Kuwa Imara Kiroho Kujenga Meli Isiyoweza Kuzama
Kutoka Ibada katika Chuo Kikuu cha Brigham Young, Sept. 16, 2014. Kwa nakala nzima katika Kiingereza, tembelea speeches.byu.edu.
Tunahitaji msimamo imara wa kiroho wa kutosha ili tuweze kuishi maisha yetu ya sasa kwa ufanisi na kuweza kurudi salama nyumbani kwetu mbinguni.
Mapema katika karne ya 17, Mfalme wa Uswidi, Gustav II Adolf, aliagiza kutengenezwa kwa meli ya kivita ambayo ingepewa jina Vasa. Meli hiyo ilileta taswira ya rasilimali nyingi, hasa mwaloni ambao ungetumika katika ujenzi wa chombo hicho. Gustav Adolf alisimamia kwa karibu sana ujenzi wake, akijaribu kuhakikisha kwamba Vasa ingefanikisha kikamilifu matumaini yake.
Baada ya ujenzi kuanza, Gustav Adolf aliamuru Vasa iwe ndefu zaidi. Kwa sababu nguzo za upana zilikuwa tayari zimejengwa kwa kutumia mwaloni wenye thamani, mfalme alielekeza kwamba wajenzi waongeze urefu wa meli bila kuongeza upana wake. Ingawaje waunzi walijua kuwa kufanya hivyo kungetia Vasa hatarini, walisita kumwambia mfalme jambo ambalo walijua hakuwa anataka kusikia. Walifanya alivyotaka. Gustav Adolf pia alisisitiza kuwa meli hii isiwe tu na staha moja ya mizinga bali mizinga kwenye staha tatu, na mizinga kubwa kabisa kwenye staha iliyokuwa juu kabisa. Tena, kinyume na busara yao, waunzi walifanya alivyotaka.
Agosti 10, 1628, Vasa ilianza safari yake ya kwanza. Baada ya Vasa kuondoka bandarini, upepo mkali ulipuliza tanga zake, na meli ikaanza kuinama. Baada ya muda sio mrefu, “ilianza kuinama kwa upande na maji yakaanza kuingia kwa kupitia madirisha madogo ya mizinga hadi ikazama polepole chini ya tanga, bendera ya kuashiria meli na kila kitu.”1 Safari ya kwanza ya Vasa ilikuwa takriban futi 4,200 (1,280 m).
Matamanio ya Gustav Adolf ya kuwa na ishara ya hadhi ya ubadhirifu iliharibu ruwaza ya kile ambacho kingekuwa chombo kizuri sana cha baharini, meli yenye uwezo mkubwa sana ya kivita kwa wakati wake. Kusita kusema kwa waunzi—hofu yao juu ya hasira ya mfalme—kulimnyima mfalme maarifa na umaizi wao. Wale wote waliohusika walisahau malengo ya shughuli ile: kulinda Uswidi na kukuza maslahi yake kule ng’ambo. Meli ambayo inajaribu kwenda kinyume na sheria za fizikia ni jahazi tu ambalo haliwezi kuelea.
Tunahitaji msimamo imara wa kiroho wa kutosha ili tuweze kukabiliana na dhoruba na mikondo kutoka pande zote, ili tuweze kuishi maisha yetu ya sasa kwa ufanisi, kufanya marekebisho yanavyotakikana, na kuweza kurudi salama nyumbani kwetu mbinguni. Kuna mambo ambayo tunaweza kufanya ili tuzidi kuwa imara kiroho. Nitagusia manne.
Kutii Amri za Mungu
La kwanza ni kutii amri za mungu. Jinsi tu Vasa ilitawalwa na sheria za fizikia, sote tunatawaliwa na sheria za kiroho. Hakuna aliyesamehewa kutoka kwazo. Tunahitaji kutii sheria hizi za kiroho, ambazo twaziita amri za Mungu.
Kufanya kazi na sheria za fizikia katika ujenzi wa meli ile kunaweza kuwa kulionekana kuwa na vizuizi kwake Gustav Adolf, lakini Vasa haingezama kabla ya misheni yake kama ingefuata sheria hizo. Badala yake, ingekuwa na uhuru na urahisi wa kutimiza kile ambacho ilipaswa kufanya.
Kwa hivyo, pia, utiifu kwa sheria za Mungu unahifadhi uhuru wetu, urahisi, na uwezo wa kutimiza uwezo wetu. Amri hazijadhamiriwa kutuzuia. Badala, utiifu unaongoza hadi ongezeko la imarisho la kiroho na furaha ya kudumu.
Utiifu ni chaguo letu. Yesu alielekeza, “Tazama, nimewapatia amri; kwa hivyo tiini amri zangu” (3 Nephi 15:10). Ni rahisi hivyo. Fanya uamuzi. Amua kuwa mtiifu kikamilifu. Hakuna kinachoweza kuzidisha kuwa imara kiroho zaidi. Hakuna kinachoweza kutupa uhuru mkubwa kutimiza lengo la maisha.
