Ujumbe wa Mwalimu Mtembeleaji
Mabinti wa Baba yetu wa Milele
Kwa maombi jifunze maneno haya na utafute kujua kitu cha kufundisha. Ni jinsi gani kuelewa “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” kutazidisha imani yako kwa Mungu na kubariki wale unaowachunga kupitia Ualimu wa Kutembelea? Kwa taarifa zaidi, nenda kwenye reliefsociety.lds.org.
Maandiko yanatufundisha kuwa “sisi tu wazao wa Mungu” (Matendo ya Mitume 17:29). Mungu alimtaja Emma Smith, mke wa Nabii Joseph Smith kama, “binti yangu” (M&M 25:1). Tangazo la familia linatufundisha kuwa kila mmoja wetu “ni binti mpendwa wa kiroho … wa wazazi wa mbinguni.”1
“Katika maisha [kabla ya kuzaliwa], tulijifunza kuhusu utambulisho wetu wa milele wa kike,” alisema Carole M. Stephens, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama.
“Safari yetu duniani haikubadilisha kweli hizo.”2
“Baba yako wa Mbinguni anajua jina lako na anajua mazingira yako,” alisema Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. “Yeye husikia maombi yako. Anajua matumaini na ndoto zako, pamoja na hofu yako na kuvunjwa moyo kwako.”3
“Kila mmoja wetu ni wa familia ya Mungu na anahitajika katika familia hiyo ya Mungu,” alisema Dada Stephens. “Familia za duniani zote zinaonekana kuwa tofauti. Na tunapofanya vyema kadiri tuwezavyo kuunda familia za kawaida zilizo imara, ushiriki katika familia ya Mungu hautegemei hadhi ya aina yoyote—hali ya ndoa, hali ya uzazi, hali ya kifedha, hali ya kijamii, au hata aina yoyote ya hali tunayoweka kwenye mtandao wa kijamii.”4
Maandiko ya Ziada
Kutoka katika Historia Yetu
Katika Historia yake ya Ono la Kwanza,5 Nabii Joseph Smith anathibitisha ukweli mwingi—ikijumuisha kwamba Baba wa Mbinguni anajua majina yetu.
Kijana Joseph alihangaika ili apate kujua ni kanisa gani angejiunga nalo na alipata mwongozo katika Yakobo 1:5. Joseph alihitimisha kwamba angemwomba Mungu.
Asubuhi moja wakati wa majira ya kuchipua mwaka wa 1820, alienda msituni kuomba lakini mara akashikwa na nguvu fulani za giza. Juu ya haya aliandika:
“Katika wakati huu wa hofu kubwa, niliona nguzo ya mwanga juu ya kichwa changu, ambao ulikuwa na mng’aro uliozidi mwangaza wa jua, ambao ulishuka taratibu hadi ukashuka juu yangu.
“Mara ulipoonekana nilijikuta kuwa nimekombolewa kutokana na adui yule aliyenifunga. Mwanga ulipotua juu yangu nikawaona Viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (Joseph Smith—Historia 1:16–17).