Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Wafundishe Kusoma Kitabu cha Mormoni
Emilien Rioux, Quebec, Canada
Wakati tulipokuwa tukihudumu katika Misheni ya Geneva Switzerland, Nilipewa mwito na kusimikwa kuwa rais wa tawi, na mke wangu alipewa mwito wa kuwa rais wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Pamoja tulifanya kazi kwa nguvu zetu zote ili kuimarisha tawi hilo lililokuwa na changamoto. Ingawa lilianzishwa miaka ya 1960, tawi hilo halikuwa na ubatizo wowote kwa miaka mingi na halikuwa limetuma wamisionari misheni kwa miaka 15.
Ilikuwa bayana kwamba tulihitaji usaidizi wa Bwana ili kupata suluhisho la changamoto nyingi ambazo zililikabili tawi hilo. Baada ya kuomba kuhusu changamoto za tawi hilo, Roho wa Bwana aliniambia, “Wafundishe waumini kusoma Kitabu Cha Mormoni, nawe utafanikiwa.”
Mara moja, tulifanya mipango ya kukubaliana na waumini wote waanze kusoma Kitabu cha Mormoni.
Matokeo ya ajabu yalifuata. Amani na Roho ilirudi katika tawi. Familia mpya zilijiunga na Kanisa. Kwa sababu ya kutiwa motisha na hamu ya kuhudumu, kijana mmoja aliondoka kwenda misheni. Ndoa kadhaa zilizokuwa na matatizo ziliimarishwa, na familia zikawa na umoja zaidi. Tawi hili linaendelea kupiga hatua leo.
Sisi na waumini katika tawi lile tulishuhudia wenyewe nguvu za kimiujiza za Kitabu cha Mormoni. Kwa kweli ni jiwe la katikati la tao la dini yetu na kwa ushuhuda wetu wa injili na wa Yesu Kristo. Tunakipenda kwa moyo wetu wote. Ni chanzo cha maarifa yasiyoisha na yasiyobadilika.
Tukio hili lilitufunza kuwa Kitabu cha Mormoni ni njia ya hakika kabisa ya kuwasaidia ndugu zetu na dada zetu kutoka katika vivuli vya giza la kiroho ambalo limeizingira dunia. Kitabu hiki kinaleta amani, shangwe, furaha, na hamu kubwa ya kumfuata Mwokozi Yesu Kristo.