Kufuata Ushauri na Kuwa Wanafunzi Maisha Yetu Yote
Pili, tunahitaji kuzingatia na kufuata ushauri kutoka vyanzo aminifu na kujitolea kuwa wanafunzi maisha yetu yote.
Mojawapo ya shida za kupata maarifa ni kiburi ambacho kinaweza kuja tunapofikiri tunajua sana kiasi cha kuwa hakuna tunachoweza kujifunza tena. Sote tumeyaona haya kwa wale watu ambao wanaamini sana werevu wao. Ni vigumu sana kumfundisha mjua yote.
Akizingatia haya, na akiwa mwenye kutaka kuwa mwanafunzi maisha yake yote, Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alisema, “mimi bado ningali mtoto na kuna mengi ya kujifunza. Watu wengi wanaweza kunifundisha kitu.”2 Wakati aliponipa mwito wa kuwa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka, Rais Eyring alinifundisha somo muhimu sana. Alisema kuwa anaposikia mtu akisimulia hadithi ambayo ameisikia mbeleni au akitumia maandiko ambayo anayafahamu vizuri sana, anajiuliza, “Ni kwa nini Bwana ananisisitizia haya?” na “Ni kipi naweza nikajifunza tena kutoka kwa simulizi hiyo au maandiko hayo?” Ikiwa tunataka kuzidi kuwa imara kiroho, tutakuwa tayari kujifunza na tutakuwa wanyenyekevu kiasi cha kutosha kukubali kuongozwa bila ya kujali umri na tajriba yetu.
Utiifu ni chaguo letu kweli. Tunaweza kusikiliza na kufuata ushauri tunaopewa na viongozi wa Kanisa, hasa wale tunaoidhinisha kama manabii, waonaji, na wafunuzi; kutoka kwa wazazi; na kutoka kwa marafiki waaminifu—au la. Tunaweza kutaka kuwa wanafunzi maisha yetu yote—au la. Tunaweza kuzidisha kuwa kwetu imara—au la. Tukikosa kuzidisha kuwa imara kiroho, tutakuja kuwa kama Vasa—jahazi ambalo haliwezi kuelea.
Kuhudumia Wengine
Tatu, kuelekea kutoka ndani kwenda nje, kuwajali wengine, na kuwahudumia wengine kunazidisha kuwa kwetu imara kiroho.
Milele inazidi kuonekana waziwazi wakati tunapowalenga wengine na kutafuta kuwasaidia watoto wa Baba wa Mbinguni. Nimepata kuwa ni rahisi kwangu kupokea msukumo wakati ninapoomba ili nijue jinsi ninaweza kumsaidia mwingine kuliko wakati ninapojiombea tu binafsi.
Tunaweza kuamini kuwa mahali fulani kwa siku zijazo tunaweza kuwa katika hali njema ya kusaidia. Hakika, wakati ni sasa. Tumekosea ikiwa tunadhani kuwa itakuwa rahisi wakati tutakuwa na muda zaidi, pesa zaidi, au chochote zaidi cha kuwahudumia wengine. Bila ya kujali hali, tuna chaguo. Tutawasaidia wengine au la? Tunaanguka mtihani muhimu sana wa maisha ya sasa ikiwa hatutachagua kuwasaidia walio na shida. Na, ikiwa tutatoa msaada, tunazidi kuwa imara kiroho.
Tumfanye Yesu Kristo Msingi Wetu
Nne, hatimaye, na la muhimu zaidi, kuwa kwetu imara kiroho kunazidi kwa uwiano na kiasi ambacho tunamfanya Yesu Kristo kama msingi wetu.
Bila Kristo, tunaelekezwa kama chombo kinachoyumba yumba kwenye mawimbi. Hatuna nguvu kwa sababu hatuna tanga. Hatuna uthabiti, hasa nyakati za dhoruba, kwa sababu hatuna nanga. Hatuna mwelekeo au malengo kwa sababu hatuna chochote ambacho twaweza kutumia kuelekeza. Ni lazima tumfanye Kristo msingi wetu.
Ili tuweze kukabiliana, kushinda, na tuwe tayari kwa upepo mkali wa pembeni na mikondo ya maisha inayogongana, tunastahili kutii amri za Mungu; tuwe wanyenyekevu, radhi, na wasomi jasiri maisha yetu yote; kuwahudumia wengine; na kumfanya Yesu Kristo kama msingi wa maisha yetu. Tufanyapo haya, tunazidi kuwa imara kiroho. Tofauti na Vasa, tuna uwezo wa kurudi katika bandari salama, tukiwa tumetimiza hatima yetu.