu zozote. “Siwezi hata kuhesabu baraka ambazo ninapokea, muradi tu ninaishi kulingana na injili,” anasema.

Kwa sababu Kanisa bado geni Madagaska (tawi la kwanza lilifunguliwa 1990), Solofo anasema kuwa sehemu ngumu zaidi ya kuwa muumini ni uvumi na kueleweka visivyo kwa Kanisa. Solofo anatoa maoni kuwa, kama vile ilivyokuwa katika maono ya Lehi ya mti wa uzima, “watu wanaweza kukosa kukubali injili kikamilifu kwa sababu wanaona aibu mbele za marafiki na wanaogopa kuwa watakataliwa na familia zao.” Kinachomfanya Solofo kuwa tofauti, anapendekeza, ni kuwa, “Sijawahi kuona aibu.” Ninaishi kulingana na injili, na kila mara mimi hutaka kushirikiana na wenzangu kazini, hata kama baadhi yao hawana moyo wa kutaka kujua.” Mara nyingi yeye hushiriki na wengine ushuhuda wake, kiasi cha kuwa wafanyikazi wenzake wamempa jina la utani la “mchungaji.”

Solofo and Hary Martine

Katikati ya mtikisiko wa kiuchumi na kisiasa, Solofo na Hary Martine wanategemea baraka za maagano yao ya hekalu (walifunga ndoa katika Hekalu la Johannesburg Afrika Kusini mwaka mmoja baada ya misheni zao—yake Uganda, na ya mkewe Madagaska), na pia imani yao kwa Bwana. “Nina injili, na mimi huweka tu maisha yangu mikononi mwa Mungu,” Solofo anaeleza. Anaweza kutegemea ushuhuda wake imara kwa sababu tayari ana imani katika “majibu ya Mungu.”